003-Kutoa Zakaah: Maana Ya Zakaah

 

Kutoa Zakaah:Maana Ya Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Zakaah ni ile haki Aliyoifaradhisha Allaah kwa Muislam katika mali yake anayotakiwa kuwapa wanaostahiki. Neno Zakaah, katika lugha (katika kamusi ya lugha ya Kiarabu) maana yake ni 'Kujitakasa', kwa sababu anayetoa Zakaah anataraji kuitakasa mali yake, nafsi yake na kupata baraka kutoka kwa Rabb wake.

 

Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]

 

Zakaah ni nguzo ya tatu ya Uislaam iliyofaradhishwa katika Qur-aan tukufu na katika mafundisho ya Nabiy mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa sababu ya umuhimu wake, Allaah ameitaja mara themanini na mbili katika Qur-aan kwa kuifuatanisha pamoja na Swalaah.

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomteua Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa gavana wa nchi ya Yemen na kadhi wao alimwambia:

 

"Unakwenda katika nchi ya watu wa Ahlul Kitab, kwa hivyo (kwanza) walinganie katika shahada ya Laa ilaaha illa Allaah na kwamba mimi ni Rasuli wa Allaah, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swalaah tano mchana na usiku, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swadaqah (Zakaah) za mali zao, zichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurejeshewa masikini wao, na kama wakitii juu ya hilo, usije ukachukuwa mali zao zenye thamani, na uiogope dua ya aliyedhulumiwa, kwani hapana kizuizi baina yake (dua hiyo) na baina ya Allaah". [Imesimuliwa na Ma-Imaamu wote wa Hadiyth]

 

Imesimuliwa pia na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Allaah amewafaradhishia matajiri wa Kiislam katika mali zao kiasi cha kuwatosha masikini wao. Na (masikini) wasingepata tabu ya njaa na mavazi isipokuwa kutokana na ubakhili wa matajiri wao. Jueni kuwa Allaah atawahesabia hesabu nzito sana na atawapa adhabu iumizayo".

 

Share