Mjomba Alimnunulia Mama Yake Nyumba Akafiriki, Mama Naye Amefariki Na Ameacha Watoto

 

Mjomba Alimnunulia Mama Yake Nyumba Akafiriki,

Mama Naye Amefariki Na Ameacha Watoto

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Asalam aleikum nilikua nauliza kuhusu wirathi nilikua nataka kujua tafadhali naomba unijibu nipate kufahamu. Mimi nina mjombangu alinunua nyumba akaandika ile nyumba jina la mamake huyo mjombangu ni ndugu tu na mamangu kwa mama na baba. Huyo mjombangu nae alikufa lakini mamake
yuhayi na huyo mamake mimi hua ni nyanyangu. na ana watoto wengi wanawake na wanaume. Lakini mamangu nae alikufa baada ya mjomba kufa kisha mamangu alikufa kisha nyanyangu nae akafa sasa nauliza mimi narithi. na mamangu amezaa watoto wawili tu wanawake sasa nilikua nataka kuuliza pengine mwaeza kunifahmisha zaidi  tafadhali mukiipata munijibu maasalam.  

 

Ufafanuzi zaidi uliotakiwa na Alhidaaya kuweza kujibu swali:

 

Ili tuweze kukujibu vizuri zaidi tungependa utujulishe yafuatayo:

 

1. Je, huyu nyanyako, mume wake yuko hai?

2. Je, una ndugu shaqiqi? au ndugu kwa mama tu au kwa baba tu?

3. Je, wazazi wake wapo hai?

 

JIBU La Muulizaji:

 

 

Laa nyanyangu hana mume wake alikufa kitambo sana tangu mimi nimdogo. Na nyanyangu anao ndugu zake shakiki kabisaa kwa mama na baba wana`wake kwanaume. Laa na wazazi wake nyanyangu wote walikufa kitambo.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Ahsanta sana kwa maelezo hayo ambayo yametusaidia sana kuweza kulijibu swali hili.

 

Mwanzo kabisa, ifahamike kuwa mtu hawezi kumuandikia mtu mwengine ambaye ana fungu maalumu katika wirathi kuwa yeye ndiye mwenye kurithi.

 

Sasa ikiwa mjombako alimnunulia nyanyako na kumpatia tunu (au zawadi) itakuwa ni sawa lau kama alimuandikia kuwa huo ni wirathi wake atakuwa amefanya makosa, hivyo hiyo nyumba itachukuliwa kuwa ni ya mjombako, naye atarithiwa na warithi wake akiwemo mamake ambaye ni nyanyako.

 

Hivyo, akiwa ni mjomba wako itategemea kama ameacha mke na watoto wao watakuwa na mafungu yao. Katika mfano huu kwa sababu mama yako alikufa baada ya mjomba wako huenda akapata fungu katika wirathi yote yakitegemea watu wa karibu wa mjomba wako. Na ikiwa mama yako atapata fungu katika vilivyoachwa na mjomba na yeye tayari amefariki, fungu lake (yaani mama yako) litarithiwa na warithi wake ukiwemo wewe na wengineo. Kwa hakika fungu lako hapo litakuwa ni maalumu lililotajwa katika Qur-aan:

 

يُوصِيكُمُ اللَّـهُ فِي أَوْلَادِكُمْ ۖ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ ۚ فَإِن كُنَّ نِسَاءً فَوْقَ اثْنَتَيْنِ فَلَهُنَّ ثُلُثَا مَا تَرَكَ ۖ وَإِن كَانَتْ وَاحِدَةً فَلَهَا النِّصْفُ ۚ وَلِأَبَوَيْهِ لِكُلِّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا السُّدُسُ مِمَّا تَرَكَ إِن كَانَ لَهُ وَلَدٌ ۚ فَإِن لَّمْ يَكُن لَّهُ وَلَدٌ وَوَرِثَهُ أَبَوَاهُ فَلِأُمِّهِ الثُّلُثُ ۚ فَإِن كَانَ لَهُ إِخْوَةٌ فَلِأُمِّهِ السُّدُسُ ۚ مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ لَا تَدْرُونَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ لَكُمْ نَفْعًا ۚ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١١﴾ 

Allaah Anakuamrisheni kuhusu watoto wenu. Mwanamume atastahiki mfano wa fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake ni zaidi ya wawili basi watastahiki theluthi mbili za alichoacha (maiti). Lakini akiwa mtoto wa kike ni mmoja pekee basi atastahiki nusu, na wazazi wake wawili kila mmoja wao atastahiki sudusi katika alichoacha ikiwa anaye mtoto. Na ikiwa hakuwa na mtoto na wazazi wake wawili ndio warithi wake, basi mama yake atastahiki theluthi moja. Na ikiwa anao ndugu basi mama yake atastahiki sudusi, baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu hamjui ni yupi miongoni mwao aliye karibu zaidi kwenu kwa manufaa. Ni shariy’ah kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [An-Nisaa: 11]

 

Lakini ikiwa hiyo nyumba ni tunu kutoka kwa mjomba wako kumpatia nyanya yako, mama yako kwa sababu aliaga dunia kabla ya mama yake hatakuwa na fungu lolote hivyo wewe hutapata chochote katika mirathi. Fungu kubwa litakwenda kwa watoto wake (wa nyanya yako) wa kiume na kike na kitakacho baki kitakuwa ni cha kaka zake na dada zake nyanya yako.

 

Tanbihi: Kwa wenye kuuliza Maswali ya Mirathi:

 

Ili maswali yenu yajibike kwa wepesi na haraka inatakiwa kuwa wale watu wote ambao wana ukaribu wa kidamu wa aliyefariki wawe ni wenye kuandikwa ili iwe hapana utata wowote. Na katika hayo tungependa watu wafuatao watiliwe maanani sana:

 

1.     Kijana mwanamume.

2.     Kijana mwanaume wa kijana mwanaume (mjukuu)

3.     Baba.

4.     Babu wa kwa baba.

5.     Ndugu mume wa kwa baba na mama (khalisa).

6.     Ndugu wa kwa baba.

7.     Ndugu mume wa kwa mama.

8.     Kijana mwanaume wa ndugu mume khalisa.

9.     Kijana mwanaume wa ndugu mume wa kwa baba.

10.   Ami wa kwa baba na mama.

11.   Ami wa kwa baba.

12.   Kijana mwanaume wa ami wa kwa baba na mama.

13.   Kijana mwanaume wa ami wa kwa baba.

14.   Mume.

15.   Binti.

16.   Binti wa kijana mwanaume.

17.   Mama.

18.   Dada khalisa.

19.   Dada wa kwa baba.

20.   Dada wa kwa mama.

21.   Bibi mzaa baba.

22.   Bibi mzaa mama.

23.   Mke.

 

Hii itatusaidia sana katika kujibu maswali yenu ya mirathi. Shukran.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share