Mwanamke Anayo Haki Ya Kuwatii Wazee Wake Kudai Talaka Kwa Mumewe Ambaye Wamekaa Miaka Kumi Bila Kupata Kizazi?

SWALI:

Assalam Alaykum WarahmatuhLwah Wabarakatuh, Ni wajibu wangu kutoa shukrani kwenu za dhati kwa kazi yenu nzuri ya kuipeleka mbele dini ya Allwah Subhana HuwaTaala malipo yenu yawe pepo juu ya hilo amiin.

Suala langu ni kuwa je mwanamke anayo haki ya kuwatii wazee wake juu ya kudai Talaka kwa mumewe ambae wamekaa kipindi kikubwa kiasi cha miaka kumi 10 hawajapata kizazi?

Ikiwa ndio au hapana kuna dalili yoyote kutoka katika Qur-an au Sunnah za Bwana Mtume Salalwah Alayhim musaalaam. Natarajia kupata mashirikiana na jawabu zuri kutoka kwenu.

Maasaalaam


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mwanamke kuomba talaka kutoka kwa mume asiyezaa.

Hakika katika hilo mwanamke hafai kuwatii wazee wake kwani kufanya hivyo ni kuwatii katika maasiya. Na haifai kwa kiumbe kumtii kiumbe mwenziwe katika kumuasi Muumba.

Thawbaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Mwanamke yeyote mwenye kumuomba mumewe talaka bila ya sababu yenye nguvu, basi harufu ya Peponi ni haramu kwake” (Abu Daawuud). 

Mambo ya kufanya ni yafuatayo ili kutatua tatizo hilo kwani shida inaweza ikawa kwa mke mwenyewe na wala sio mume:

 

1.   Wanandoa wende kupimwa kwa daktari na kutazamwa tatizo lililopo.

 

2.   Ikiwa ni mume au mke basi wawe ni wenye kufanya dawa kwani inaweza kuwa ni ugonjwa na hakuna ugonjwa ila una dawa.

 

3.   Wanandoa wamuombe sana Allaah Aliyetukuka Awape mtoto wa kheri.

Na Insha Allaah Allaah Atawapatia mtoto wa kheri bila ya kuachana. Na hata kama hamkupata basi mjue kuwa huo ni mtihani kutoka kwa Allaah Aliyetukuka au kupata mtoto si kheri kwenu. Mshukuruni Allaah Aliyetukuka kwa hilo na hiyo itakuwa ni kheri kwenu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share