009-Kutoa Zakaah: Hukmu Ya Asiyetoa Zakaah

 

Kutoa Zakaah: Hukmu Ya Asiyetoa Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Kutoa Zakaah ni fardhi, na ni katika mambo waliyokubaliana 'Ullamaa wote kuwa yeyote anayeikanusha fardhi hii anakuwa kesha toka katika dini akiwa ni kafiri aliyertadi, isipokuwa kama mtu huyo ni Muislam mpya, na kwa ajili hiyo husameheka kutokana na kutoelewa kwake.

 

Ama yule anayeacha kutoa Zakaah lakini wakati huo huo hakanushi kuwajibika kwake, huyo anapata dhambi ya kuacha kuitoa, lakini kuacha huko hakumtoi katika dini, isipokuwa ikiwa anaishi katika nchi inayohukumiwa na shariy’ah ya Kiislam, basi anayehukumu atatakiwa aichukuwe Zakaah hiyo kwa nguvu.

 

Ipo ikhtilafu baina ya 'Ulamaa iwapo anayeacha kutoa Zakaah atozwe gharama kwa kuacha kwake huko kwa ajili ya kumtia adabu, na gharama yenyewe ni kuchukuliwa nusu ya mali yake, na hii inatokana na Hadiyth iliyotolewa na Imaam Ahmad na Annasaiy na Abu Daawuud na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy kutoka kwa Bahza bin Hakim kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema:

 

"Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"…Atakayekataa (kutoa Zakaah) tutaichukuwa (kwa nguvu, na pia tutachukua) pamoja na nusu ya mali yake haki katika haki ya Rabb wetu Mtukufu na watu wa Aali Muhammad si halali kwao kuchukuwa chochote katika hiyo (Zakaah)".

 

[Amesema Imaam Ahmad kuwa isnadi ya Hadiyth hii ni sahihi na amesema Al Hakim kuwa hii ni Hadiyth sahihi].

 

Hata hivyo wapo baadhi ya maulamaa walioidhoofisha Hadiyth hii na wengine wakasema kuwa hukmu hii ilifutwa baadaye, wakiegemea baadhi ya Hadiyth zinazoelezea juu ya baadhi ya watu waliochelewa kulipa Zakaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwachukulia nusu ya mali zao.

 

Ama ikiwa watu watakataa kutoa Zakaah wakiwa wanaelewa kuwa ni jambo la wajibu, na ikiwa zipo nguvu za kuweza kupambana nao, basi watapigwa vita mpaka wakubali kuitoa. Na hii inatokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim kuwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Allaah Muhammadan RasuluLLaah, na wasimaamishe Swalaah na watoe Zakaah. Wakishafanya hivyo, damu yao na mali yao zitakingika kwangu isipokuwa katika kulipa haki za Kiislam, na hesabu yao iko kwa Allaah".

 

Imeelezwa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa; Alipofariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abuu Bakr akawa (Khalifa), baadhi ya waarabu walikataa kutoa Zakaah, na Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alitayarisha jeshi la kupambana nao.

‘Umar akasema (kumuuliza Abuu Bakr):

 

"Vipi unataka kupigana vita na watu (Waislam), wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Allaah na atakayetamka hayo itakingika kwangu mali yake na nafsi yake isipokuwa katika haki yake (anayodaiwa au kisasi kwa makosa aliyofanya), na hesabu yake iko kwa Allaah?”

 

Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Wa-Allaahi nitampiga vita yeyote atakayetenganisha baina ya Swalaah na Zakaah, kwa sababu Zakaah ni katika 'haki yake' (shahada hiyo). Wa-Allaahi lau kama wataacha kunipa mbuzi mdogo (na katika riwaya nyingine 'Kamba') iliyokuwa ikilipwa wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ningewapiga vita kwa kukataa kwao kuitoa".

 

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Wa-Allaahi nilipoona kuwa Allaah amemfungulia Abu Bakr kifua chake aamue kuwapiga vita, nikajuwa kuwa yuko katika haki".

[Muslim - Abuu Daawuud - na At-Tirmidhiy na Maimaamu wengine wa Hadiyth]

 

Share