Nini Hukmu Ya Kuua Mtu?

SWALI:

 

Dhambi ya kuuwa inasamehewa?? Maana nimepokea majarida yenu katika mda wa ijumaa kama tatu hivi yakisisitiza kuhusu mwanadam kufanya TAUBA SHUKRA ALLAH YU PAMOJA NASI.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hukumu ya dhambi ya kuua.

Hakika ni kuwa hakuna dhambi ambayo haisamehewi na Allaah Aliyetukuka kwani Yeye ni Mkarimu na Msamehevu sana kwetu pindi tunaporudi Kwake ni kuomba maghfira’

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Sema: Enyi waja Wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Allaah; bila shaka Allaah Husamehe dhambi zote; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu” (az-Zumar [39]: 53).

 

Kwa hiyo, kwa usamehemu Wake, Allaah Anasamehe kila aina ya dhambi, kubwa au dogo bila ya tatizo lolote lile. Anasema tena Aliyetukuka:

Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na atakayefanya hayo atapata madhara. Na atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaamah na atakaa humo kwa kufedheheka milele. Ila yule atakayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri; basi hao ndio Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema; na Allaah ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu. Na aliyetubia na kufanya mema, basi kwa hakika yeye anatubu kweli kweli kwa Allaah” (al-Furqaan [25]: 68 – 71).

 

Katika Aayah zilizo juu tunapata mambo yafuatayo katika masharti ya kusamehewa dhambi la kuua:

 

1.     Kutokata tamaa na rehema ya Allaah Aliyetukuka.

2.     Anafaa atubie baada ya kuua.

3.     Amuamini Allaah Aliyetukuka.

4.     Afanye matendo mema baada ya hilo ovu.

 

Ukisha tekeleza hayo basi hata hayo mabaya hubadilishwa na Allaah Aliyetukuka kuwa mema kwake. Tunapata funzo kuhusu tawbah ya mwenye kuua katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

عن أبي سعيد الخدري رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال : )) كان فيمن كان قبلكم رجل قتل تسعة وتسعين نفسا ، فسأل عن أعلم أهل الأرض ، فدُلَّ على راهب ، فأتاه فقال : إنه قتل تسعة وتسعين نفسا ، فهل له من توبة ، فقال : لا ، فقتله فكمل به مائة ، ثم سأل عن أعلم أهل الأرض ، فدُلَّ على رجل عالم ، فقال : إنه قتل مائة نفس ، فهل له من توبة،  فقال : نعم ، ومن يحول بينه وبين التوبة ، انطلق إلى أرض كذا وكذا ، فإن بها أناسا يعبدون الله ، فاعبد الله معهم ، ولا ترجع إلى أرضك ، فإنها أرض سوء ، فانطلق حتى إذا نصَفَ الطريق أتاه الموت ، فاختصمت فيه ملائكة الرحمة وملائكة العذاب ، فقالت ملائكة الرحمة : جاء تائبا مقبلا بقلبه إلى الله ، وقالت ملائكة العذاب : إنه لم يعمل خيرا قط ، فأتاهم ملَكٌ في صورة آدمي ، فجعلوه بينهم ، فقال : قيسوا ما بين الأرضين ، فإلى أيتهما كان أدنى فهو له ، فقاسوه فوجدوه أدنى إلى الأرض التي أراد ، فقبضته ملائكة الرحمة))  (الإمام مسلم في صحيحه)   

Imetoka kwa Abu Sa'iydil-Khudriyyi (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Alikuweko mtu kabla yenu aliua nafsi tisiini na tisa. Akauliza kutaka kumjua aliyekuwa na elimu kuliko wote duniani, akapelekwa kwa mtawa. Akawambia kuwa ameua watu tisini na tisa kisha akamuuliza kama atasamehewa. Mtawa akamwambia "husamehewi". Akamuua na yeye pia ikawa ni watu mia aliowaua.

Akauliza tena kutaka kujua mtu mwenye elimu kabisa duniani akapelekwa kwa mtaalamu. Akamwambia kuwa ameua watu mia na akamuuliza kama atasamehewa. Mtaalamu akamwambia. "Ndio, kwani nani atakayejiweka  baina yako na baina ya Tawbah? Nenda mji fulani kwani huko kuna watu wanaomuabudu Allaah. Nenda ukaabudu pamoja nao na usirudi mji wako kwani ni mji mbaya huo".

Akaelekea huko lakini alipofika nusu njia Malaika wa kutoa roho akachukua roho yake. Malaika wa Rahma na Malaika wa adhabu   wakaanza kumgombania. Malaika wa Rahma akasema: "Ametubu na amekuja kumtafuta Allaah". Malaika wa adhabu akasema: "Hakufanya lolote jema". Akatokea Malaika katika umbo la binaadamu akawajia na wakamuomba awahukumie jambo hilo. Akasema: "Pimeni umbali baina ya miji miwili (yaani mji wake aliotoka na mji aliokuwa anaelekea) na wowote utakaokuwa ni karibu zaidi basi ndio huo utakaokuwa ni wake". Wakapima na kuona kwamba mji ambao alikuwa anaelekea kwenda ulikuwa karibu zaidi. Hivyo Malaika wa Rahma akamchukua [Muslim]

[Kwenye As-Swahiyh imesema: "Mji mwema ulikuwa karibu kwa dhiraa moja. Hivyo akahesabiwa kuwa ni mtu wa mji huo"]. [Riwaya nyingine katika As-Swahiyh inasema: "Allaah Aliamrisha (mji muovu) usogee mbali hivyo (mji mwema) ukasogea karibu na akasema" Pimeni umbali baina yao" Walipopima waliona kwamba yuko karibu na mji mwema kwa umbali wa dhiraa moja, kwa hiyo akasamehewa]

 

 

 

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share