Kisa Cha Anfaal - Laiti Ningelijua ........

 

  Kisa Cha Anfaal – Laiti Ningelijua……

 

         Imefasiriwa na Ummu ‘Abdul-Wahhaab   

 

 

 Alhidaaya.com

 

 

Anfaal, msichana wa kitajiri, alikaa bila ya stahamala katika chumba cha daktari akisubiri matokeo ya vipimo vyake. Alikuwa na haraka ya kuhudhuria sherehe na alihofia huenda akachelewa kwenye miadi yake ya kutengeneza nywele. Kabisa hakufikiria yale matokeo kwamba huenda yakawa na kitu muhimu. Ilikuwa ni tahadhari tu iliyotiliwa mkazo na familia yake.

 

Hakuwahi kusumbuliwa na maradhi yoyote makubwa, mbali na maumivu madogo madogo ya mwili. Baadae ilikuwa zamu yake kumuona daktari.  Alifanya haraka iwezekanavyo kuingia ndani.  Alishangaa kumuona daktari akiwa mwenye huzuni na aliguswa zaidi pale alipoulizwa, "Hii ni yako?"

 

Alijibu, "Hapana, ni ya mwanangu."

 

Alitaka kujua ukweli na alifikiri kwamba labda daktari angeweza kuuficha ukweli, pindi akimwambia kuwa ni yake yeye mwenyewe. Alimtaka akae, hivyo alikaa huku akihisi aina fulani ya woga. Alimuangalia daktari kwa wasiwasi, pale aliposema.

 

"Kwanini hukumtuma mwanamme kuchukuwa matokeo?"

 

Anfaal akasema, nilikuwa najia njia ya huku kwa hivyo hakukuwa na haja ya kumtuma mtu yoyote."

 

Daktari alimwangalia kwa huzuni akisema, "Inaonyesha wewe ni msichana mwenye elimu.  Unaeelewa asili ya uhai."

 

Alinyamaza, hapo Anfaal alianza kutetemeka.

 

Akauliza, "Una maanisha nini daktari?"

 

Daktari akasema, "Matokeo yanaonyesha kwamba kuna ugonjwa kwenye damu." Aliziangalia zile karatasi na akabakia kimya. Anfaal alitakiwa amuulize ili afahamishwe zaidi.  Alilia kwa woga, "Ni Saratani (cancer)?"

 

Hakumtizama, wingu la huzuni liliziba uso wake. Ilikuwa kama aliyemhukumu kifo.

 

Alisema katika sauti ya kuvunjika moyo, "Nimekwisha!" Hapo daktari alitambua kwamba alikuwa amesema uongo, lakini ilikuwa amechelewa kuuficha ukweli. Alimuangalia kwa huruma na kumwambia, "Pole. Kwanini ulisema uongo? Hata hivyo uhai na kifo vimo ndani ya Uwezo ya Allaah.  Wapo wagonjwa wengi wanaoishi muda mrefu na wenye afya wakafariki mapema."

 

Anfaal alihisi kama aliyekuwa anazama, kama kwamba kuna ngumi nzito inayokandamiza moyo wake. Alijaribu kujikaza ili arudishe nguvu, akasema, "Naomba radhi.  Ahsante daktari."

 

Daktari alimpa moyo akisema, "Kuwa mwenye nguvu na matumaini mema.  Sayansi ya utibabu inaendelea kukuwa. Yale magonjwa yasiyoweza kutibika leo yanaweza kutibika kesho, bado nina matumaini. Niwachie namba yako ya simu."  Aliikariri namba yake ya simu bila ya kutambua nini anachokisema.  Huku akihisi mshituko mkubwa na uchungu, alimshukuru tena daktari na kuondoka.

 

Alipokuwa nyumbani aliuficha ukweli. Hakujua jinsi ya kuishirikisha (kadhia ile).  Hata hivyo, kila mtu alikuwa kashughulika, tayari kwa sherehe. Mama yake aliuliza, "Je ulikuwa kwa daktari? Kwanini hukwenda kutengeneza nywele?"  Lilikuwa ni suala la mpito tu lisilohitajia jawabu. Kwa ufupi alisema, "Siendi kwenye sherehe!"

