Kutafuta Mke Au Mume Katika Mitandao Ya Kijamii Inajuzu?

 

SWALI:

 

Assalaam alaykum warahmatullah wabarakat, Jee inajuzu kisheria kuchagua mchumba kwenye website. Kwani nimeona katika website moja ya mafunzo ya kiislam wameweka sehemu ya kuchagua mchumba. Ni hilo tu, Asslam alaykum.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutafuta mchumba kwenye internet.

 

 

Kwa hakika hii inaonekana ni njia moja ya kutafuta mchumba, hivyo kuwashikanisha Waislamu walio mbali na kuwaleta pamoja.

 

Hakika Uislamu umeweka njia zake za kutafuta mchumba – mume kumtafuta mke na kinyume cha hayo. Hata hivyo, yapo matatizo ambayo yanapatikana katika suala hilo na hasa kukiwa hakuna udhibiti wa Kiislamu kuhusu suala zima la kutafuta mchumba. Mara nyingi hutokea udanganyifu kwani hamko karibu na inawasogeza watu kutojuana inavyopaswa na hiyo kupelekea ndoa hizo kutodumu.

 

Pia watu wasiwe na mawasiliano ya moja kwa moja bila usimamizi, na inapobidi wakutane, basi wasikutane peke yao bila kuwepo Maharimu zao pamoja nao. Hayo yote yanasaidia sana kuepusha Sharia’h kuvunjwa au watu kuingia katika maasi na haraam.

 

Suala nyeti ni kuwa wachumba hawa watajuaje kuwa mwenziwe ni mwenye Dini na maadili mema kama ilivyotakiwa na Shari’ah yetu ya Kiislamu. Hivyo, kukiwa na udhibiti na mume akaweza kupata maalumati kuhusu mchumba wake na kinyume chake na kuweza kukutana basi itakuwa haina neno. Lau itakuwa ni kinyume cha hivyo itakuwa ni suala ambalo halifai kwani madhara yake yatakuwa ni makubwa zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share