Iweje Haifai Kusomewa Du'aa Na Mtu Na Hali Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) Aliwaombea Watu Du'aa?

SWALI:

 

Assalam Aleykum,

 

Nimesoma makala kuhusu masuala ya kusoma dua.  Kwa kweli kama nimeelewa vizuri mnasisitiza mtu asome dua yeye mwenyewe na si kusomewa na shehe.  Katika maelezo mliyotoa mwishoni kuna sehemu ambazo mnarefer watu waliomwendea mtume (S.W.W) kumuomba awasomee dua, na baadhi walisomewa dua na watu wengine ambao tu ni washika ibaada akiwemo yeye mtume wetu (S.W.W.) alisomewa na swahaba (R.A.)

 

Sasa nilidhani mnazuia mtu kusomewa dua na mtu mwingine (especially shehe) sasa mbona mtume aliwasomea watu dua?  Mimi concern yangu ni kwamba mtu asome dua yeye mwenyewa kadri awezavyo (atakavyojaaliwa) na ni jambo la kheri LAKINI PIA MTU ANAPOHITAJI MAOMBI YA DUA KUTOKA KWA MTU MWINGINE AMBAYE YEYE ANAONA/ANAAMINI KUWA KWA ULE UPAMOJA ALLAAH ATAISIKIA DUA YAKE (SIMAANISHI KWAMBA AKIOMBA YEYE MWENYEWE HAIPOKELEWI, LA!) bali ni katika kufanya mambo mengi ya kujikurubisha kwa Allaah.  Kusoma mwenyewe na pia wakati mwingine kuwaita wale unaowadhani ni sawa kwako kuwaita wakaja kusoma dua kwako au pamoja nawe.

 

Hapo haijalishi kama huyo aliyeitwa kusoma dua ni Shehe au ndugu yako mwingine yeyote (amemuamini) maana sisi sote tu wanaadamu na tuna madhaifu yetu (dhahiri na ambayo si dhahiri) huenda yule umdhaniaye mzinzi, mlevi etc analingana tu na yule umdhaniae bora (kwa maana hata huyo bora ni mzinzi wa siri labda wewe/nyinyi hamjui etc).  Hapa nadhani ni ile nia yako ya kusoma dua kwa Allaah sadaka yako unayoitoa na imani yako katika kile unachokifanya.  Hapa namaanisha imani yako kwamba unayemuomba dua SI SHEHE AU NDUGU YAKO MCHAMUNGU ALIYEPO HAP, LA!  BALI UNAYEMUOMBA NI ALLAAH MMOJA TU.

 

Nawaomba ndugu zangu katika uislam mnieleweshe hapo juu kama nimekosea maana nina imani na nataka kuwaita watu (ninaowaamini) kwa ajili ya kusoma dua ya pamoja katika nyumba yetu mpya.  Ni kosa?  Ni dhambi?  Au? Ahsanteni sana na Mwenyezi Mungu awabarik

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuombewa du’aa na wengine unaoamini kuwa ni wema na wazuri.

‘Ibaadah ni jambo ambalo linafanywa ili kumleta karibu mja na Mola wake Mlezi. Ndio kwa ajili hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Du’aa ni Ibaadah” (at-Tirmidhiy na wengineo). Kwa sababu Du’aa ni ‘Ibaadah ni lazima ifanywe kwa njia anayotaka Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), sio namna tutakavyo sisi.

 

Inavyoonekana ni kuwa labda hukielewa vyema makala hiyo. Kwa mujibu ya Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba du’aa peke na hivyo ndivyo walivyofanya Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum). Na kwa ajili hiyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hapendwi na Allaah asiyemuomba”.

 

Ama kusomeana du’aa baina ya watu kwa kukusanyika katika nyumba moja au sehemu moja haijapatikana kabisa katika maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake. Ama ile Hadiyth inayosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaka ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) asimsahau katika du’aa zake njema wakati alipokuwa anasafiri. Hii ni Hadiyth sahihi kabisa inayotufundisha Sunnah ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tuwe ni wenye kuwaomba wanaosafiri kwani du’aa ya msafiri inakubaliwa na Allaah Aliyetukuka. Kwa njia hiyo hakuna makosa kabisa kwani imepatikana dalili hiyo katika uongofu wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na huyo mtu wa kukuombea ambaye ni si lazima awe Shaykh, unaweza kumuambia yeyote kwani hujui nani ni mwenye taqwa zaidi kuliko mwengine. Hivyo, kuombeana du’aa baina ya Waislamu ni jambo ambalo ni zuri lakini si kukusanyika katika nyumba au sehemu nyingine. Linalofaa ni kila mmoja kumuombea mwenziwe kwa wakati wake tena kwa siri na hasa katika nyakati ambazo du’aa inakuwa ni yenye kukubaliwa na Allaah Aliyetukuka.

 

Ama kuhusu sisi Waislamu tunatakiwa tuwe na dhana nzuri mmoja kwa mwengine kama ndugu. Ikiwa mtu anafanya madhambi kwa dhahiri inafaa kwa Waislamu wenziwe wawe ni wenye kumuusia aache madhambi hayo na awe ni Muislamu mwema. Hatufai sisi kama Waislamu kuwa na dhana mbaya baina yetu kwani jambo hilo huleta husuma, hasadi na chuki baina ya ndugu. Mas-ala ya kudhaniana yaondoke kabisa baina yetu kwani jambo hilo na sifa hiyo inamuweka mtu pabaya sana. Muislamu yeyote unayemuona katika Msikiti mara kwa mara inatakiwa umshuhudilie kuwa ni mwema kama anavyotuambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na umuachie siri zake kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Ama kuhusu kuingia katika nyumba mpya inatakiwa usome du’aa hii kama tulivyofundishwa: “Allaahumma inniy as’aluka khayraha wa khayra maa jabaltahaa ‘alayhi wa a’udhu Bika min sharrihaa wa sharri maa jabaltahaa ‘alayhi” (Abu Daawuud na Ibn Maajah).

Na nyingine ni:

“Kwa jina la Mwenyezi Mungu tunaingia, na kwa jina la Mwenyezi Mungu tunatoka, na Mola wetu tunamtegemea” (Abu Daawuud na Ibn Baaz katika Tuhfatul Akhyaar, uk. 28)

Kisha unatoa salaam hata kama hakuna watu.

 

Na hilo la kuita watu kuja kusoma du’aa na kula chakula, hakuna mafundisho yaliyopatikana kuhusiana nayo.

 

Na katika kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka ni kufanya ya faradhi na kuongeza ‘Ibaadah nyingine za Sunnah.

 

Na Muislamu mzuri mwenye mapenzi ya kweli kwa Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni yule anayemuiga matendo yake na kufuata mafundisho yake na kuacha ambayo hakuyaleta wala kuyafundisha.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 
Share