Wardi Katika Msitu - Kisa Cha Nuur

 

Wardi Katika Msitu – Kisa Cha Nuur

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Bismillahir-Rahmaanir-Raheem. Alhamdulillah

 

Hakika Himdi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tunamsifu na tunamuomba msaada na tuna muomba maghfira. Na tunamuomba atuhifadhi na shari za nafsi zetu, na maovu ya matendo yetu. Anaemuongoza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hapana wakumpoteza na Anaempoteza hapana wa kumuongoza.  Nakiri kwamba hapana mwabudiwa wa haki illa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hali ya kuwa Peke Yake Hana mshirika, na ninakiri kwamba Muhammad ni mja wake na ni Rasuli wake.  Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi na Swahaba zake na wanaofuata hao kwa wema mpaka Siku ya Malipo.

 

 

Napenda nishirikiane nanyinyi kisa cha safari yangu kufikia Uislamu dini ya asili iliyo safi na ya haki kabisa Aliyotuletea Rabb wetu kutuongoza katika njia iliyonyooka  kufuata kitabu chake na Rasuli  wake wa mwisho. 

  

 

Kabla Ya Uislam

 

Jamii, malezi na dini yangu

 

Nimezaliwa India katika jamii ya Sikh (Singa Singa).  Nimekulia katika malezi ya mzazi mmoja tu ambaye ni mama yangu, baba yangu alitangulia zamani kuja Canada akituacha mimi na mama yangu na mdogo wangu wa kike.   Watu katika mujtamaa wangu ni watu washupavu, tabia zao nyingi ni mbaya na za uwongo, za kuhadaiana. Na matajiri ndio zaidi wenye tabia hizo, maskini ni mtu wa kupuuzwa na kudharauliwa, na hakuna kuwaonea huruma wala kuwasaidia, bali wanazidi kuwa katika hali hiyo. 

 

 

Mama yangu alikuwa mkali sana na mshupavu. Alipata tabu kutulea kuhakikisha tunapata elimu nzuri pamoja na mafunzo mazito ya dini yetu ya Ki Singa Singa.   Mzunguko wa maisha yangu yalikuwa ya kidhiki kwa kukosa mapenzi ya wazazi wawili, kwa hiyo sikuwa katika hali   nzuri ya kisiha ya akili, kimwili hata ikawa imeniathiri hisia zangu. 

 

 

Nimesomeshwa katika shule bora kabisa ya dini yetu na mafundisho niliyopewa kuhusu Allaah (Mungu) ni kuwa tuamini kwamba haifai kumuwaza Allaah kwa kufuata akili za binaadamu, yaani hakuna nafasi ya hoja au busara katika jambo hilo.   Nakumbuka nilivyokuwa nikiwaza kuhusu mbingu na ardhi na nilivyozaliwa na kuwaza moyoni, "kama vyote hivyo vimeumbwa, bila ya shaka kuna muumbaji wa hivi vyote.”  Nikimuuliza mama yangu, hakuwa ananipa jibu lolote bali kuniambia niamini tu na kukubali mafunzo ya dini yetu. Nikifundishwa kuwa kuwasiliana na Allaah ni kuepukana na njia za kutafakari sana huku nikiamini kuwa Allaah mmoja hasa yupo na ninaweza kuzungumza nae na kwamba ananisikia.

 

 

Fikra Zangu Zilivyopanuka

 

Nilipotimia miaka 13 familia yangu ikaja kuishi Canada kuwa pamoja na baba yangu.  Ghafula nikajikuta kwenye mawingu ya mabadiliko ya maadili.  Ikanichukua muda kujisawazisha.  Maisha yangu nyumbani yalikuwa ya kubanwa kabisa wakikhofu wazazi wangu nisibadilike kuingia katika  maadili na kuathirika na tamaduni za nchi hii.  Nilipoingia chuo kikuu nikajihisi huru kidogo na ndipo nikaanza kuwaza vile nilivyo kuwa nahisi undani mwangu.  Nilisoma masomo ya Biology, Chemistry na Physics nikitaka niwe Engineer, ili tu niwafurahishe wazazi wangu waliokosa mtoto wa kiume, kwani hiyo ilikuwa ni tamanio lao kubwa na   baba yangu hakunipa mapenzi yale anayostahiki baba kumpa mwanawe.  Na tamanio hili lilikuwa likiwavunja moyo katika mujtamaa wetu kuwa hawana mtoto wa kiume bila ya kufikiri kuwa hayo ni makadirio ya Allaah. 

