Kisa Cha Ardhi Ya Fadak: Baina Ya Abu Bakr Asw-Swiddiyq Na Faatwimah (رضي الله عنهما)

 

Kisa Cha Ardhi Ya Fadak: Baina Ya Abu Bakr Asw-Swiddiyq

 

 Imetafsiriwa na Muhammad Faraj (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Utangulizi

Mashia wanadai kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimdhulumu Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) binti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kukataa kumrithisha ardhi ya Fadak iliyoachwa na baba yake, na kwamba Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alizusha hadithi ya uongo aliyoisikia peke yake inayodai kuwa eti Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

“Sisi Rusuli haturithiwi, na kile tunachokiacha (baada ya kufa kwetu) ni Sadaka”.

 

 

Na kwamba kwa ajili hiyo Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuudhi Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kwamba mwenye kumuudhi Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amemghadhibisha Allaah.

 

 

Nini Fadak?

Fadak ni ardhi iliyokuwa ikikaliwa na Mayahudi katika nchi ya Hijaz, na inasemekana pia kuwa ardhi hiyo ipo Madina, karibu na mji wa Khaibar.

Baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kuuteka mji wa Khaybar uliokuwa ukikaliwa na Mayahudi, hofu iliingia ndani ya nyoyo za Mayahudi waliobaki, jambo lililowafanya wakubali kuandikiana mkataba na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), mkataba ambao ndani yake walikubaliana kuwa ardhi ya Fadak ichukuliwe na Waislamu, na kwa ajili hiyo ardhi hiyo ikaingia katika hukmu ya ‘Fai’y’, nayo ni mali aliyoleta Allaah kwa Nabiy wake bila kuitaabikia wala kutumia farasi wala ngamia, na kwa ajili hiyo ardhi hiyo ikawa milki ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَمَا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْهُمْ فَمَا أَوْجَفْتُمْ عَلَيْهِ مِنْ خَيْلٍ وَلَا رِكَابٍ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يُسَلِّطُ رُسُلَهُ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٦﴾

Na ngawira yeyote ile Aliyoifanya Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwao; basi hamkuyaendea mbio kwa farasi na wala vipando vya ngamia lakini Allaah Huwapa mamlaka na nguvu Rusuli Wake dhidi ya Amtakaye. Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza. [Al-Hashr – 6]

 

 

Nilimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) Akisema:

 

 

Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim na wengine kuwa baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki dunia, alikuja Bibi Faatwimah kwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhum) akidai urithi wake kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi sallam), na urithi huo ni ardhi ya Fadak na pia sehemu ya ngawira ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) aliyoipata katika vita vya Khaibar.

 

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:

 

‘Mimi nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

“Sisi (Rusuli) haturithiwi, tulichokiacha (baada ya kufa kwetu) ni Sadaka”.

 

 

Na katika riwaya nyingine iliyomo ndani ya Musnad ya Imam Ahmed kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alisema:

 

“Sisi Manabii haturithiwi”.

 

 

Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akamkasirikia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) huku akitoa dalili kutoka katika Qur-aan tukufu aya isemayo:

 

 

يُوصِيكُمُ اللَّـهُ فِي أَوْلَادِكُمْ ۖ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ ۚ 

Allaah Anakuamrisheni kuhusu watoto wenu. Mwanamume atastahiki mfano wa fungu la wanawake wawili. [An Nisaa:11]

 

Na akasema kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) amesema:

 

وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ ۖ 

Na Sulaymaan alimrithi Daawuwd;.. [An-Naml:16]

 

 

na Amesema juu ya Zakariyaa (‘Alayhis-salaam):

 

يَرِثُنِي وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ ۖ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيًّا ﴿٦﴾

Anirithi na arithi kizazi cha Ya’quwb, na Mjaalie Rabb wangu awe mwenye kuridhisha. [Maryam:5-6]

 

 

Kabla sijaendelea mbele ningependa kuashiria kwa ufupi tu, kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuichukua ardhi hiyo kwa manufaa ya nafsi yake, wala hakukitumia kile alichopata ndani ya ardhi hiyo kwa ajili ya watu wa nyumba yake, bali alikuwa akikusanya mali inayopatikana humo na kufanya kama alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa akiigawa baina ya watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), na kilichobaki akiitumia katika njia ya Allaah kwa manufaa ya Waislamu kama alivyosema Allaah katika Suratul Hashr katika aya tutakayoitaja kwa ukamilifu kila tukiendelea mbele.