 

Alipanda juu kwenye chumba chake na kujifungia mlango.

 

Alijinyoosha juu ya kitanda chake akiwa na nguo zake zote huku akisikiliza sauti za familia yake, kama kwamba zilikuwa zikitokea sehemu ya mbali.  Aliuhisi upepo unamvumia kwa sauti ya huzuni ya mauti, ukimlilia kuwa anakaribia kifo.  Alikihisi chumba kuwa ni kigeni kwake kama kwamba punde angelikiwacha. Vipi kuhusu nyumba? Isingeweza kumkumbuka. Alikuwa kama mgeni. Wengine watachukua chumba chake na kumsahau.  Alijaribu kulia lakini machozi hayakumsaidia.

 

Kwa uchungu aliangalia vilivyomzunguka.  Mapazia yote aliyojaribu kuyapata kwa taabu, yatabaki. Haitojalisha ikiwa yalitengenezwa kwa kitambaa kisichopatikana kwa urasihi, atayawacha kwa ajili ya wengine.  Alitamani laiti asingelijitaaabisha nafsi yake kwa ajili ya kitu kile. Alitamani laiti angelijiwekea hakiba ya wakati wake na fedha zake kwa vitu vya manufaa, ambavyo vingeweza kumsaidia wakati wa dhiki kama huu.

 

Alishangaa, "Ni kitu gani muhimu kwangu?" Alikuwa msichana mrembo na tajiri mwenye kila kitu ambacho moyo wake ulitamani. Kuna chochote kati ya hivyo kingeweza kumnusuru kutokana na kifo? Daima aliutumia muda wake mrefu kwenye kazi mashuhuri yenye mshahara mzuri. Bado alikuwa nayo hiyo kazi, lakini ingeliweza kumnusuru ili aepukane na kifo?

 

Wazo lilimjia, Aliharakia kwenye simu ambapo kila mtu alikuwa hayupo.  Alimpigia simu daktari na kumuuliza kwa bidii, "Je nitaweza kupata tiba ikiwa nitasafiri kwenda nje?"

 

Daktari alisema, “Hakuna jipya nje, ila ni kupoteza pesa tu.”

 

Aliweka simu chini akakaa kwenye kiti kilicho karibu nae.

 

Mshahara wake au mali yake haikuweza kubadilisha jambo. Alitembea kwenye vyumba vyote kama kwamba anaaga.  Alitembea kwenye bustani ndogo akaiangalia miti huku akinong’ona, “Natamani hii miti ingelielewa kuwa naondoka, mawe yote, kuta….. Natamani hii milango ingelijua kuwa karibuni mikono yangu haitoifungua tena. Natamani mauwa yote ambayo niliyapandisha na kuyamwagilia maji yangeelewa. Mara ngapi miba na mawe magumu yalinichoma mikono yangu? 

 

Mara ngapi nilimwagilia mauwa yaliyonyauka kwa machozi yangu pindi maji yakikosekana. Natamani yangeelewa nini maana ya kuondoka duniani. Hii miti ya matunda ilikuwa midogo nilipoipandisha, nilijitahidi kadiri ya uwezo wangu kuinawirisha mpaka imekomaa na kutoa matunda. Je inaelewa kama karibuni nitaondoka? Itakumbuka masiku nilipokuwa pamoja nayo? Je na hivi viti nilivyokuwa navitumia kwa kupumzikia, vitapungukiwa kwa kutokuwepo kwangu? Je vipo tayari kwa mtu mwengine kuja kuvikalia? Na hizi dhahabu na mapambo ya thamani na fakhari yatanisaidia huko niendako? Je hizi nguo za kila aina ya mitindo zilizojaa makabatini zitanisaidia? Pia hii TV kubwa kama sinema ambalo hujiburudishia kwa kuangalia miziki na yote yaliyoharamishwa litanisaidia? Je vyote hivyo vitapungukiwa nitakapoondoka?  Natamani vyote hivyo vingelijua kuwa naondoka duniani. Natamani kama vyote hivyo vingenisaidia huko niendako. Lakini la!  Vyote hivyo viko tayari kuja kurithiwa! Llaiti ningeliyajua hayo nisingeliyajali maisha haya.  Nisingelihisi fakhari na kiburi…….

