Kusema كَرَّم اللَّه وَجْهَه Unapomtaja 'Aliy Inajuzu Au Lilo Sahihi Ni Kusema رضي الله عنه?

 

Kusema كَرَّم اللَّه وَجْهَه (Karrama Allaahu Wajhahu) Unapomtaja 'Aliy Inajuzu

 

Au Lilo Sahihi Ni Kusema رضي الله عنه (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum! Nalileta suali langu nikitaka usaidizi wenu! Niliwahi kuongea na mtu kuhusu mas-ala ya bid-a akaniambia hata hilo neno la karramallahu wajhahu analokusudiwa Sayyidna Ali radhiyallahu anhu ni bid-a akisema kua halikua wakati wa mtume alayhi swalatu wassalam wala katika wakati wa makhalifa wane. Jee, hili ni neno la kweli ama mwaeweza kunielimisha vipi kuhusu hili neno? Shukran!

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Qur-aan Tukufu tayari Ashatueleza fadhila na ubora wa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwa jinsi ambayo hatutakuwa na njia ya kuzua sifa nyingine kwa Swahaba wengine.

 

Sifa hiyo ya Maswahaba wote imetolewa katika Aayah ifuatayo:

 

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu [At-Tawbah 9: 100].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Aayah hii Amewakusanya wote kwa kusema: “Radhwiya Allaahu ‘anhum”.

 

Kwa hivyo, sifa hii ya Karrama Allaahu wajhahuu haipo katika Qur-aan, wala hakupatiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala kupatiwa na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wenyewe. Hii ni sifa aliyopatiwa baadaye kutaka kuonyesha kuwa yeye alikuwa juu ya Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wengine wote. Na ikiwa wanaomuita hivyo, wanasema kuwa anastahiki sifa hiyo kwa kuwa uso wake haukusujudia sanamu basi wapo pia Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wengine wengi ambao hawakusujudia sanamu kwa hivyo nao wangepatiwa sifa kama hiyo lakini hawakupatiwa.

 

Kwa hiyo, turidhike na sifa Aliyowasifia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na tuache sifa nyingine za bid’ah ambazo mara nyingi utakuta zikitumiwa na watu wa bid’ah na wale wanaomtukuza sana ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuliko Maswahaba wengine nao ni Mashia

 

Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) anasema katika Tafsiyr yake: “Nasema: Ni jambo lililoonea katika wenye vitabu vingi ambao wanaandika (‘Alayhis Salaam) baada ya jina la ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) pekee na si kwa Swahaba wengine, au utakuta wanaandika Karrama Allaahu wajhahu. Pamoja na kuwa maana yake inakubalika, Swahaba wote walikuwa wanapaswa kupewa heshima kama hiyo. Mashaykh wawili (Abu Bakr na ‘Umar) na Amiyrul Muuminiyn ‘Uthmaan walikuwa wanastahiki zaidi kuitwa hivyo, (Radhwiya Allaahu ‘anhum) Allaah Awaridhie wote.” Tafsiyr Ibn Kathiyr, Mj. 3/517-518.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share