 

 

Hadithi Hii Ni Sahihi?

Jambo muhimu la kulishughulikia hivi sasa ni usahihi wa hadithi hii aliyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ndani yake kuwa:

 

 

“Sisi Rusuli haturithiwi”.

 

 

Ikiwa hadithi hii aliyoitamka Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni sahihi, basi hatutokuwa na haki ya kumlaumu Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), bali hatuna budi kuikubali na kuacha upendeleo, kwani aliyetamka maneno hayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyetuletea Qur-aan kutoka kwa Rabb wake, na yeye ndiye mwenye kujuwa zaidi kuliko Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anha) na kuliko mtu yeyote mwingine.

 

 

Kwa hivyo sisi tunasema kuwa; Maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) tunayaweka juu kuliko maneno ya mtu yeyote mwingine awe mtu huyo mtukufu namna gani. Sasa ikiwa kweli Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ametamka maneno hayo, kwanini basi tumlaumu Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa kuyafuata na kuyatekeleza?

 

 

Ushahidi Ndani Ya Vitabu Vya Mashia

Hadithi hii ya kuwa Rusuli (‘Alayhim-salaam) hawarithiwi, ni sahihi na imo hata ndani ya vitabu vya Mashia na si katika vitabu vya Ma Sunni peke yao.

 

 

Sasa ikiwa hadithi hii ni sahihi na imo hata ndani ya vitabu vya Mashia, kwanini basi atuhumiwe Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ameitunga yeye hadithi hii na kwamba kwa ajili hiyo amemghadhibisha Bibi Faatwimah?

 

 

Imesimuliwa na Al-Kulayniy katika kitabu chake maarufu ‘Al-Kaafiy’ kuwa:

‘Abu ‘Abdillaah (Imam Ja’afar asw-Swaadiq) amesema:

 

 

‘Na hakika 'Ulamaa ni warithi wa Rusuli. Na hakika Rusuli hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa’.

Al-Kaafiy 1/42.

Imam Muhammad Baaqir al-Majlisiy katika kitabu chake kiitwacho Mir'at al – ‘Uquul 1/111 amesema kuwa hadithi hii ni sahihi.

 

 

Khomeini ameiandika hadithi hii katika kitabu chake kiitwacho ‘Al-Hukuumah al-Islamiyah’ (Serikali ya Kiislamu), na akaitumia kama ni ushahidi wa Wilaayat al-Faqiyh chini ya kichwa cha maneno; (Sahihat al Qaddah) aliposema:

 

 

‘Amesema ‘Aliy bin Ibraahiym kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Hammad bin Issa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Maymun al Qaddah kuwa Abu ‘Abdillaah (Ja’afar asw-Swaadiq (‘Alayhis-salaam) amesema:

 

 

‘Atakayefuata njia ya kutafuta elimu, basi Allaah atamrahisishia njia ya Peponi. Na 'Ulamaa ni warithi wa Rusuli. Na Rusuli hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa.’

Al-Kaafiy, kitab fadhl Al-‘Ilm, mlango wa Sifat al Ilm wa Fadhlihi, hadithi nambari 2

 

 

Na katika kitabu hicho hicho cha ‘Al-Hukuumah al-Islaamiyah’ ukurasa wa 133 Khomeini ameiandika hadithi nyingine iliyopokelewa kwa njia ya Muhammad Yahya kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin Iysa kutoka kwa Muhammad bin Khalid kutoka kwa Abu Abdullah (Imam Ja’afar asw-Swaadiq (‘Alayhis- salaam) kuwa amesema:

 

 

‘Hakika 'Ulamaa ni warithi wa Rusuli, na hii ni kwa sababu Rusuli hawaachi Dirham wa Dinari kwa ajili ya kurithiwa, bali wao wanaacha maneno yao’.

Al-Hukuumat al-Islaamiyah uk. 133

 

 

Kutokana na yaliyotangulia tunamaliza kwa kusema kuwa;

Si haki kutoikubali hadithi hii ya Kutorithiwa kwa Rusuli katika kadhia ya Fadak, na kuikubali katika kadhia ya Wilayat al Faqih, kama alivyoandika Khomeini na kabla yake Majlisi.