 

Laiti ningelijua kwamba mimi ni mgeni katika ulimwengu huu, nisingelidanganya wala kutamani anasa zake …….!

 

Laiti ningeliyajua haya kwamba kuishi maisha mepesi ni rahisi kuliko kuishi maisha ya anasa….!

 

Laiti ningeliishi maisha mepesi, nisingeliona taabu kuyavuka maisha ya ulimwengu huu na kwenda kuishi maisha mengine.  Familia yangu hivi sasa inaburudika na sherehe.  Ni mara ngapi nimerefusha wakati wangu katika sherehe kama hizi! na kwa kiasi gani nilishughulikia mitindo ya mavazi na nywele!  Vinaweza kunisaidia?

 

Anfaal alijikalisha kwenye kiti cha karibu yake kama kwamba aliutambua ukweli ambao hapo awali hakuujua.

 

Alisema, "Ni nini nichukuwe?  Hamna isipokuwa sanda na amali zangu. Aina gani ya amali zitakazokwenda na mimi katika safari yangu ndefu? Hamna!  Naam, hamna!" Alimkumbuka rafiki yake Sarah, ambaye alimtumia kwa kumpa nasaha na maelekezo ya kheri katika njia ya Allaah. Alizowea kumkumbusha Aayah za Qur-aan: 

 

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۖ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿١٨٥﴾ 

Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na uhai wa dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu. [Aal ‘Imraan: 185] 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾ 

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Hashr: 18]

 

Kabisa hakuzingatia umuhimu wa kufanya amali njema.  Hivi sasa anahitajia amali hizo ili azihudhurishe kwa Allaah, kwani Atasimamishwa ili atowe maelezo ya hesabu yake, lakini atasema nini? Kwani hakuwa mwenye kuzikumbuka Rehma za Allaah na Maamrisho Yake?  Vipi ataweza kuomba msamaha wakati hakuweza kabisa kufikiria kumtii Yeye alipokuwa na siha yake?

 

Alitamani laiti angelisoma Qur-aan Tukufu badala ya vile vitabu rahisi vya hadiyth za kubuni (novels). Alitamani laiti angeliongeza taaluma ya dini yake kuliko kusoma magazeti. Aliendelea kutamani laiti angelitenda mambo kadha-wa-kadha, na asingelifanya mambo ya kumuasi Rabb wake. Alitamani laiti asingelimkasirikia, au kusema uongo au kumsengenya mtu yoyote.  Alitamani laiti asingelijivuna na kudharau maskini.

 

Alisema, "Natamani ningeweza kuanza maisha yangu yote upya ili nirekebishe makosa yangu na nitii Maarisho ya Allaah. Niliabudia matamanio yangu nikampuuza Muumba wangu. Natamani ningepata muda kidogo wa kuishi ili nirekebishe madhambi yangu.

 

Aliikumbuka Aayah za Qur-aan ambazo babu yake alizoweya kuzisoma: 

 

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ فَلَا أَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلَا يَتَسَاءَلُونَ ﴿١٠١﴾فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٠٢﴾وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿١٠٣﴾تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ ﴿١٠٤﴾

Mpaka itakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: Rabb wangu! Nirejeshe (duniani). Ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha. (Ataambiwa) Laa hasha! Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu.  Na nyuma yao kuna barzakh mpaka Siku watakayofufuliwa. Basi itakapopulizwa baragumu, hakutokuwa na unasaba baina yao Siku hiyo, na wala hawatoulizana. Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni ambao wamekhasirika nafsi zao; katika Jahannam ni wenye kudumu. Moto utababua nyuso zao; nao humo watakuwa ni wenye midomo iliyosinyaa na kuvutika mbali na meno. [Al-Muminuwn: 99-104]

 

Hapo alisema, "Ee Rabb, nimekusudia ……" Machozi yalimwagika kwenye macho yake.  Alilia kwa majuto na siyo kwa maumivu. Aliamua kumtii Allaah katika maamrisho Yake yote pindi akiishi zaidi kidogo tu!!. Simu ilipolia alitembea kinyonge kwenda kuipokea. Huku machozi yakimtoka alisema, "Enhe?"