 

 

Nilipokuwa naingia ndani kabisa katika masomo ya Biology na kuelimika elimu ya mwili wa binaadamu, nilikuwa nikiwaza uzuri, ufundi, ustadi na uhodari wa maumbile haya, kwamba kila sehemu ya mwili ina kazi yake maalumu na zote zinafanya kazi barabara kabisa kumuezesha binaadamu aishi.  Je!  Ni nani huyo aliyetengeneza mjengo huu wa mwili?   Yuko wapi?  Akili yangu ikawa inanizunguka sana!! Nikitazama mbingu na ardhi, jua, mwezi, mimea, wanyama na bahari, almuradi nilitembea mbali kwa mawazo na kuwaza mjenzi wa hayo yote bila ya kumjua ni nani, huku sina raha kabisa na hamu kubwa imenishika nimtambue. 

 

 

Ibada na ada yangu zikaanza kuwa hazina muhimu akilini mwangu, nikaanza kuzikataa ndani ya moyo wangu kwanza.   Nikaanza kuwaza sababu ya maisha yetu binaadamu.  Nikahisi kuwa kuna kitu kilichopunguka katika kufahamu kwangu kuhusu maisha. Vipi Muumba wa binaadamu na dunia yote hakujijulisha kwetu?   

 

 

Kuumwa Kwangu

 

Ikaendelea hivyo mpaka siku za Spring 2002, nikaanza kuumwa.  Sikuwa na wasiwasi sana nikajua   kuwa nitapona tu na kila kitu kitarudi kama mwanzo. Lakini haikuwa hivyo, nilizidi kuumwa mpaka nikafikia katika hali ya kukata tamaa ya maisha, niliona ndio basi nakufa, hakuna wa kunisaidia, sio daktari wala mama, wala ndugu wala rafiki, wote hawakuweza kunifaa hata mimi mwenyewe sikuweza kujisadia lolote.    Niliyatamani hayo mauti na kupendelea bora nife kuliko kuadhibika na mateso hayo ya maumivu.  Nikawa najiuliza, "Kama Allaah (Mungu) anadhibiti mambo yote ya watu vipi ananitesa hivi? Kama kweli yupo mbona haniponyeshi na wazee wangu wanamuomba?

 

 

Nikatambua kuwa uzuri wangu, uhodari wangu, ujeuri na kiburi changu, vyote nilokuwa navyo vikawa vinayayuka, sina tena hayo, kwani faida gani kuwa nayo hayo na hayanifai kitu katika hali hii?   Maumivu makali, mateso, dhiki ya roho, kuchanganyikwa akili kulinipeleka kuwa katika kiza, nikawa sioni sisikii, nimo matesoni tu na tamaa ya kuishi inazidi kupotea. 

 

 

Kuzungmza Na Allaah Na Kusikia Kuhusu Uislamu

 

Kwa mara ya kwanza nikaanza kuzungumza na Allaah na kumuomba, bali kumuomba msamaha na kusema, "Ee Allaah kama kweli upo, na nafikiri kweli upo, basi nisamehe, nisaidie na nionyeshe njia, na nijulishe sababu ya maisha na ukweli wake”.  Baada ya haya, kidogo nikahisi raha fulani imepenya katika moyo wangu. 

 

 

Siku ya pili yake nilikuwa natizama T.V., walikuwa wakionyesha kisa cha mtu aliyesilimu.  Nilipendezewa na mabadiliko aliyopata huyo mtu baada ya kuingia katika Uislamu, zaidi katika utakaso, ukweli, uaminifu, udhalilifu wake yalikuwa ni mambo ya tunu kabisa.   Alikiri huyo mtu kuwa Uislamu ndio uliomfanya kupata sifa hizo.   Nikasema moyoni "Lazima niitafute hii dini ya Kiislamu niisome niijue ikoje?  Waislamu wanaamini nini kuhusu Allaah? Hili ni wazo kubwa muhimu nililotaka kujua jibu lake.