 

 

Kwa nini Mashia wawe wanaikubali kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) pale wanapotaka na waikatae pale wasipoitaka juu ya kujuwa kwao kuwa kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) haiwezi kubadilishwa na kiumbe chochote kile, hata kama kiumbe huyo ni binti yake na kipenzi chake?

 

 

Imepokelewa Kwa Njia Nyingi

Si kweli kusema kuwa hadithi hii imepokelewa kwa njia ya Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yake, na mwenye kumtuhumu Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anakuwa ama amekusudia kumsingizia uongo Sahaba huyu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi sallam), au ni mtu mjinga asiyeelewa elimu ya hadithi.

 

 

Inajulikana na kila mtu kuwa hadithi hii ni maarufu sana na imesimuliwa na Swahaba wengi sana wakiwemo ‘Umar, ‘Uthmaan, ‘Aliy, Twalhah, Az-Zubayr, Sa’ad, Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Al-‘Abbaas bin ‘Abdul Muttalib, wake wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Hurayrah na wengine (RadhwiyAAllaahu anhum), na riwaya zote hizo ni sahihi zilizothibiti katika vitabu vya Ahlus Sunnah.

 

 

Kwa hivyo kauli hii imesimuliwa na Swahaba wengi (Radhwiya Allaahu ‘anhum) katika vikao mbali mbali, na hapana hata mmoja aliyeikanusha, bali wote waliikubali na kwa sababu hii hapana hata mmoja kati ya wake zake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuja kudai urithi wake, na hata ami yake alipokumbushwa juu ya hadithi hiyo hakushikilia kuutaka urithi, na kila aliyekuja kutaka urithi alikuwa akikubali mara anapokumbushwa juu ya hadithi hii, na hali hii ikaendelea bila kubadilika hata ulipofika wakati wa ukhalifa wa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye hakuwarithisha mali hiyo wanawe kama tutakavyoona kila tukiendelea mbele.

 

 

Ifuatayo ni mojawapo ya hadithi iliyomo ndani ya Al-Bukhaariy na ndani ya vitabu vingine inayotujulisha kuwa hadithi hii ni maarufu miongoni mwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum)

 

 

Anasema Malik bin Aus (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

‘Nilikuwa nimekaa nyumbani kwa ‘Umar na mtumishi wake Yarfa akaja na kumwambia ‘Umar:

‘Uthmaan na ‘Abdur-Rahmaan na Az-Zubayr na Sa’ad wanataka kukuona, niwaingize?’

‘Umar akasema:

‘Waache waingie’.

Kisha akaja tena na kumwambia ‘Umar:

“Niwaingize ‘Aliy na ‘Abbaas?”

‘Umar akasema:

“Waache waingie”.

‘Abbaas (baada ya kuingia) akasema:

‘Ewe amiri wa Waislam, nakutaka uhukumu baina yangu na mtu huyu (Ali juu ya mali ya urithi)’.

‘Umar akasema (kuwauliza Othman na ‘Abdur-Rahmaan na Az-Zubayr na Sa’ad):

‘Nakuombeni kwa ajili ya Allaah ambaye kwa amri Yake mbingu na ardhi zimenyanyuka; Nyinyi si mnajuwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

‘Sisi haturithiwi na tunachokiacha (baada ya kufa kwetu) ni sadaka? Na kwamba alijikusudia nafsi yake?’

Wakajibu:

‘Kweli alisema hayo’.

Kisha ‘Umar akawageukia Ali na ‘Abbaas akawauliza:

‘Nyinyi nyote (wawili wenu) si mnajuwa pia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alisema hayo?’

Wawili wao wakasema:

‘Kweli amesema hayo?

‘Umar akasema:

‘Sasa niacheni nizungumze nanyi juu ya jambo hili; Allaah alimchagua Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi sallam) kuisimamia Fa'iy hii”, na akamhusisha nayo yeye peke yake na si mtu mwengine yeyote, kama Allaah alivyosema:

 

 

وَمَا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْهُمْ فَمَا أَوْجَفْتُمْ عَلَيْهِ مِنْ خَيْلٍ وَلَا رِكَابٍ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يُسَلِّطُ رُسُلَهُ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٦﴾مَّا أَفَاءَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ فَلِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنكُمْ ۚ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

 