 

Akasikia mtu akisema: "Naweza kuzungumza na Anfaal?" Alimtambua msemaji.  Alikuwa ni daktari wake.  Akajibu, "Ndiye anaezungumza."

 

Daktari alisema kwa furaha. "Hongera mtoto wangu! Huna tatizo lolote.  Mshukuru Allaah!"

 

Alipigwa na bumbuwazi kwa mshangao. Hakujua aseme nini. “Hamna maradhi?  Vipi?  Je daktari unafanya mzaha!

 

Daktari akasema, "Allaah Anilinde kwa hayo, sifanyi mzaha. Punde mfanyakazi wa maabara ameniomba radhi. Alieleza kuwa kulitokea mchanganyiko wa majina. Jina lako liliandikwa badala ya mtu mwengine.  Ripoti yako ipo mbele yangu.  Wewe ni mzima kabisa.  Mshukuru Allaah ee mwanangu"

 

Kwa furaha alisema, "Shukrani kwa Allaah" (Nakushukuru Allaah), Ahsante daktari."

 

Aliweka simu chini akihisi kama kwamba ndio kwanza amezaliwa.  Kuanzai hapo, alitambuwa kuwa yupo salama kwa muda tu, lakini mauti yatakuja tu siku moja.  Hakuwa na muda wa kupoteza.  Hata kama aliishi muda mrefu (lakini bado) yeye ni mgeni.

 

Kitu cha mwanzo alichokifanya ni kuswali, ambapo kwa muda mrefu alikuwa amepuuza. Aliahidi kutii Maarisho ya Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuswali, kufunga, na kudumu kwenye mavazi ya heshima. Vile vile aliachana na yale yote Allaah na Rasuli Wake waliyoyakataza. Ili asiyasahau haya, alizinakili Aayah za Qur-aan kwenye kadi kisha akazitundika kwenye ukuta.  

 

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٥٦﴾

Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Rasuli ili mpate kurehemewa. [An-Nuwr: 56]

وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّـهِ ۖ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٨١﴾

Na iogopeni Siku mtakayorejeshwa ndani yake kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. [Al-Baqarah: 281]

 

Na akahofu asije kurudia makosa tena akaja kujuta tena. Akanakili pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) imkumbushe: 

 

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ﴿٥٤﴾وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ﴿٥٥﴾أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ﴿٥٦﴾أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ﴿٥٧﴾أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ﴿٥٨﴾

Na rudini kila mara kutubu kwa Rabb wenu na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa. Na fuateni yaliyo mazuri zaidi ambayo mmeteremshiwa kutoka kwa Rabb wenu kabla haijakufikieni adhabu ghafla na hali nyinyi hamhisi.  Isije nafsi ikasema: Ee majuto yangu kwa yale niliyokusuru katika upande wa Allaah! Na hakika nilikuwa miongoni mwa wenye kufanya masikhara. Au iseme:  Lau Allaah Angeliniongoa, bila shaka ningelikuwa miongoni mwa wenye taqwa. Au iseme pale itakapoiona adhabu: Lau ningelikuwa na fursa ya kurudi (duniani) basi ningekuwa miongoni mwa wafanyao ihsaan. Au iseme pale itakapoiona adhabu: Lau ningelikuwa na fursa ya kurudi (duniani) basi ningekuwa miongoni mwa wafanyao ihsaan. [Az-Zumar: 54-58]. 

  

Kwenye upande mwengine aliandika kauli ya ‘Umar ibn Al Khatwaab: 

 

Hesabuni nafsi zenu kabla ya kuhesabiwa, na zipimeni kabla ya kupimwa, kwani ni bora (wepesi) kwenu kupima (amali zenu) leo kabla ya (kupimwa) kesho kwenye Hesaabu, na jipambieni kwa siku ya Hadhara kuu: 

يَوْمَئِذٍ تُعْرَضُونَ لَا تَخْفَىٰ مِنكُمْ خَافِيَةٌ﴿١٨﴾

 

Siku hiyo mtahudhurishwa, hakitafichikia kwenu kinachofichwa. [Al-Haaqah: 18]  

  

Na methali ya busara:

 

"Tubia kabla hujafa, kwasababu huwezi kujua lini utakufa, hivyo basi daima kuwa ni mwenye kutubu."

 

Share