Manufaa Gani Ya Ulevi Yaliyotajwa Katika Qur-aan Na Madhara Ya Kamari

 

 

Manufaa Gani Ya Ulevi Yaliyotajwa Katika Qur-aan Na Madhara Ya Kamari

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalaamu alaikum warrahmatullahi wabarakatu, Katika suratul-bagarah ayah ya 219 inasema: Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Swali langu ni hili: manufaa gani

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Katika Aayah hii kuna msingi mkubwa wa kuharamishwa kwa vitu hapa duniani. Na hakika ni kuwa kujua kwetu hekima kuhalalishwa au kuharamishwa vitu si muhimu kwani tunajua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anahalalisha vizuri na kuharamisha vibaya. Vilivyo haramu vina madhara kwetu na halali ni maslahi kwetu. Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akatuambia:

 

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿١٥٧﴾

157. Wale wanomfuata Rasuli; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza munkari, na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu, na anawaondoshea mizigo yao (shariy’ah ngumu) na minyororo (vikwazo, taklifu) ilokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini na wakamtukuza, na wakamnusuru na wakafuata nuru (Qur-aan) ambayo imeteremshwa pamoja naye; hao ndio wenye kufaulu.  [Al-A’raa: 157]

 

 

Ama manufaa madogo ya kamari na vileo ni hapa hapa duniani. Manufaa ya kamari ni:

 

  1. Kupata fedha kwa njia nyepesi na kuzitumia kwa mahitaji yake ya kibinafsi na familia.

 

 

Ama manufaa ya vileo (pombe) ni kama yafuatayo:

 

  1. Kudhaniwa na wanywaji kuwa inatoa dhiki na fikira kwa muda
  2. Kutumika kuhifadhia baadhi ya vyakula.
  3. Kusafisha sehemu za jeraha na kuua viini.
  4. Kuondosha kinyesi.
  5. Kudhaniwa na wanywaji kuwa inasisimua.
  6. Kutumika katika mafuta aina ya virashio na manukato.

 

 

Hata hivyo, manufaa haya yanazidiwa na madhara yake mengi yaliyo dhahiri na yanayoathiri Dini, jamii na akili. Tunataja machache hapa:

 

 Madhara ya kamari ni kama:

 

  1. Kupoteza pesa kwa kushiriki kwenye mchezo huo ambao mara nyingi mtu hushindwa na huliwa pesa zake.
  2. Kuingia kwenye uraibu wake na kujikuta kila wakati unapotezea muda huko na kushughulishwa nayo na kuacha ya muhimu ya ‘Ibaadah na familia.
  3. Kufilisika.

 

Ama madhara ya pombe ni kama yafuatayo:

 

  1. Kuacha nguzo za fardhi kama Swalaah, Swawm n.k.
  2. Kukosa hayaa, heshima, ustaarabu, na kufanya matendo ya kipuuzi mara nyingi.
  3. Kutoa maneno maovu, matusi.
  4. Kugombana na watu.
  5. Kutoa harufu mbaya mdomoni.
  6. Kuharibu ndoa kwa kukosa kutimiza haki za mke na watoto.
  7. Madhara kadhaa ya kuathiri afya ya mtu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share