Kurithi Wazazi Makafiri Inajuzu?

 

SWALI:

Kati ya wazazi wawili mmoja ni mkristu.  Je naweza kurithi mali walizoacha? na vipi ?

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Jibu la swali hili lipo wazi katika Hadithi iliyonukuliwa na Imaam Maalik katika al-Muwattwaa’ yake: Yahya alipokea kutoka kwa Maalik kutoka kwa Yahya bin Sa‘iid kutoka kwa Sulaymaan bin Yasar kuwa Muhammad bin al-Ashath alimwambia kuwa alikuwa na halati (mama mdogo) Mkristo au Myahudi aliyefariki. Muhammad bin al-Ashath alimuuliza ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'anhu): “Je, ni nani wenye kumrithi? ‘Umar bin al-Khattwaab alimjibu: “Ni watu wa Dini yake”. Baada ya hapo alikwenda kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan, na kumuuliza kuhusu hilo. ‘Uthmaan alimwambia: “Je, unadhania nimesahau alivyo kwambia ‘Umar bin al-Khattwaab? Watu wa Dini yake ndio wenye kumrithi”.

Hivyo, ni wazi kuwa Muislamu hawezi kumrithi asiyekuwa Muislamu na kinyume chake pia ni sawa. Kwa hivyo, ikiwa yule mzazi aliyokuwa ni Muislamu ndiyo aliyeaga dunia basi huyo kijana aliyekuwa Muislamu ndiye atakayemrithi. Lakini ikiwa mzazi asiyekuwa Muislamu ameacha wasia na amekutunukia kitu basi utakichukua bila ya wasiwasi wowote.

Na Allah anajua zaidi.

 

Share