Ameacha Wake Wawili Watoto Watano Wakiume, Mke Aliyemtaliki Ana Watoto Watatu

SWALI:

 

Baba yetu amefariki karibu mwezi wa pili sasa na mirathi imepangwa kuzungumzwa baada ya kuisha eda za wake zake wawili. Ameacha watoto watano wakiume (watu wazima wenye familia zao) kutoka mke wa kwanza. Pia ameacha mtoto mmoja wa kiume (umri miaka 2) kutoka mke wa pili. halafu kuna mke alimtariki kitambo kabla ya kumuoa huyu mke wa pili, huko alizaa naye watoto watatu wa kiume (wote -umri chini ya miaka 10) vilevile baba alikuwa akiwalea wajuu zake wanne-3 wa kike, 1 wa kiume, watoto wa aliyefariki dada yetu (kutoka mke wa kwanza) SWALI NI KWAMBA NANI NI WARITHI HALALI WA HUYU ALIYEFARIKI NA NINI UWIANO WA MGAO WA MALI ZA ALIYEFARIKI KWA HAO WARITHI?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi ya warithi waliofiliwa na mume/ au baba yao. Wale ambao wanamrithi aliyefariki akiwa ni mwanamme kama ilivyo kwenu ni wazazi wakiwa hai, mke au wake zake na watoto wake kama alivyopanga Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan.

 

Kwa kuwa hamukutaja kama wazazi wa aliyefariki wapo kumaanisha kuwa wameshaaga, yaani hawapo tena duniani. Ikiwa si hivyo mtatueleza. Baada ya kueleza hayo ni kuwa wale watakaomrithi kulingana na ulivyoeleza ni:

 

  1. Wake zake wawili ambao wanamkalia eda, ama yule aliyetalikiwa hatapata chochote. Hawa wake wawili watagawa thumuni (1/8) ya mali ya mzee. Hii inamaanisha kila mke atapata nusu ya thumuni (1/16). Hii ni kulingana na kauli Ya Allaah Aliyetukuka: “Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumuni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni” (an-Nisaa’ [4]: 12).

 

  1. Ama watoto kwa kuwa wote ni wanaume watarithi sawasawa kilichobaki. Na watoto watakaorithi ni watoto wakiume watano kwa mke wa kwanza. Mtoto wa kiume wa miaka miwili wa mke wa pili na pia watoto wa tatu kwa mtalaka wake. Ama wajukuu hawatapa chochote kwa kuwepo watoto wake.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share