Kuswali Na Viatu Vinavyovaliwa Ndani Ya Nyumba Inafaa?

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatullah wabarakatu

 

Huku ninakoishi kuna baridi sana, sasa majumbani kwetu kuna viatu ambavyo hutumika kutembelea ndani ya nyumba tu kwa sababu ya baridi, yaani ni twahara sasa ninaweza kuvitumia kuswalia.

 


 

 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuswali na viatu vinavyovaliwa ndani ya nyumba.

 

 

 

Hakika ni kuwa hata kama viatu hivyo vingekuwa vinavaliwa nje ya nyumba unafaa kuswalia maadamu ni twahara, havina najisi. Utwahara wa viatu ni kuwa vikavu.

 

Tufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wanaswali na viatu ambavyo walikuwa wanatembelea navyo ndani ya Msikiti. Na kwa ajili hiyo Mughiyrah bin Shu‘bah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha na kupangusa juu ya champali na viatu vyake” (Ahmad na at-Tirmidhiy).

Na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokewa na Abu Salamah Sa‘iyd bin Yaziyd aliyesema: “Nilimuuliza Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): Je, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali na viatu vyake”. Akasema: “Ndio” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa hiyo, waweza kuvaa hivyo viatu hata ikiwa hakuna baridi. Na hata ikiwa umetokwa na wudhuu baada ya kuwa umevivaa ukiwa nao, huna haja ya kuvivua bali waweza kupangusa juu yake wakati wa wudhuu kisha ukaswali navyo maadamu kabla ya kuvivaa ulikuwa ushatia nia ya kupangusa juu ya viatu endapo wudhuu utaondoka na kabla ya kuvivaa uwe umetia wudhuu kwa kuosha miguu kabla ya kuvaa viatu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share