007-Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Qur-aan)
Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Qur-aan)
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo. Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika. [At-Tawbah: 34 – 35]
Na akasema:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Aal-‘Imraan: 180]
Katika aya hii, Allaah Amesema "Watafungwa kongwa" badala ya "Watakuja kufungwa kongwa".
kwa ajili ya kutujulisha ukaribu wa mtu kukumbana na adhabu hizo. Kwa sababu mtu akeshakufa tu Qiyaamah chake kishasImaama, na kuanzia hapo mpaka siku ya Qiyaamah ataanza kukumbana na baadhi ya adhabu kutokana na yale maovu aliyoyatenda.
Wangapi wametoka majumbani mwao kwa miguu yao wenyewe, wakarudishwa wakiwa wamebebwa. Wangapi walifunga wenyewe vifungo vya suruali zao, wakaja kufunguliwa na waoshaji maiti.
Mwanaadamu anapotafakari juu ya wale wanaobebwa juu ya majeneza kila siku na kupelekwa makaburini wakiacha mali zao nyingi nyuma yao, mali zitakazokuja kufaidiwa na warithi, ataona namna gani yeye alivyohangaika kuichuma mali hiyo na nani atakayekuja kufaidika nayo, na nani atakayehesabiwa juu ya mali hiyo.
Ikiwa mali imepatikana kwa njia zisizokuwa za halali au ikiwa mali hiyo haikutolewa ndani yake haki ya Allaah, basi mali hizo watasatarehe nayo warithi, na yule aliyechuma ndiye atakayeulizwa naAllaah na kuhesabiwa.
Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa Akamaliza Aayah hii kwa kusema:
وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
"Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. NaAllaah ana khabari za yote mnayoyafanya."
Na maana yake ni kuwa hata kama utawaachia mali hiyo watu wako, wao pia watakuja kufa na watakaokuja baadaye nao watakufa, na mwisho kabisa hapana atakayebaki isipokuwa Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa, siku atakayozirithi mbingu na ardhi na kila kilicho juu yake.