 

 

Nikaanza kutafuta katika internet kuhusu Uislamu nikasoma Tawhiid na iliniingia moja kwa moja akilini na kuikubali, maana niliona yote yaliosemwa yalikuwa ya hikma na yenye kuleta maana kabisa.  Zaidi kilichonivutia ni kukazaniwa neno la “Laa Ilaaha Illa Allaah” nikawa nawaza haya sana bila ya kiasi. Nikaanza kujifundisha tabia za Kiislamu nikapendezewa kuona sifa nzuri nzuri na mafundisho yake.  Nikawaza sasa, "Je vipi kuamini kwao kuhusu akhera?  Wanaamini nini baada ya mtu kufa?”    Nikaanza kusoma tafsiir ya Qur’an nikatambua kuwa kweli haya ni maneno ya Allaah hasa niliyekuwa namtafuta.  Ni kitabu cha mwisho, kilichokamilika na risala na uongofu wa Muumba uliomo humo, haukuwa na shaka ulikuwa wa wazi kabisa na wa kuridhisha.    Huku nikipata nafuu ya maumivu. 

 

 

Mama yangu akawa anaona tofauti yangu ya siha na pia akaona mabadiliko ya tamaa yangu, na kuwa ipo furaha fulani inayoonekana katika uso wangu.  Nikawa namuonyesha maneno ya Allaah akawa anayapokea vizuri na kukubaliana na mimi (huku sijui matokeo yake yatakuwa nini baada kuingia Uislamu). Qur'an ikanizidisha kuwaza dalili za Allaah zikawa zinakubaliana kabisa na mawazo yangu ya mwanzo hasa nikipitia katika aya kama hizi:

 

 إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ النَّاسَ وَمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن مَّاءٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ وَالسَّحَابِ الْمُسَخَّرِ بَيْنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ﴿١٦٤﴾

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na mabadiliko ya usiku na mchana na merikebu zipitazo katika bahari kwa vile viwafaavyo watu na Aliyoyateremsha Allaah kutoka mbinguni katika maji Akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake na Akaeneza humo kila aina ya mnyama na mgeuko wa upepo na mawingu yanayotiishwa baina ya mbingu na ardhi ni Aayaat (dalili, zingatio) kwa watu wenye akili. [Al-Baqarah: 164]

 

 

Nikazidi kujua aya zinazoelezea maumbile ya ulimwengu na binaadamu, elimu ambayo imejulikana na binaadamu baada ya miaka ya utafiti wa elimu ya sayansi. 

 

أَوَلَمْ يَرَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ كَانَتَا رَتْقًا فَفَتَقْنَاهُمَا ۖ وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ ۖ أَفَلَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٠﴾

Je, hawakuona wale waliokufuru kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeshikamana Tukazibabandua na Tukajaalia kutokana na maji kila kitu kilicho hai. Je, basi hawaamini? [Al-Anbiyaa: 30] 

 

مَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ وَهِيَ دُخَانٌ فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ﴿١١﴾

Kisha Akazielekea (Istawaa) mbingu nazo ni moshi; Akaziambia hizo na ardhi: Njooni kwa khiari au bila kutaka.  Zikasema: Tumekuja hali ya kuwa wenye utiifu. [Fusw-swilat: 11]

 

وَالسَّمَاءَ بَنَيْنَاهَا بِأَيْدٍ وَإِنَّا لَمُوسِعُونَ ﴿٤٧﴾ 

 Na mbingu Tumezijenga kwa nguvu na qudra na hakika Sisi ndio Wenye kupanua. [Adhariyaat: 47]

 

وَاللَّـهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِّن مَّاءٍ ۖ فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ أَرْبَعٍ ۚ يَخْلُقُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤٥﴾

Na Allaah Ameumba kila kiumbe kinachotembea kutokana na maji. Basi miongoni mwao wanaotembea juu ya matumbo yao, na miongoni mwao wanaotembea kwa miguu miwili, na miongoni mwao wanaotembea juu ya minne. Allaah Anaumba Atakavyo. Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Muweza. [An-Nuwr: 45]

 

 

Haya hayawezi kuwa ni maneno ya binaadamu.     Nikaamini kabisa maneno haya kuwa hakika ni maneno ya pekee ya Muumba.   Sasa vipi basi binaadamu wote hawatambui haya?  Vipi hawamtambui Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wao Aliyewaumba?  Nikazidi kupitia aayaah kama hizi zinazotaja kuhusu Allaah Muumba, na kuzidi kutumainika na dini ya Kiislamu. 

