016-Kutoa Zakaah: Kuitanguliza

 

Kutoa Zakaah: Kuitanguliza

 

Alhidaaya.com

 

 

Inajuzu kuitanguliza na kuitoa kabla ya kufikia wakati wake hata kabla ya miaka miwili.

 

Anasema Ash-Shawkaaniy katika kitabu chake 'Naylul-Awtaar';

 

"Wanachuoni wengi kama vile Az-Zuhriy na Al-Hassan Al-Baswriy na Maimaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abuu Haniyfah wamejuzisha kuitanguliza Zakaah kabla ya kufikia wakati wake".

 

Ama Imaam Maalik na Sufyaan Ath-Thawriy na baadhi ya Wanachuoni wengine wameona kuwa haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati wake, wao wameziegemea zile Hadiyth zinazowajibisha kutoa Zakaah baada ya kukamilika mwaka.

 

Anasema Ibn Rushd:

 

"Ikhtilafu iliyopo baina ya Wanachuoni ni kuwa - Zakaah ni ‘Ibaadah au haki iliyowajibishwa kupewa masikini. Wanaosema kuwa Zakaah ni ‘Ibaadah, wao wameifananisha na Swalaah na wakasema kuwa haiwezekani kutolewa kabla ya kufikia wakati wake.

Ama wale wenye kuona kuwa ni haki iliyowajibika, wamejuzisha kuitoa kabla ya kufikia wakati wake ikiwa mtu mwenyewe amejitolea kufanya hivyo".

 

Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameegema madai yake katika riwaya inayosema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kuchukua katika mali ya Al-‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuitolea Zakaah kabla ya kufikia wakati wake.

 

Share