Zingatio: Siku Kumi Tukufu Za Dhul-Hijjah
Siku Kumi Tukufu Za Dhul-Hijjah
Naaswir Haamid
Rabb wetu Mtukufu Ametujaalia kila aina ya neema ili tuweze kujikurubisha Kwake. Lengo kuu ni kumukhofu Yeye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ili kupata salama Siku ya Hisabu.
Bila ya shaka katika neema Zake kubwa juu yetu ni kuzaliwa tukiwa ndani ya Ummah wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni lulu ambayo hata Nabiy Muwsaa ('Alayhis-salaam) aliililia kuipata lakini hakuipata.
Miongoni mwa mazuri ya Ummah huu mtukufu ni kuwepo masiku kumi maalumu kwa ajili ya kughufuriwa madhambi yetu katika njia nyepesi kabisa:
وَالْفَجْرِ ﴿١﴾وَالْفَجْرِ ﴿١﴾
Naapa kwa Alfajiri. Na Naapa kwa masiku kumi. [Al-Fajr: 1-2]
Hizo ni siku ambazo tunazo sasa hivi kwenye mwezi wa Dhul-Hijjah (mfungo tatu). Hizi ni siku za manufaa na kumkumbuka Allaah:
لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ
Ili washuhudie manufaa yao; na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu... [Al-Hajj: 28]
Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha utukufu wa siku hizi kwa kusema:
"Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama siku kumi hizi" (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah) Akaulizwa, je, hata Jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) "Hata Jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo".[Imesimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kupokelewa na Imaam Al-Bukhaariy]
Hichi ni kipindi cha kukaza kamba, tukajikurubisha kwa Muumba katika namna ya kumtukuza Yeye. Tumuombe Atughufirie madhambi yetu kwa unyenyekevu ndani ya kipindi hichi:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا
Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli);..[At-Tahriym: 8]
Kwa mwenye kuweza kufunga siku tisa za mwanzo katika mwezi huu, basi asiiwache nafasi hii ‘adhiymu. Kwa aliyebanwa, basi pia asiitupe bakhshishi hii kwa kufunga siku ya ‘Arafah (siku ya tisa katika mwezi wa Dhul-Hijjah). Swawm hii ya ‘Arafah itampatia nafasi (In Shaa Allaah) ya kufutiwa madhambi ya miaka miwili:
Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema kuhusu Swawm ya 'Arafah kuwa ((inafuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake)) [Imepokelewa na Imaam Muslim]
Naye mama yetu ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ametusimulia (kupitia maneno ya Nabiy) kwamba siku ya ‘Arafah ni siku ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawaachia huru waja wake kutokana na moto:
"Hakuna siku Allaah Anayowaacha huru waja na moto kama siku ya ‘Arafah". [Imepokelewa na Imaam Muslim]
Tusisahau pia kuleta dhikri na kumuomba sana Muumba wetu kwa du’aa nzuri nzuri kama alivyotufunza kipenzi chetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Manabii kabla yangu ni:
'Laa Ilaaha Illa Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lahu, Lahul-Mulku Wa-Lahul-hamdu Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr’ [Imepokelewa na At-Tirmidhiy]