Na ngawira yeyote ile Aliyoifanya Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwao; basi hamkuyaendea mbio kwa farasi na wala vipando vya ngamia lakini Allaah Huwapa mamlaka na nguvu Rusuli Wake dhidi ya Amtakaye. Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza. 7.  Ngawira Aliyotoa Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Allaah na Rasuli na kwa ajili ya jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na msafiri aliyeharibikiwa, ili isiwe mzunguko wa zamu baina ya matajiri tu miongoni mwenu. Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al Hashr - 6-7]

 

 

‘Umar akaendelea kusema:

‘Kwa hivyo ngawira ile alipewa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) peke yake. Wa-Allaahi hakuichukuwa yeye akakunyimeni nyinyi, bali alikuwa akikugawieni katika mapato ya ardhi hiyo mpaka ilipobaki mali hii.

 

 

Kwa hivyo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa watu wa nyumba yake katika mali hii matumizi yao ya mwaka mzima, kisha alikuwa akichukuwa kilichobaki ndani yake na kuijaalia kuwa mali ya Allaah (kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu).

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akaendelea hivyo maisha yake yote. Nakuombeni kwa ajili Allaah muniambie: Si mnayajuwa yote hayo?”

Wote wakasema:

‘Ndiyo’

Kisha ‘Umar akawauliza Ali na ‘Abbaas:

‘Nakuombeni kwa ajili Allaah muniambie:

‘Si mnayajuwa yote hayo?’

Wote wawili wakasema:

‘Ndiyo’.

 

 

Kisha ‘Umar akaongeza:

‘Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki dunia, Abu Bakr akasema:

 

 

‘Mimi ni Khalifa wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam), na akachukuwa dhamana na kufanya kama alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Na Abu Bakr alipofariki dunia, mimi (‘Umar) nikasema:

 

 

‘Mimi ni Khalifa wa Khalifa wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), nikawa kwa muda wa miaka miwili nafanya vile vile kama alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) na Abu Bakr. Kisha mkanijia wawili nyinyi (‘Aliy na ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na neno lenu likawa moja mkinishtakia juu ya jambo hili hili. Mlikuja kutaka sehemu yenu katika urithi wa bin ami yako na huyu (Aly) akitaka sehemu ya urithi wa mkewe kutoka kwa baba yake. Nikakuambieni: Mkitaka nitakupeni nyinyi dhamana hiyo, kwa sharti ile ile (kuwa mfanye vile vile alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa sallam) na alivyokuwa akifanya Abu Bakr na mimi).

 

 

(Sasa mnanitaka mimi nitowe uamuzi mwingine kinyume na uamuzi huo (wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

 

Wa-Allaahi naapa kwa Yule ambaye kwa amri Yake, mbingu na ardhi zimenyanyuka kuwa sitohukumu kinyume na hivyo mpaka Kiama kitakaposimama. Na kama mumeshindwa kuisimamia basi irudisheni kwangu na mimi sitoshindwa kukusimamieni’.

[Al-Bukhaariy – Muslim – At-Tirmidhyy – An-Nasaaiy – Ibn Maajah – Abu Daawuud na wengine.]

 

 

 

Katika hadithi hii tunapata faida zifuatazo;

 

 

1.     Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakusema uongo wala kuizuwa hadithi hii

 

2.     Swahaba wote walikuwa wakiijuwa pia

 

3.     Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiisimamia ardhi hiyo ya Fadak na kugawa mapato yake sawa kama alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), jambo ambalo hata ‘Aliy na Al-‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikiri.

 

 

Kwa hivyo mwenye kuikanusha hadithi hii anaonesha dalili ya ujahili wake au kukusudia kwake kumsingizia uongo Khalifa wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Du’aa ya Nabii Zakariyaa (‘Alayhi Ssalaam)

Kuhusu kauli ya Nabiy Zakariyaa (‘Alayhis-salaam) alipoomba du’aa akasema:

 

يَرِثُنِي وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ ۖ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيًّا ﴿٦﴾

 

Anirithi na arithi kizazi cha Ya’quwb, na Mjaalie Rabb wangu awe mwenye kuridhisha. [Maryam:6]

 

 

Kusema kuwa Nabiy Zakariyaa (‘Alayhis-salaam) alikusudia kuomba mrithi wa kurithi mali yake ni hoja isiyokuwa na uzito kutokana na sababu zifuatazo;

Haitokuwa vizuri kwa Mchaji wa Allaah wa kawaida tu kumuomba Allaah Amruzuku mtoto kwa ajili ya kurithi mali yake. Itakuwaje basi kwa Nabiy mtukufu kama Nabiy Zakariyaa (‘Alayhis-salaam) aombe mtoto kwa ajili ya kumrithi mali yake? Alichokiomba Nabiy Zakariyaa (‘Alayhis-salaam) ni mtoto atakayeweza kurithi matendo pamoja na daraja yake baada ya kufa kwake.

