Amewaandikia Nyumba Watoto Wa Mke Wa Mwisho, Watoto Wa Mke Wa Mwanzo, Wanadai Mirathi Baada Ya Miaka 12

SWALI:

 

A'aleykum. Mzee alikua na wake watatu. Mzee aliwaandikia nyumba watoto wa mke mwisho kwa sababu hawa watoto walikua wadogo na yeye mzee sana. Huu mwaka wa 12 wamekuja watoto wa mzee kudai haki yao kwenye hii nyumba. Je wanayo haki?

Tunaomba ushauri nini kifanyike ili amani ipatikane?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Mirathi ya watoto kutoka kwa baba yao aliyeaga dunia.

Hakika ni makosa kwa mzazi kuacha wasiya nani arithi nini wakati anaaga dunia au kabla ya hapo. Mirathi kawaida kishari’ah haandikiwi chochote bali anapata kile kilichopangwa na Allaah Aliyetukuka. Wasiya mtu anaweza kumuandikia asiyerithi na haifai kuzidi thuluthi moja.

 

Ama katika kadhiya hii, inatakiwa mali iliyoachwa na mzee yatiwe thamani kisha yagawiwe kulingana na shari’ah ya Kiislamu. Mgao wa kila mmoja utategemea kama mzee huyo alikuwa na wazazi au la? Na wakati anaaga dunia alikuwa na wake wote watatu au wengine walikuwa wamekufa? Kulingana na uzee wa aliyefariki inaonekana kama hakuacha mzazi nyuma hata mmoja. Ikiwa wazazi wake watakuwa wapo hai mtatueleza. Ikiwa ni kama hivyo, basi mgao utakuwa kama ifuatavyo:

 

1.     Mke au wake atapata au watapata thumuni (1/8). Ikiwa aliyebaki hai ni mmoja atapata thumuni na ikiwa wapo wote watatu watagawa hiyo thumuni.

2.     Watoto watapata kilichobaki, mtoto wa kiume akipata sehemu mbili ilhali msichana akipata moja. Sasa inategemea aliacha watoto wangapi. 

 

Inatakiwa kwa sasa waliobaki wafanye haki kwa kuigawa inavyotakiwa na Uislamu. Na wenye kufanya uadilifu huo watapata thawabu nyingi kutoka kwa Mola wao Mlezi. Ikiwa baadhi ya wake wameaga dunia au watoto wengine wamefariki, sehemu zao watagawiwa warithi wao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share