Tofauti Baina Ya Muumin Na Muhsin

 

SWALI:

 

Ni nini tofauti kati ya mtu ambaye ni Muhsin na Muumin?

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu tofauti baina ya Muumini na Muhsin.

 

Hakika hizi ni daraja na cheo ambacho Muislamu hupanda. Mwanzo mtu huwa ni Muislamu (Muslim), kisha akawa Muumini yaani Imani imeongezeka na baadaye kuwa Muhsin. Muhsin kilugha maanake ni kuwa mwema, na Muhsin ni yule aliyezidi kimatendo kuliko wengine.

 

Muislamu ni yule aliyefanya juhudi katika kutekeleza nguzo za Uislamu, ilhali Muumini ni yule aliyezitekeleza nguzo za Uislamu na Imani. Na Muhsin ni yule anayemuabudu Allaah Aliyetukuka kama kwamba anamuona na ikiwa hamuoni basi Allaah Anamuona. Haya yanaelezewa katika Hadiyth ndefu ya ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) pale Jibriyl alipokuja kuwafundisha Dini na akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu maana ya Uislamu, Imani na Ihsaan (Muslim)

 

عن عُمَر رضي اللهُ عنه أَيْضاً قال:   بَيْنَما نَحْنُ جُلْوسٌ عِنْدَ رسُولِ الله صلى الله عليه وسلم ذات يَوْم  إذْ طَلَعَ عَلَيْنَا رَجُلٌ شَدِيدُ بَياضِ الثِّيَاِبِ شَديدُ سَوَادِ الشَّعْرِ، لا يُرَى عليه أَثَرُ السَّفَرِ ولا يَعْرِفُهُ مِنَّا أَحَدٌ، حَتى جَلَسَ إلى النَّبِّي صلى الله عليه وسلم، فأسْنَدَ رُكْبَتَيْهِ إلى رُكْبَتَيْهِ ووَضَعَ كَفَّيْهِ على فَخِذَيْهِ، وقال: يا محمَّدُ أَخْبرني عَن الإسلامِ، فقالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم:(( الإسلامُ أَنْ تَشْهَدَ أَنْ لا إلهَ إلا اللهُ وأَنَّ محمِّداً رسولُ الله، وتُقِيمَ الصَّلاةَ، وتُؤتيَ الزَّكاةَ، وتَصُومَ رَمَضان، وتَحُجَّ الْبَيْتَ إن اسْتَطَعتَ إليه سَبيلاً)). قالَ صَدَقْتَ. فَعَجِبْنا لهُ يَسْأَلُهُ ويُصَدِّقُهُ، قال : فَأَخْبرني عن الإِيمان. قال: ((أَن تُؤمِنَ باللهِ، وملائِكَتِهِ وكُتُبِهِ، ورسُلِهِ، واليَوْمِ الآخِرِ، وتُؤمِنَ بالْقَدَرِ خَيْرِهِ وشَرِّهِ)) قال صدقت. قال : فأخْبرني عَنِ الإحْسانِ. قال:(( أنْ تَعْبُدَ الله كَأَنَّكَ تَرَاهُ فإنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فإنَّهُ يَرَاك)). قال: فأَخبرني عَنِ السَّاعةِ، قال: ((ما المَسْؤولُ عنها بأَعْلَمَ مِنَ السَّائِلِ )). قال: فأخبرني عَنْ أَمَارَتِها، قال:(( أن تَلِدَ الأمَةُ رَبَّتَها، وأَنْ تَرَى الحُفاةَ العَُراةَ العالَةَ رِعاءَ الشَّاءِ يَتَطَاوَلُونَ في الْبُنْيانِ )) ثُمَّ انْطَلَقَ، فَلَبِثْتُ مَلِيّاً، ثُمَّ قال : ((يا عُمَرُ، أَتَدْرِي مَنِ السَّائِلُ؟)) قُلْتُ: اللهُ ورسُولُهُ أَعلَمُ . قال:(( فإِنَّهُ جِبْرِيلُ أَتاكُمْ يُعَلِّمُكُمْ دِينَكُمْ))   رَوَاهُ مُسْلِمٌ

 

Kutoka kwa 'Umar رضى الله عنه  ambaye amesema: Siku moja tulikuwa tumekaa na Mtume صلى الله عليه وسلم  , hapo alitokea  mtu ambaye  nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana; hakuwa na alama  ya machofu ya safari na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtumeصلى الله عليه وسلم akaweka magoti yake karibu na magoti yake (Mtume) na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake kisha akasema; Ee Muhammad! Niambie kuhusu Uislamu.  Mjumbe wa Allaah  صلى الله عليه وسلمalisema:  Uislamu ni kukiri kuwa hakuna mola isipokuwa  Allaah na Muhammad ni Mjumbe wake, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji (Makkah) ukiweza.  

(Akasema yule mtu yaani Jibriyl) Umesema kweli. Tulipigwa na mshangao kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha.  Na akasema tena: Niambie  kuhusu Iymaan.  Akasema (Mtume صلى الله عليه وسلم) Ni kumwamini Mwenyeezi-Mungu, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Qiyaama, na  kuamini ya kuwa kheri na shari zinatoka Kwake (Allaah سبحانه وتعالى  ). (Akasema Jibriyl): Umesema kweli, akasema hebu nielezee kuhusu Ihsaan.  Akasema Mtume صلى الله عليه وسلم   Ni kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى   kama vile unamuona na kama humuoni basi Yeye Anakuona.  Akasema (Jibriyl):  Niambie    kuhusu Qiyaama.  Akajibu (Mtume  صلى الله عليه وسلم : Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile Muulizaji. Kisha akamwambia: Nijulishe alama zake: Akajibu (Mtume صلى الله عليه وسلم): Kijakazi atazaa bibi yake, na utaona wachunga wenda miguu chini, wenda uchi (wasio na uwezo wa kumiliki hata mavazi), mafukara (wasiokuwa hata na sehemu ya kuishi kwa umaskini) wakishindana kujenga majumba ya fahari. Kisha akaondoka (Jibriyl) na nilitulia kidogo (nikitafakari). Kisha akasema Mtume صلى الله عليه وسلم : "Ewe 'Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza? Nikasema: Allaah na Mjumbe wake wanajua zaidi.  Akasema Mtume   صلى الله عليه وسلم: Ni Jibriyl, alikuja kuwafundisha dini yenu.

 

Pia tazama Riyaadh asw-Swaalihiyn, Hadiyth namba 60).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share