Afanye Nini Ili Allaah Amsamehe Dhambi Na Aweze Kujikuribisha Kwake?

 

SWALI:

NAOMBA MUNIJUILISHE KITU GANI NIFANYE ILI NIWEZE KUNIKURUBISHA KWA MOLA WANGU NA ANIGHUFIRIE DHAMBI ZANGU. AU AMALI GANI NIFANYE ILI NIPATE HAYO


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kuhusu kufutiwa dhambi zako madamu una nia ya kutubia, jambo hili halina shaka kabisa kuwa lina uwezekano kwani dalili zake nyingi mno katika Qur-aan na Sunnah.  Maswahaba walitia shaka kuhusu madhambi yao waliyotenda kabla ambayo ni makubwa zaidi kuliko yako nayo ni kuwa walikuwa ni wenye kumshirikisha Allaah kabla ya Uislamu. Lakini walipotaka ufafanuzi kuhusu madhambi yao, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akateremsha Aayah ifuatayo:

(( قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَى أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ))  

((Sema: Enyi waja  Wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na Rahma ya Allaah. Hakika Allaah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu))  [Az-Zumar: 53]

 

Tafadhali ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo mengi mno kuhusu Tawbah ili upate kuridhika nafsi yako ikiwa utatubia kweli  na uweze kubakia katika radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

Tawbah

Ama kuhusu kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), ni amali nyingi kabisa zisizokuwa na hesabu. Jambo la kwanza kabisa ni kutimiza Swalah zako tano kila siku. Kiungo kifuatacho pia kina maelezo marefu yatakayokupa umuhimu, fadhila na faida za Swalah, ambayo pindi ukiitimiza ipasavyo utaweza kuzidi kujiepusha na maouvu.

Swalah

Kisha fanya mema mengi ambayo yatafuta maovu yako na pia yatazidi kukurubisha kwa Mola wako Mtukufu kwani mema hufuta maovu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ذَلِكَ ذِكْرَى لِلذَّاكِرِينَ))

((Hakika ya mema huyaondosha maovu)) [Huud: 114]

Amka usiku katika thuluthi ya mwisho ya usiku uswali Tahajjud na umuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusamehe madhambi yako na Akuongoze.

Jishughulishe na kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kila mara asubuhi na jioni, kwa kusoma Qur-aan, kusikiliza mawaidha, kutafuta elimu ya Dini yako, yote haya yatakupa faida ya dunia na Akhera. Elimu na manufa yote haya yanapatikana Alhidaaya, tembelea na fuata nasaha zetu ili Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuhidi katika njia iliyonyooka.  .  

Tunatumai kwamba utafuata nasaha zetu za dhati hizo na tunakuombea at-Tawfiyq na uongofu kutoka kwa Mola Mtukufu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share