 

 

Inajulikana pia kuwa Nabiy Zakariyaa (‘Alayhis-salaam) alikuwa mtu masikini aliyekuwa akifanya kazi ya useremala. Utajiri gani basi atakaoupata kutokana na kazi yake hiyo hata amuombe Allaah amruzuku mtoto wa kuurithi.

 

 

Bali uhakika unaojulikana na kila mtu ni kuwa Rusuli yote (‘Alayhim-salaam) hawakuwa wakijiwekea chochote na kwamba kile wasichokihitajia walikuwa wakiwapa masikini.

 

 

Kwa ajili hiyo neno ‘al irth’ (urithi) linapotumika kwa ajili ya Rusuli (‘Alayhim-salaam) siku zote huwa ni kwa ajili ya urithi wa elimu au urithi wa utume na si kwa ajili ya urithi wa mali.

Kwa mfano;

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ

Kisha Tukawarithisha Kitabu wale Tuliowakhitari miongoni mwa waja Wetu.. [Faatwir – 32]

 

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)Akasema:

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

 

10. Hao ndio warithi. 11. Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuun:10-11]

 

 

Aayah hizi na nyingine zilizo mfano wake zinatufahamisha uzuri maana ya ile hadithi inayosema kuwa; Rusuli hawarithiwi mali, bali wanarithiwa elimu.

 

 

Nabii Sulaymaan alimrithi Nabi Daawuud (‘Alayhis-salaam)

Kutokana na ushahidi uliotangulia tunaweza kuifahamu vizuri maana ya kauli ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliposema:

 

وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ ۖ  ﴿١٦﴾

Na Sulaymaan alimrithi Daawuud.. [An-Naml:16]

 

 

Tunafahamu kuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa anatujulisha hapa juu ya urithi wa Utume na urithi wa Ilimu, na si urithi wa mali na mambo mengine ya kidunia.

 

 

Na inafahamika zaidi tutakapofahamu kuwa Nabiy Daawuud (‘Alayhis- salaam) alikuwa na wake wengi sana na watoto wengi pia, na hakutajwa hapa isipokuwa Nabiy Sulaymaan peke yake (‘Alayhis-salaam) aliyeurithi utume kutoka kwa babake.

 

 

Ungekuwa urithi uliokusudiwa katika aya hii ni urithi wa mali, kwa nini basi wasitajwe na ndugu zake pia?

 

 

Ungekuwa urithi uliokusudiwa katika aya hii ni urithi wa mali na mambo ya kidunia, pasingekuwa na umuhimu wowote wa kutajwa ndani ya Qur-aan, kwani ni jambo la kawaida katika mila zote na katika dini zote kwa mtoto kumrithi mwanawe na si kawaida ya Qur-aan kusema kwa mfano:

 

 

‘Fulani alifariki dunia na mwanawe akarithi mali yake’.

 

 

Urithi Wa Wanawake Katika Madhehebu Ya Ithna- ‘Ashariyah

Jambo la kushangaza ni kuwa katika madhehebu ya Kishia Ithna- ‘Ashariyah, wanawake hawaruhusiwi kurithi ardhi wala nyumba.

Katika Al-Kaafiy, kitabu maarufu kinachotegemewa sana na Mashia kilichoandikwa na Al-Kulayniy, mwanachuoni huyo ameuhusisha mlango maalum chini ya kichwa cha maneno;

‘Hakika wanawake hawarithi nyumba wala ardhi’.

 

 

Ndani ya mlango huo ameinukuu hadithi iliyosimuliwa na Abu Ja’afar kuwa amesema:

 

 

‘Hakika wanawake hawarithi chochote katika ardhi wala nyumba’.

