Achague Kuolewa Na Anayependana Naye Japokuwa Si Mcha Mungu Au Ambaye Ni Mcha Mungu?

 

SWALI:

 

 Asalaam Aleikum Warahmatullah Taala Wabarakatuh, Ninawashukuru sana uongozi mzima wa taasis hii ya Alhidaya, kwani kupitia taasisi yenu nimetoka kwenye giza nene na sasa Alhamdulillah nipo kwenye mwanga na ninatimiza wajibu wangu kama muislam anavyopashwa kutimiza. Swali langu ni kwamba? Kwa kipindi cha nyuma kabla sijatoka gizani! Nilikuwa na mpenzi yaani mvulana ambaye tulishirikiana kutenda maovu hayo na kusema ukweli nampenda sana kijana. Lakini sasa kwa muda mrefu sasa yaani ni zaidi ya miaka minne hatupo pamoja kwani tumekuwa tukiishi mabara tofauti tofauti, lakini mawasiliano yetu yamekuwa ni kwa telephone tu, Sasa baada ya kuusoma Uislam na kuuelewa, nikagundua kama kijana huyo ana walakini kidogo, kwakuwa yeye hajihusishi kabisaa na mambo ya dini na hata ninapomuusia kwake yeye inakuwa tu kama ninatafuta sababu ya kumuacha, na ikiwa nimekwisha elewa kama sifa kubwa ya muoa au muolewaji ni mtu kuwa mchamungu, nami napenda sana kuishi maisha ya kiuchamungu na mpenzi huyu ila ndio hivyo tena kwake inakua ngumu. Na kwa upande mwingine kuna kijana mwingie yeye Maishallah ana muelekea Allah kwa unyenyekevu kabisa na anakila sifa ya uume katika uislam, na yuko tayari kunioa na tukaishi maisha hayo nitakayo mimi kwa sababu naye ndio maisha anayoishi. TATIZO ni kwamba nampenda yule mpenzi wangu alafu familia yake yote inanifahamu na inatambua kama mimi ndiye nitakaeolewa na kijana wao kiasi hata wazazi wanazungumza kwa simu. SASA JE NIFANYE NINI? NINAPENDA NA PIA NINAOGOPA KULAUMIWA NA FAMILIA YAKE NZIMA, LAKINI PIA NINAPENDA NA KUFURAHIA SANA MAISHA YA UCHAMUNGU KAMA KIJANA HUYU ATAKAE KUNIOA.  Kwa kweli nahitaji msaada wenu kwa hili kwani wakati flani nahisi kama haya mapenzi yatanipeleka motoni, na vilevile najiuliza nitaweza kumpenda kijana huyu mwingine ili nitekeleze wajibu wangu kama mwanamke wa kiislam? Sababu tutakuwa tunakumbushana na kukatazana batwili na hali ikiwa na yeye anajua maana na hukmu za ndoa katika uislaam,


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunapenda kukuarifu kwamba hatukuwa tukipokea maswali kama tulivyoweka tangazo. Lakini kutokana na umuhimu wa Swali lako tumeona tulipe kiupambele kwani linahusiana na maamuzi makuu yatakayokuathiri katika maisha yako ya kidunia na Akhera.

 

Pili tunakupa nasaha kwamba katika maamkizi ya salaam, usiwe  unaongeza  neno 'Ta'ala' kwenye Salaam kwa kusema 'Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLlaahi Ta'ala wa Barakaatuh', kwani si jambo tulilofundishwa katika Salaam na hivyo ni bora mtu kuliepuka katika Salaam.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mapenzi na yaliyopita kabla ya kujua kwako haki na ukweli. Mwanzo tumefurahi sana kwa swali lako kuhusu suala hilo nyeti katika jamii yetu ya Kiislamu.

 

Inatakiwa ifahamike kwa kila mmoja ambaye ni Muislamu kuwa kupenda ni lazima kuwe kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka na kuchukia pia kuwe ni kwa ajili Yake. Haiwezekani kwa Muislamu kuwa Muislamu wa kihakika ikiwa atakuwa anayaendea maaswiya na mambo ya madhambi. Tufahamu kuwa katika huu ulimwengu unalofanya utalaumiwa na waja lakini la muhimu ambalo tunahitajika tuzingatie ni kutopata lawama ya Muumba wetu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi mlioamini! Atakayeiacha miongoni mwenu Dini yake, basi Allaah Atakuja leta watu Anaowapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Allaah, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Allaah, Humpa Amtakaye. Na Allaah ni Mkunjufu na Mwenye kujua” (al-Maa’idah [5]: 54).

 

Inatakiwa tujue kuwa tuliyoyafanya kabla ya kusilimu yote yamefutwa, lakini ya makosa utakayo yafanya sasa yanaandikwa na yasiyowapita kabisa. Weka mawazo yako pamoja, tilia sana maanani nasaha za Allaah Aliyetukuka na Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na hayo ndiyo yatakayotufanya tufaulu kukubwa sana.

 

Naomba tusome pamoja yafuatayo:

 

1.        Imaam al-Bukhaariy na Muslim wametunukulia Hadiyth ifuatayo kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke huolewa kwa mambo manne: Kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na Dini yake. Chagua mwenye dini au utapata hasara”. Na ndivyo mwanamme anavyochaguliwa.

 

 

2.        Imaam at-Tirmidhiy naye ametunukulia yafuatayo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam): “Akikujieni mnaye mridhia Dini yake na maadili yake basi muozeni. Mkitofanya hivyo basi kutakuwa na fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa sana”.

 

Uchaguzi ni wako dada yetu kwani nasaha za hapo juu zipo wazi kabisa. Nasi tuko pamoja nawe katika kuichunga haki, hata hivyo itabidi ufuate mambo yafuatayo ili usighurike na shetani kiumbe ambaye haitaki Dini:

 

1.                  Kata mawasiliano na yule rafiki wako wa kwanza kwani huyo atakupeleka motoni baada ya kuongoka. Akikupigia simu mwambie wazi kuwa uhusiano wenu umeisha kwani hutaki kurudi katika dhambi. Watu wa maasiya ni muhimu kususiwa lau sivyo basi wataendelea tu huku wakiona kuwa wako sawa.

 

 

2.                  Ili kuweza kumsahau huyo rafiki wa kwanza fanya haraka kufanya nikaha na huyu wa pili aliyeshika Dini baada ya kuswali Swalatu Istikhaarah. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo:

 

 

Muda Wa Swalah ya Istikhaarah

 

Kwa Nini Tuswali Istikhaarah Na Iswaliwe Kwa Ajili Ya Nini - Ipi Du'aa Yake

 

Du’aa Ya Swaalatul-Istikhaarah Ni Kabla Ya Swalah Au Baada Ya Swalah?

 

 

 

Mkiwa wawili hivyo itakusaidia kuishikilia Dini kwani mtakuwa mnahimizana katika ya kheri. Na pia hilo litakufanya mwenzio wa kwanza aone basi yake yashakwisha. Usichelewe kwani kuchelewa kunaweza kukuweka pabaya.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupatie ujasiri na hima ya kuchagua la kweli na haki na kuweza kushikamana nalo.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share