Kuanzishwa Swafu Mpya Katika Swalah Kabla Kujaa Iliyo Ya Mbele – Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Assalaamu 'Alaykum,

 

Kuna tatizo sugu misikitini mwetu la maamuma kuanzisha swafu mpya kabla ya iliyo mbele yake kujaa ikiwa amechelewa. Ni nini hukumu yake? Licha ya kukumbushwa mara kwa mara bado wanarudia.

 

Nimesoma katika kitabu cha Umdatus-Saalik kipo cha tafsiri ya Kiingereza (lakini asili yake ya Kiarabu bado pia imo) ambamo katika mlango wa mada hiyo, mwandishi ameongeza maelezo yake kwamba anayefanya hivyo hapati thawabu za jamaa tafadhali nifafanulie kwa idhini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ili tuwasaidie ndugu zetu.

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuanzishwa swafu mpya kabla ya mbele kujaa.

 

 

Kwa kuweza kufahamu suala hili ni muhimu kwetu sisi mwanzo twende katika Hadiyth na maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na umuhimu wa kuunga na kutengeneza swafu.

 

Wapo miongoni mwetu ambao hawaoni umuhimu wowote wa kutekeleza suala hilo na wengine hata huona ni usumbufu. Hata hivyo, ni jukumu na wajibu wa Imaam kuweza kuwaelimisha maamuma wake kuhusu hilo na hata kuhakikisha kuwa kabla ya kufunga Swalah amewakumbusha maamuma wake na kuhakikisha mwenyewe au kuwakilisha wasaidizi wake wasimamie kuhakikisha kuwa swafu zote zimebana na zimenyooka sawa sawa.

 

Hakika ni kuwa zipo Hadiyth nyingi zinazoelezea kuhusu umuhimu wa kuunganisha swafu, kujaza swafu za mbele kabla ya kuanza mpya na ujira wa hilo. Kinyume chake ni maangamivu ambayo yanaupata Ummah kwa kukaidi agizo hilo. Hebu tutazame baadhi tu ya Hadiyth kuhusu hayo:

 

1.  Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Lau watu wangejua yaliyomo baina ya mwadhini na swafu ya kwanza, kisha wasipate (swafu ya kwanza) ila kwa kuikimbilia basi wangefanya hivyo” (al-Bukhaariy na Muslim)

 

 

 

2.   Imepokewa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah na Malaika Wake wanawaombea wenye kuswali katika swafu, na mwenye kuziba upenyo (nafasi) Allaah anamnyanyua daraja yake” (Ahmad, Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan).

 

 

3. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliusia: “… Wala msiache upenyo kwa Shaytwaan, na mwenye kuunganisha swafu, Allaah Humuunganisha na mwenye kuikata, naye Hukatwa na Allaah” (Ahmad na Abu Daawuud, na kusahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy).

 

 

 

4.  Imepokewa na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Kulikimiwa Swalah, naye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatukabili kwa uso wake, akasema: “Tengezeni swafu zenu, kwani mimi nawaona nyuma ya mgongo wangu” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

 

 

5.  Imepokewa na Jaabir bin Samurah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alitutokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Je, hamupangi swafu kama wanavyopanga Malaika mbele ya Mola wao Mlezi?” Tukasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Na Malaika wanapanga vipi swafu mbele ya Mola wao Mlezi?” Akasema: “Wanatimiza swafu za kwanza na wanazipanga sawasawa” (Muslim).

 

 

 

6.  Imepokewa na Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Tengezeni swafu zenu kwani katika kutengeza swafu ni katika kusimamisha Swalah” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

 

 

7.  Na imepokewa na an-Nu‘man bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtaendelea kuweka swafu sawa au Allaah Atazibadilisha nyuso zenu” (al-Bukhaariy na Muslim). Na katika riwaya ya Ahmad na Ibn Hibbaan: “… au Allaah Atazibadilisha nyoyo zenu”.

 

Hakika ni kuwa Imaam Ibn Maajah ana mlango katika Sunan yake wa 54 ambao ameupatia kichwa cha habari, “Mlango wa Swalah ya Mtu Nyuma ya Swafu Peke Yake”. Katika mlango huo ameelezea Hadiyth mbili, nazo ni kama zifuatazo:

 

 

 

1.  Imepokewa na ‘Aliy bin Shaybaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), aliyekuwa miongoni mwa mwakilishi wa watu wake: “ Kisha tukaswali Swalah nyingine nyuma yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alipomaliza Swalah, alimkuta mtu akiswali peke yake kwenye swafu. Mpokezi akasema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimngojea mpaka alipomaliza Swalah, kisha akamwambia: ‘Rudia Swalah yako, kwani hakuna Swalah kwa yule anayeswali nyuma ya swafu (peke yake)”. Kulingana na az-Zawaa’id, isnadi yake ni Hasan.

 

 

 

2. Waabiswah bin Ma‘bad (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Mtu mmoja aliswali peke yake nyuma ya swafu, hapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuamuru airudie (Swalah hiyo)”.

 

 

 

Inabidi mtu ahakikishe kuwa hakuna nafasi kabisa kwenye swafu ya mbele yake ndio aanzishe swafu nyingine au aweze kuswali pekee kwenye swafu nyingine, na hali hiyo ya kuswali pekee baada ya kuhakikisha kuwa hakuna nafasi kwenye swafu ya mbele ni hali ya dharura na inakubalika baada ya kuwa mtu amekwisha hakikisha kuwa hakuna hta nafasi ya kujibana kwenye swafu ya mbele yake.

 

Makusudio ya Hadiyth hizo mbili hapo juu yapo kwenye jibu jingine ndani ya kiungo hiki:

 

Kuanza Swafu Ya Nyuma Kwa Kumvuta Mtu Wa Mbele Katika Swalah Ya Jamaa

 

 

Kwa hiyo, inabidi maamuma wafundishwe umuhimu wa kupanga swafu sawa, kutoanzisha swafu mpya kabla ya mbele kujaa na kutoswali mtu peke yake bila dharura na madhara yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share