Imeandikwa na At-Tuwsi pia katika At-Tahadhiyb na Al-Majlisi katika Bihaar al-Anwaar kuwa Maysar amesema:

 

 

‘Nilimuuliza Abu ‘Abdillaah (‘Alayhis-salaam) juu ya wanawake na haki zao katika urithi akasema:

 

 

‘Wana haki zao katika thamani ya udongo na ujenzi na mbao na miti tu, ama ardhi na nyumba, wao hawana haki ya urithi (wowote ndani yake).’

 

 

Na kutoka kwa Muhammad bin Muslim kutoka kwa Abu Ja’afar (‘Alayhis-salaam) kuwa amesema:

 

 

‘Wanawake hawana haki ya kurithi ardhi wala nyumba’.

 

Na kutoka kwa ‘Abdul Malik bin Aayun kuwa mmoja wa ma Imam alimwambia:

 

 

‘Wanawake hawana haki ya urithi katika ardhi wala nyumba’.

 

 

Ni jambo la kushangaza Wa-Allaahi! Vipi wanaweza kuzungumza juu ya kudhulumiwa kwa bibi Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kuwa eti amenyimwa urithi wa ardhi ya Fadak iliyoachwa na baba yake (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) wakati katika madhehebu yao, mwanamke hana haki ya kurithi vitu hivyo?

 

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Naye Hakuwarithisha Wanawe

Inajulikana kuwa alipotawala ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) naye pia hakuwarithisha ardhi hiyo watoto wa Bibi Faatwimah ambao ni Al-Hasan na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Hii ni dalili kuwa hata Sayiduna ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiijuwa vizuri na kuikubali hadithi hii isemayo; ‘Sisi Rusuli haturithiwi’, ama sivyo kwa nini basi awanyime wanawe haki ya urithi kutoka kwa mama yao alourithi kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

 

Yeye mwenyewe Ali (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ana hiari yake kama hana haja ya haki yake katika urithi huo, lakini wanawe ilimbidi awarudishie haki yao hiyo wanayodai kuwa walinyang’anywa na Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Sasa ikiwa ‘Aliy mwenyewe hakuirudisha ardhi hiyo kwa wenyewe, kwanini basi wanamlaumu Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu)?

 

 

Bali imepokelewa hadithi kutoka kwa Murtadha katika kitabu chake kiitwacho Ash-Shaafi’i fil Imaamah kuwa alipopewa Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ukhalifa wa Waislamu, watu walimwendea na kumkumbusha juu ya kuirudisha ardhi ya Fadak, lakini ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akajibu:

 

 

‘Kwa hakika ninamsitahi Allaah kuibadilisha amri na kurudisha kile alichokizuwia Abu Bakr, kisha ‘Umar akaiendeleza amri hiyo’.

 

 

Vichekesho

Katika kitabu cha Al-Kaafiy, kilichoandikwa na Al-Kulayniy imo hadithi ya kushangaza sana na ya kuchekesha, hii ikiwa ni dalili ya kwenda kwa kupepesuka na kujigonga huku na kule kama vipofu wale wanaoshikilia kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimdhulumu Bi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).

 

 

Hadithi inasema:

‘Abul Hassan (Imam ‘Aliy ar-Ridhwaa) alipokwenda kumtembelea Al-Mahdi alimkuta akiwarudishia watu haki zao zilizochukuliwa kwa dhulma. Imam Ridhwaa akamuuliza:

 

 

‘Na haki zetu tulizodhulumiwa, kwanini huturudishii?’

Al-Mahdi akamuuliza:

‘Ni nini hicho mulichodhulumiwa ewe Abal Hassan?’

Akajibu:

‘Allaah Alipompa Nabiy wake ushindi na kuiteka ardhi ya Fadak…’

Al-Mahdi akamwambia:

‘Hebu nielezee iwapi ardhi hiyo?’

 

 

Imam Ridhwaa akasema:

‘Sehemu moja ya ardhi hiyo ni mlima Uhud, na ya pili imefika mpaka Al-‘Ariysh iliyopo Misri na nyengine ni sehemu ya kandokando ya bahari na sehemu nyingine ni Dawmat al Jandal.’

Al-Kaafiy, bab al Fay wal Anfal 1/543 na pia katika Bihar al Anwar 48/156.

 

 

Itakuwaje basi kipande cha ardhi kilichopo Khaybar kikaweza kuwa na ukubwa wa kiasi hicho.

