006-Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Sunnah)

 

Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Sunnah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mambo matatu naapa juu yake na nakuhadithieni Hadiyth muihifadhi (vizuri).

 

Mali haipungui kwa kutoka Swadaqah, na mtu anapodhulumiwa akasubiri, basi Allaah humuongezea utukufu, na mtu anapojifungulia mlango wa kuombaomba, basi Allaah humfungulia mlango wa ufakiri". [At-Tirmidhiy kutoka kwa Abuu Kabshah Al-Anmaary (Radhwiya Allaahu ‘anhum)]

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakika Allaah anazikubali Swadaqah na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anailea kama mmoja wenu anavyomlea nyumbu wake mpaka tonge (anayoitoa Swadaqah) inafikia ukubwa wa jabali Uhud". [Ahmad - At-Tirmidhiy na ameisahihisha]

 

Hadiyth hii inatujulisha kuwa mtu anapotoa Zakaah au Swadaqah, basi Zakaah hiyo inaingia mikononi mwa Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa kwanza, kabla haijaingia mikononi mwa masikini anayepewa, ikitufahamisha jinsi gani Allaah anavyoitukuza ‘Ibaadah hii ya Kutoa Zakaah na jinsi anavyompenda mja wake mwenye kutoa Zakaah au Swadaqah hata akaipokea kwa mikono yake Mwenyewe Subhanaahu wa Ta’aalaa kwanza, akaizidisha jaza yake na kuifanya iwe na ukubwa wa Jabali Uhud.

 

Anasema Waki’iy:

 

"Hadiyth hii pia inasadikisha kauli yake Subhanaahu wa Ta’ala katika Qur-aan pale Aliposema:

 

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ

Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayepokea tawbah ya waja Wake, na Anapokea Swadaqah. [At-Tawbah: 104]

 

Na Aliposema:

يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ 

Allaah Huifuta baraka (mali ya) ribaa na Huzibariki swadaqah.[Al-Baqarah - 276]

 

Imepokelewa kuwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Mtu mmoja kutoka katika kabila la Bani Tamiym alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:

 

"Ee Rasuli wa Allaah, mimi nina mali nyingi na nina jamaa wengi na wageni huja kwangu kwa wingi. Kwa hivyo nijulishe nini nifanye na vipi nitowe?"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 

"Utoe Zakaah kutoka katika mali yako, kwa sababu hiyo ni tohara itakayokutahirisha, na uwaendee watu wako (ndugu zako wa nasaba), na uijue haki ya masikini na ya jirani na ya muombaji". [Ahmad]

 

Na Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mambo matatu naapa juu yake, Allaah hawezi kumfanya aliye na sehemu yake katika Uislam akawa sawa na yule asiye na sehemu. Na sehemu za Uislaam ni tatu. Swalaah, Funga na Zakaah. Na Allaah Anapokuwa pamoja na mja wake hapa duniani, basi huko akhera hamuachi akawa na mwengine asiyekuwa Yeye. Na mtu anayewapenda watu hapa duniani, basi siku ya Qiyaamah Allaah Atamjaalie awe pamoja nao…" [Ahmad]

 

Na kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Mtu mmoja alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam);

"Ee Rasuli wa Allaah; Unasemaje juu ya mtu anayetoa Zakaah ya mali yake?"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Atakayetoa Zakaah ya mali yake, keshaiondoa shari yake".

 

Share