 

 قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ ۖ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ﴿٣٢﴾كَذَٰلِكَ حَقَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ عَلَى الَّذِينَ فَسَقُوا أَنَّهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ﴿٣٣﴾قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ۚ قُلِ اللَّـهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ﴿٣٤﴾قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ ۚ قُلِ اللَّـهُ يَهْدِي لِلْحَقِّ ۗ أَفَمَن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن لَّا يَهِدِّي إِلَّا أَن يُهْدَىٰ ۖ فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ﴿٣٥﴾

Sema: Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)?  Watasema: Ni Allaah; basi sema: Je, basi hamuwi na taqwa?  Basi Huyo Ndiye Allaah, Rabb wenu wa haki. Na kuna nini baada ya haki ila upotofu? Basi wapi mnageuzwa? Hivyo ndivyo Neno la Rabb wako lilivyothibiti juu ya wale waliofanya ufasiki kwamba hawatoamini. Sema: Je, yuko kati ya washirika wenu anayeanzisha uumbaji kisha anaurudisha? Sema: Allaah Anaanzisha uumbaji kisha Anaurudisha. Basi vipi mnaghilibiwa? Sema: Je, yuko kati ya washirika wenu anayeongoza kwenye haki? Sema: Allaah Anaongoza kwenye haki. Je, basi anayeongoza kwenye haki anastahiki zaidi kufuatwa au ambaye asiyeongoza isipokuwa tu yeye aongozwe?  Basi mna nini, mnavyohukumu? [Yuwnus: 31 – 35]

 

 

Huu ndio uongofu niliokuwa nautafuta!  Furaha ikanizidi ya moyo na kujihisi mwepesi kabisa. Qur'aan hii haikunionyesha uongofu tu, bali imenionyesha uvumbuzi wa matatizo ya binaadamu akiwa pekee au akiwa pamoja na familia yake au akiwa   na mujtamaa wake (jamaa).  Imemuonyesha wazi binaadamu wajibu wake, haki yake na jukumu lakekatika madaraka yake.  Imempangia maisha katika mambo ya mahitajio yake, tabia na matendo yake katika jamii kwa njia iliyo ya hikma na ya heshima kabisa. 

 

 

Qur'ani imefundisha binaadamu vipi kujiepusha na matamanio ya nafsi yaliyo kuwa ya mazowea katika nyoyo za binaadamu mwanamme na mwanamke.

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾ 

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An Nuwr: 31]

 

 

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾ 

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59]

 

 

Qur'aan imempa haki mwanamke kwa kulinganisha na uumbile lake na hali kadhalika mwanamme.  Uislamu ni mpango mkamilifu na njia ya maisha bora kabisa ya kumfaa binaadamu kumuongoza katika mwangaza, kumtoharisha na maovu, na kumtoa katika kiza na kumuweka katika heshima anayostahiki, nimetambua kuwa ni hiari yake mtu kufuata haki au kuikanusha.  Allaah anasema Katika Qur-aan Tukufu:

 

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ وَإِن تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۗ إِنَّمَا تُنذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ ۚ وَمَن تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ ۚ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ ﴿١٨﴾وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ ﴿١٩﴾وَلَا الظُّلُمَاتُ وَلَا النُّورُ ﴿٢٠﴾وَلَا الظِّلُّ وَلَا الْحَرُورُ ﴿٢١﴾وَمَا يَسْتَوِي الْأَحْيَاءُ وَلَا الْأَمْوَاتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ ﴿٢٢﴾

Na wala mbebaji yeyote hatobeba mzigo (wa dhambi) wa mwengine. Na aliyeelemeshwa mzigo akiita ili kusaidiwa kubebewa mzigo wake, hatobebewa chochote, japokuwa ni jamaa wa karibu. Hakika wewe unaonya wale wanaomkhofu Rabb wao kwa ghayb, na wakasimamisha Swalaah. Na yeyote anayejitakasa, basi hakika anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake; na kwa Allaah ndio mahali pa kuishia. Na halingani sawa kipofu na mwenye kuona. Na wala viza na nuru. Na wala kivuli na joto. Na wala hawalingani sawa walio hai na wafu. Hakika Allaah Anamsikilizisha Amtakaye; nawe huwezi kuwasikilizisha walioko kaburini. [Faatwir: 18 -22]

 

 

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَوَمَن كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢٢﴾ 

Je, aliyekuwa maiti kisha Tukamhuisha na Tukamjaalia nuru anatembea kwayo kati ya watu, ni sawa na yule ambaye yumo katika viza si mwenye kutoka humo? Hivyo ndivyo walivyopambiwa makafiri yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-An’aam: 122]

