Alishika Dini Alipokuwa Hana Kazi Sasa Hana Muda Wa Kufanya ‘Ibaadah Na Anapotoa Nasaha Anaonekana Mjeuri

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum warahmatullahi wabarakatuh - rehma za allah subhanahu wataala ziwe juu yenu. amin.

 

mimi ni mwanamke, nlikua nimeshika dini sanaa wakati nlipokua sijapata kazi, saivi nimepata kazi najitahidi nipate muda wa kusoma quran na kufanya ibada zangu nyingi lakini naposhika quran au kutaka kusoma tasbihi naingiwa na usingizi..wallah najitahidi kuongea na watu maneno mazuri anayopenda allah subhanahu wataala bado naambiwa mie mjeuri kwa kua watu wengi hawaapendi uwaendee kinyume na wanavotaka wao uende...nalia na naumia sana kuwa mbali na dini yangu na najiona nateseka sana sijui nifanyeje!

nataka niwe nauliza maswali yangu humu kwa wingi lakini yanachelewa kujibiwa basi hua sina mwengine wa kumwambia please nawaomba musichelewe kunijibu ndugu zanguni napata shida sana...ahsante.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kushika Dini wakati ambao ulikuwa huna kazi na kudorora katika ‘Ibaadah baada ya kupata kazi.

Awali ya yote tunasikitika kuona maswali yako yanachelewa kujibiwa lakini hilo liko nje ya uwezo wetu kwani maswali yanayokuja ni mengi. Na mfumo wetu wa kujibu ni kuanza na yale yaliyoletwa mwanzo kabla ya kuja kwa mengine. Huenda kuwa ulipotuma yalikuwa mengi na hatuwezi kuanza na yaliyochelewa na kuacha yaliyotumwa mwanzo. Kwa kila hali, tutajitahidi kufanya bidii ili tuweze kuyajibu kwa muda unaofaa, InshaAllaah.

 

Ama tukija katika swali lako ni kuwa kwa kila hali mwanaadamu na hasa Muislamu huwa anajaribiwa na Allaah Aliyetukuka kwa mitihani tofauti. Kukosa kazi ni mtihani na hivyo hivyo kupata kazi. Hata hivyo, sisi Waislamu tunatakiwa katika hali yoyote ile tuwe tunashikamana na Dini yetu kama inavyotakiwa. Ndio Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

Ajabu kwa mambo ya Muumini, hakika mambo yote kwake ni kheri. Na hilo halipatikani ila kwa Muumini: Anapopatikana na furaha hushukuru na hiyo ikawa kheri kwake na anapopatikana na madhara husubiri, na hilo likawa kheri kwake” (Muslim).

 

Kila mtu tufahamu kuwa hupata Imani kwa kadiri ya Imani yake, na katika daraja hiyo ni Mitume na Manabii (‘Alayhimus Salaam) ambao mitihani yao ni mikubwa zaidi. Ni ada kwa wengi wanapokuwa hawana kazi au ni masikini kufanya ‘Ibaadah kwa wingi na kumuomba Allaah Aliyetukuka Awaondolee shida hiyo lakini pindi wanapopata kazi au kutajirika, basi humsahau Allaah moja kwa moja.

Jambo hili hutokea kwa sababu ya ukosefu wa Ikhlaasw na na Niyah njema. Mara nyingi unamuomba Allaah Aliyetukuka na kumuabudu ukingoni, mguu mmoja kwa Allaah na mwengine kwa Shaytwaan. Kwa ajili hiyo, Allaah Aliyetukuka Akatuambia:

Na katika watu wapo wanaomuabudu Allaah kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi” (Al-Hajj 22: 11).

 

Kazi inatakiwa isimtoe mtu katika kufanya ‘Ibaadah. Ikiwa itakuwa hivyo, itakuwa afadhali kwa Muislamu aache kazi kuliko kuwa na kazi ambayo itampatia hasara hapa duniani na Kesho Akhera. Allaah Aliyetukuka Anatuzungumzia kuhusu Waumini wa kweli kweli:

Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Allaah, na kushika Swalah, na kutoa Zakaah. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho zitageuka” (An-Nuur 24: 37).

Na Akasema,

Na itakapokwisha Swalah, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Allaah, na mkumbukeni Allaah kwa wingi ili mpate kufanikiwa” (Al-Jumu‘ah 62: 10).

 

Kwa ajili ni lazima ufanye bidii na juhudi kubwa ya kuweza kufanya ‘Ibaadah, kwani kazi yako haitakuwa na baraka ikiwa hutamkumbuka Allaah Aliyetukuka. Kuongea na watu ni vizuri, hata hivyo unatakiwa ujirekebishe kwa kutekeleza ‘Ibaadah. Na njia rahisi ya kuweza kudumu katika ‘Ibaadah ni kuwa na marafiki wema, wazuri na walioshika Dini; kuwa na wakati wa kusoma Qur-aan, kujua maana yake na kujaribu kutekeleza. Na ukianza kusoma usisahau kujilinda kwa Allaah Aliyetukuka kutokana na Shaytwaan aliyelaaniwa. Jaribu kuleta Adhkaar za asubuhi na jioni na kabla ya kumpatia Muislamu mwenzio mawaidha, mwanzo jaribu kabisa kujirekebisha na kulifanyia kazi hilo ambalo una kasoro nalo. Kiburi na ujeuri vinaletwa na kuhisi kuwa wewe ni mkubwa wa daraja na hakuna akufikiyae kwa daraja na cheo. Kuondoa kiburi na ujeuri, jaribu kukaa na masikini, kuzungumza nao na wale ambao hawana kazi kwani wakati mmoja ulikuwa pamoja nao na ulikuwa na adabu aliyotufundisha Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kuumia kwa kuambiwa wewe ni mjeuri na ikiwa si hivyo, hilo ni jambo la kawaida. Hata hivyo, ukitazama kuumia kwako pia angalia jinsi gani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoudhiwa mpaka akaambiwa kuwa yeye ni mchawi, mwenda wazimu na kadhalika.

Huo ni mtihani ikiwa huna sifa hiyo na ikiwa unayo basi fanya bidii ujirekebishe kabisa kuhusu hilo. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

Hapana shaka Tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri” (Al-Baqarah 2: 155).

 

Katika mtihani huo wako unatakiwa usubiri na uzidishe ‘Ibaadah ili upate kushinda na kufaulu.

 

Tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka na wewe nawe zidi kuomba ili upate kuupita mtihani ulio nao na uweze kurudi katika ‘Ibaadah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share