010-Kutoa Zakaah: Wanaowajibika Kutoa

 

Kutoa Zakaah: Wanaowajibika Kutoa

 

Alhidaaya.com

 

 

- Muislam anayemiliki Niswaab, nacho ni 'Kiwango maalum cha mali’ kilichowekwa na shariy’ah katika aina yoyote ile ya mali inayowajibika kuitolea Zakaah.

 

- Niswaab hiyo lazima iwe ishatolewa ndani yake mahitajio ya dharura ya lazima kama vile chakula, mavazi, makazi, vyombo vya nyumbani, chombo cha usafiri na vyombo vyake vya kufanyia kazi, madeni n.k.

 

- Lazima kiwango hicho kiwe kimemilikiwa kwa muda wa mwaka mzima (mwaka wa Kiislam) bila kupungua katika wakati wowote ule ndani ya mwaka huo, na kama kitapungua katika wakati wowote ule kabla ya kutimia mwaka, basi hesabu nyingine mpya itaanzwa kuanzia pale kinapokamilika tena Kiwango hicho.

 

Amesema Imaam An-Nawawiy:

 

"Madhehebu yetu na madhehebu ya Imaam Malik na Ahmad na ya ‘ulamaa walio wengi ni kuwa; Mali inayotolewa Zakaah kwa ajili yake, kama vile dhahabu, fedha na wanyama wa kufugwa, lazima kiwango chake kibaki kwa muda wa mwaka mzima bila kupungua. Na wakati wowote ule kitakapopungua, basi mwaka wake unakatika, na wakati wowote ule kitakapotimia tena, unaanza kuhesabiwa mwaka mwingine".

 

Ama Abuu Haniyfah anasema:

 

"Kinachotakiwa ni kuwepo kwa Kiwango (Niswaab) mwanzo wa mwaka na mwisho wake, na haidhuru iwapo kitapungua katikati ya mwaka, hata kama mtu alikuwa nazo Dirham mia mbili kisha zikapotea zote katikati ya mwaka na akabakiwa na dhirham moja tu, au kama alikuwa na kondoo arubaini wakapungua na akabaki mmoja tu, kisha mwisho wa mwaka akaweza kumiliki (Dirham) mia mbili kamili au (kondoo) arubaini kamili, basi itawajibika Zakaah kwa vyote".

 

Masharti haya hayahusiani na Zakaah za mazao na matunda, kwa sababu vitu hivyo Zakaah yake inatolewa siku ya mavuno.

 

Allaah Anasema:

وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

"Na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake". [Al-An’aam: 141]

 

Share