 

 

Mlima Uhud upo Madiynah, na Dawmat al-Jandal ipo karibu na mpaka wa Saudia na Jordan. Ama Al-‘Ariysh ni mji uliopo huko Misri karibu na mlima wa Sinai.

 

 

Bila shaka sisi hatuamini kuwa Ar-Ridhwaa alisema maneno kama hayo isipokuwa huu ni uongo mwingine wanaowazulia watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Bibi Faatwimah Hakumsemesha Tena Abu Bakr?

Kutokana na ushahidi nitakaoutaja hapo chini tutaona kuwa zile kauli zinazosema kuwa Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anha) hakumsemesha tena Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mpaka kufa kwake si kauli za kweli, bali ukweli ni kuwa alimsemesha na akaridhika naye kabla ya kufa kwake na ushahidi nitakaoutoa unatokana na hadithi zilizopokelewa kutoka pande zote mbili, yaani katika vitabu vya Mashia na vya Masunni.

 

 

Katika Fathul Bari 233/6, kitabu kinachosherehesha hadithi za Imam Al-Bukhaariy imeandikwa kuwa;

 

 

‘Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikasirishwa na Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu alidhani kuwa Abu Bakr aliyasikia maneno hayo kutoka kwa mtu mwingine na hii ndiyo sababu iliyomfanya akasirike na asimsemeshe tena.

 

 

Na maana ya neno ‘asimsemeshe tena”, ni kuwa hakumsemesha tena kuhusu jambo hili la ardhi ya Fadak, kwa sababu imepokelewa kutoka kwa Al-Bayhaqiy kutoka kwa Ash-Sha’abiy hadithi sahihi inayoondoa tatizo hilo na kutuhakikishia kuwa Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliacha kumkasirikia Abu Bakr na akamsemesha, isipokuwa Bibi Faatwimah alishughulika sana na huzuni ya kufiwa na baba yake, kisha aliumwa sana mpaka alipofariki dunia.

 

 

Ama katika vitabu vya Mashia, imeandikwa katika kitabu ‘Mihjaajus Swaalihiy’, na vingine kuwa Abu Bakr alipoona kuwa Bibi Faatwimah amemkasirikia akamuendea mpaka nyumbani kwake na kumwambia:

 

 

‘Maneno yako ni kweli, isipokuwa mimi nilimuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kukupeni nyinyi watu wa nyumba yake, akiwapa pia (katika mali hiyo) masikini na mafakiri na wasafiri wanaoishiwa. Nikataka kufanya kama alivyokuwa akifanya baba yako.’

 

 

Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akasema:

“Wa-Allaahi utafanya kama alivyokuwa akifanya?”

Akasema:

“Wa-Allaahi nitafanya hivyo – Rabb wangu shuhudia”.

 

 

Bibi Faatwimah Akaridhika, Na Abu Bakr Akawa Anawapa Haki Yao Ndani Yake Kisha Kilichobaki Akikigawa Kwa Wanaostahiki.

 

 

Hitimisho

Kwa kumaliza tunasema kuwa;

Baada ya kutambua kuwa hadithi ya kutorithiwa Rusuli (‘Alayhim-salaam) ni sahihi upande wa Masunni na upande wa Mashia, tunaelewa pia kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na haki alipokataa kumrithisha ardhi hiyo Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), kwani hata hiyo aya inayozungumza juu ya mali ya Fa’iy, basi Allaah ameikamilisha kwa kusema:

 

ۚ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

 

Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Hashr:7]

 

 

Tunaelewa pia kuwa urithi huo haukuwa haki ya Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) peke yake, bali ulikuwa wa watu wote wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) wakiwemo wake zake (Radhwiya Allaahu ‘anhunna) na hapana hata mmoja kati yao aliyekwenda kuidai baada ya kufahamu maana ya hadithi hiyo.

 

 

Swahaba wengi (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakiijuwa hadithi hiyo akiwemo Aliy bin Abu Talib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye hata alipotawala, yeye pia hakuirithisha ardhi hiyo, bali aliendelea kufanya kama alivyokuwa akifanya Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anha) alimkasirikia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipodhani kuwa hakuisikia hadithi hiyo kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) lakini alipouelewa uhakika aliridhika na akaacha kuendelea kumkasirikia Abu Bakr.

 

 

Share