002-Kutoa Zakaah: Utangulizi

 

Kutoa Zakaah: Utangulizi

 

Alhidaaya.com

 

Kutoa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Islam.Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Nguzo za Uislaam ni tano. Shahada kuwa hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, na Kusimaamisha Swalaah, na Kutoa Zakaah, na Kufunga mwezi wa Ramadhwaan na Kuhiji Makkah kwa mwenye uwezo wa kufika huko".

 

Kufaridhishwa kwa Zakaah ni jambo muhimu na tukufu sana kwa Waislam kwa sababu ya wingi wa faida yake na kwa ajili ya haja kubwa ya kuwepo kwa jambo hilo, kutokana na masikini na mafakiri wanaohitajia sana msaada wa ndugu zao wenye uwezo, kwani katika Kutoa Zakaah uhusiano mzuri unajengeka baina ya Waislam matajiri na Waislam masikini, na hii ni kwa sababu siku zote moyo wa mtu huelekea na kumpenda yule anayemfanyia wema na ihsani. Zakaah inasaidia pia katika kuzisafisha na kuzitakasa nyoyo.

 

Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo.  [At-Tawbah: 103]

 

Katika kutoa Zakaah au Swadaqah kunaizoesha nafsi katika kuwapendelea kheri watu wenye haja na katika kuwaonea huruma na pia kunaipatia nafsi baraka nyingi kutoka kwa Allaahu Subhanaahu wa Ta’aalaa.

 

Allaah Anasema:

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ

Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Sabaa: 39]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Allaahu Anasema: 'Ee mwana Aadam, toa na sisi tutakupa"

 

Anasema Ibn Uthaymiyn:

"Kutoa Zakaah ni jambo liliofaradhishwa katika Uislam, na ni nguzo muhimu sana baada ya Shahada mbili na Swalaah, na dalili ya kuwajibika kwake imo ndani ya Qur-aan na pia katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pamoja na ijmai ya Waislam, na yeyote anayeikanusha nguzo hii anakuwa Kafir aliyertadi katika Uislaam, na hukumu yake ni kutubishwa, na akitubu anasamehewa. Ama akikataa kutubu na akaendelea kuikanusha basi hukmu yake ni kuuliwa. Ama anayeifanyia ubakhili au akapunguza katika Zakaah yake, huyo anakuwa miongoni mwa madhalimu wanaostahiki adhabu ya Allaahu.

 

Allaahu Anasema:

 

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo.  Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika. [At-Tawbah - 34 - 35]

 

 "Miongoni mwa faida za kutoa Zakaah anazozipata mtu katika dini yake" anaendelea kusema Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah), "Ni kuitimiza nguzo katika nguzo za Kiislam, jambo litakalomletea mtu furaha katika dunia yake na katika akhera yake, na pia inazidi kumkaribisha mja kwa Rabb wake na kumuongezea Imani, kama ilivyo katika mambo yote ya kumtii Allaahu Subhanaahu wa Ta’aalaa."

 

Share