 

 

Kuchukua Shahada (kuingia Uislamu)

 

Aayaah zote hizo na nyingine nyingi zikanifanya nikubali Uislamu ndani ya moyo wangu japokuwa sijakiri Shahada.  Nikaamua sasa nikatafute Muislamu anipe shahada.  Nani atakaenipa? Wapi?  Nikachukua kitabu cha simu kutafuta duka la vitabu vya KiiIslamu.  Nikapiga simu duka moja nikafunga safari kulifuata, nalo ni mbali na kwetu.  Kufika nikajidai kwanza kutizama vitabu kisha kumuuliza mwenye duka kuhusu Uislamu na vipi kuingia katika dini hii, akanifahamu kuwa nataka kuchukua shahada. Akaniuliza, "Je ndugu unataka kuchukua shahada hivi sasa?"  Machozi ya furaha yakanitoka na kumuitikia, hapo hapo nikakiri shahada, "Ash-hadu An-Laa Ilaaha Illa Allaah Wa Ash-hadu Anna Muhammadan Rasulu Allaah.” 

 

 

Furaha ilioje moyoni mwangu, nilijihisi ni mtu mwingine kabisa.  Nikarudi nyumbani huku natabasamu, furaha ikidhihirika usoni mwangu.  Zikapita siku nikawa najifunza kuswali na kuibia kuswali kwani niliogopa wazazi wasijue, ambao nimekuja kujua kuwa jamii yetu ni maadui wakubwa   wa Uislamu.  Nikaendelea kuficha, lakini mama yangu alikuwa hana raha kuniona kutwa niko kwenye internet nikisoma mambo ya Kiislamu, mwisho ikabidi nimwambie.   Kwa vile aliniona kuwa nimekuwa mtu mwenye furaha, na bado sijapona vizuri, ikawa kama kuumwa kwangu ni usalama wa kuingia dini hii.  Kama kwamba nikimsoma mawazo yake mama yangu anasema, "Si kitu madamu unapata nafuu ya  maradhi yako na madamu una furaha basi, lakini naichukia hiyo dini,” kwani alikwisha niambia kuwa utatutia aibu kubwa katika jamii yetu, tutakuwa na uso gani mbele ya jamaa zetu?  

 

 

Ikawa kila siku ni masuali hayo hayo, na habari zikawafikia jamaa zangu wa ki Singa Singa ambao hawakunyamaza, bali waliwaita wazazi wangu na kuwataka watoke katika aibu hiyo.  Wazee wangu hawakuweza kunilazimisha kwani walihofu nisirudie hali yangu ya kuumwa. Subhaana Allaah! Nikawa nasema moyoni kila kitu kina kheri yake, kuumwa kwangu kumekuwa kheri kwangu kwamba wazazi wangu wananistahmilia kubadili dini yangu ingawa wanaichukia.  Ukhasama ukawa baina ya jamii yangu na wazazi wangu.  Wakaukata uhusiano kabisa, na wachache tu ndio waliobakia kuwa na aila yangu.  Jeuri, kiburi na chuki ya dini ya Kiislamu ndio sababu ya ari yao hiyo.    

 

 

Nikaanza kwenda msikitini nikajuana na wanawake wengi walionipokea kwa mapenzi na undugu wa dhati wa Kiislamu.  Nikajulishwa na mwalimu wa Qur'ani nikawa nakwenda kwake kusoma.  Mwalimu huyo ni kama mama yangu, dada yangu, rafiki yangu, nikashikana naye sana, alikuwa akinisaidia kwa kila aina ya njia ya kuimarisha dini yangu.   Nikajifunza namna ya kusoma Qur'aani (Qaida) na Alhamdulillah nikaweza kusoma na kuijua vizuri vile inavyopasa.

 

 

Baada ya siku chache kuanza kujifunza Qur'ani, nilimuota bibi yangu mzaa mama ambaye tokea kufariki kwake miaka mingi sikupata kumuota.  Nilimuota anafuraha na huku anamkumbatia mwalimu wangu.  Ndoto ilikuwa ya wazi kabisa hata niliamka usingizini na kupigwa na bumbuwazi!  Ni ndoto au ni kweli?  Ni ndoto! Ndoto ya kweli!  Bibi yangu amefurahi mimi kuingia katika uislamu!  Bibi yangu ananijulisha kuwa niko katika njia ya haki.  Jambo la mwanzo nilipoamka nikamuelezea mama yangu ambaye naye alishangaa, lakini akanipuuza kwa vile hakutaka niiamini hii dini yangu.  

