Sehemu Zake Za Siri Taabaan, Katika Miezi Mitatu Anafanya Mara Moja Tu Tena Kwa Mashaka, Je, Ana Jini Mahaba?

SWALI:

 

ASALAMU ALAYKUM. Mashekhe wetu walimu wetu, Eweeeee; Mwenyenzi Mungu wajaalie watu hawa walimu hawa waislamu hawa, wanaojibu majawabu haya ya haki, wape muda mrefu wa kuishi kwa ajili ya kuiendeleza haki ndani ya dini yetu ya kiislamu AMINA YA RABI. Napenda kuuliza hivi, Kaka yangu ana matatizo ya [uume wake haufanyi kazi vizuri anaweza akachukuwa muda mrefu kama miezi mitatu na katika hiyo miezi mitatu ukafanya kazi siku moja tuu. na akitaka kufanya tendo la ndoa na mke wake uume unarudi [hausimami] na yumo kewnye ndoa si zaidi ya miaka miwili. Ameenda hospitali ameambiwa kuwa spams wake hawana nguvu amepewa dawa mambo yapo pale pale. Kilichotokea ameambiwa ana [jini wa mahaba]. Tunaomba ushauri wenu, au kama kuna tiba yoyote kutoka kwenu tafadhalini tunaomba.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu utaabani wa uume wa ndugu yako.

Hakika zipo sababu nyingi zinazomfanya mwanamme awe hafai kabisa kuhusiana na tendo la ndoa. Moja wa sababu ni mwanamme kuwa na ada za siri kama kujichua kwa kutumia mkono au kifaa chochote kile. Ada hiyo inamfanya mwanamme asiwe adhoofike katika kitendo hicho muhimu na cha ‘Ibaadah baina ya mume na mke. Na kutoweza mwanamme kufanya kitendo hicho inaweza mpelekea mke kudai talaka au mwengine asiye madhubuti kutafuta starehe nje ya ndoa ikiwa Imani yake ni dhaifu.

 

Ikiwa mmekwenda hospitali na mkapewa dawa lakini bila mafanikio inatakiwa nduguyo atafute tiba mbadala. Tiba hizo ni kwa mfano zile zinazoitwa za Kiswahili. Wapo matwabibu mahiri kabisa kuhusiana na masuala miongoni mwa wale waliobobea ima kwa kufundishwa na waalimu wao au kupata katika vitabu vya madaktari wa zamani wa Kiislamu. Tiba nyingine mbadala ambayo dawa kama hizo ni zile za Kichina au Kihindi. Wachina wamefungua hospitali zao nyingi katika miji mikubwa ulimwenguni na pia katika miji hiyo huweza kupata dawa za miti shamba katika maduka ya Wahindi ambao wamejikita katika kuuza dawa zao hizo. Jaribu hii ni njia ya pili na huenda Allaah Aliyetukuka Akaleta shifaa Yake.

 

Wakati huo huo unaweza ukampeleka nduguyo kwa Shaykh mcha Mungu aliye mahiri katika kazi ya kumsomea mgonjwa bila ya kuingiza ushirikina ndani yake. Kawaida huyu Shaykh atasoma kisomo cha shari’ah (Ruqyah) ili ibainike kama kweli ana jini au hana. Kwa kuweza kupata maelezo zaidi kuhusu kulala kwake huenda tukaweza kupata bayana hiyo. Kwa kawaida ni kuwa mume ambaye analala na jini kimapenzi anajisikia mchovu asubuhi na huwa anahisi anafanya kitendo cha kujamiiana na mwanamke asiyemuona. Ikiwa anayo hayo anaweza kwenda akasomewa. Na hata kama hahisi hayo anaweza kwenda kusomewa kwani kisomo cha Qur-aan ni dawa.

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

Mke Wangu Amevaliwa Na Majini Wa Mahaba? Hapendi Kutenda Kitendo Cha Ndoa Na Mimi

Naingiliwa Kwa Kitendo Cha Ndoa Na Majini

Mke Analalamika Mume Ana Mashetani Yanamfanya Asiweze Kukamilisha Tendo La Ndoa

Mume Au Mke Hawezi Tendo La Ndoa Kwa Zaidi Ya Miaka 5, Hukmu Ni Nini?

Mume Hamtoshelezei Matamanio Yake Ya Tendo La Ndoa, Anaomba Ushauri

 

Tunamuombea shifaa ya haraka nduguyo kwa ugonjwa alio nao.

 

Na Allaah Aliyetukuka Anajua zaidi

 

Share