 

 

Wazee wangu wakawa wanatia shaka na mimi kutoka kwangu kwingi kuhudhuria darasa, mikutano ya dini, na hata mara nyingine wakinitumia mtu kunifuata kuniona nakwenda wapi.  Ajabu ni kwamba nilipokuwa natoka kwenda disco, na sinema na kurudi usiku hapo mwanzoni walikuwa hawaniambii kitu.  Lakini nnapokwenda kusoma dini na kurudi mapema nyumbani kuweko chumbani kwangu wakiniambia, "mbona kutwa uko chumbani hutoki?”  Maajabu!!

 

 

Nikaendelea hivyo hivyo na huku nikizidi kupata nafuu ingawa sikupona kabisa, lakini Alhamdulillah namshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kunifikisha hapa nilipofikia kwa Kuniongoza, Kunitoa katika kiza na Kunitia katika mwangaza. Na ndio maana nimejibadilisha jina langu kujiita 'Nuur' badili ya Rimmie.   Alhamdulillah, neema zote ni Zake Mola wa Mbingu na Ardhi namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Azidi Kuithibitisha imani yangu na Anijaaliye miongoni mwa watu wema mpaka nitakapokutana Naye.

Amiin.

 

  

Maelezo Zaidi Kutoka Kwa Mwalimu Wake Nuur

  

Aliponipigia simu Nuur kwa mara ya kwanza kutaka kusoma Qur'ani, na nilipojua kuwa katoka katika jamii ya Singa Singa, kwanza mwili ulinisisimka, maana niliona wengi wao wanaobadili ni kutoka dini ya Ukristo na kutoka jamii nyingine lakini sijapatapo kuona kutoka jamii hii. Nilikuwa na hamu kubwa ya siku tulioagana ifike.  Nikachungulia dirishani kumsubiri wakati anakuja na nilipomuona, Subhana Allaah, msichana mwenye uzuri wa kupendeza kabisa, mpole, na juu ya hayo nimeona ajabu ya akili yake aliyomjaalia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).  Alikuwa akihudhuria mara mbili tu kwa wiki, kila mara akitumia saa moja na nusu, akisoma masomo mawili au matatu kwa mara moja, kisha  baada ya siku   ya pili yake akirudi amekwishajifunza vizuri, hata ameweza kumaliza kujifunza kusoma Qaida ya Qur'aan kwa muda wa miezi miwili na nusu tu! Kisha akawa anaendelea kusoma sura mpaka akafikia karibu kumaliza juzuu ya Amma nzima.  Maajabu ni kwamba hata matamshi yake ya kiarabu yalikuwa kama mtu aliyezaliwa nayo lugha ya Kiarabu.  Na hawa ndio wale Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kawataja kuwa 'Ulul-Al-baab" yaani "Watu wenye akili.”  (Ya kutafakari )

 

 

Siku ya harusi yake iliofanywa msikitini, alipendeza sana, na ajabu ni kuwa hakujipamba mapambo yeyote, si wanja, wala podari wala si rangi ya mdomo, lakini alikuwa ananġaa kwa uzuri na ucheshi, Nuru ya kweli ilikuwa ikinġara usoni mwake.    Mama yake alikuwa akilia sana.  Nikamwambia "Nuur! mama yako analia sana" Akanijibu "ee dada yangu, huonii kuwa analia machozi ya kusikitika kwamba siku ya leo hakutegemea kumuozesha mwanawe msikiti wa Waislamu?  na siyo machozi ya furaha wakati mimi nna furaha ya kupata dini ya haki?  Basi mwache alie tu, machozi hayo kwangu hayana thamani, namuomba tu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amuongoze   na yeye".     

 

 

Hivi sasa Nuru anasoma masomo ya Sheria ya Kiislamu, aliniambia kuwa anataka kujua lugha ya Kiarabu vizuri ili aweze kufanya daawa katika jamii yake ya Kipanjabi.  Kwa vile ni nadra kuingia katika Uislamu   mtu kutoka kwenye jamii hiyo na kwa jinsi ilivyothibitika imani yake huyu msichana, nimependa kukiita kisa chake "Wardi katika msitu"    "A rose in the forest".

 

Tumuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Athibitishe imani yake na zetu sote.  Aamiyn. 

 

 

Share