Kuna Du’aa Ya Kumfanya Mume AtoeTalaka Kiwepesi?

SWALI:

 

Asallaam aleikum warahmatullah wabarakatu. MIMI NIMEOLEWA NA MUME WANGU HATUNA WATOTO KWA KIPINDI CHA MIAKA MITATU SASA MUME WANGU AMEKUWA JEURI NA WAKATI MWENGINE ANALALA NJE, AU ANALEWA, HASWALI, WALA  HANIHUDUMII KWA MASUALA YA KULA, KUVAA NA MALIPO YOYOTE YA NDANI MIMI NAFANYA KAZI MASAA MACHACHE NALIPIA KILA KITU MWENYEWE YEYE MSHAHARA WAKE SIJUI ANAUFANYA NINI NA MARA NYINGI ANANIKOPA PESA NA HANIREJESHEI. NIMEKAMATA SIMU ANA MWANAMKE NA KAMA MIEZI MITATU SASA MAMBO YAMEZIDI JEURI NA VITISHO. NIMEMWAMBIA ANIPE TALAKA YANGU MAANA KATIKA NAFSI YANGU NIMECHOKA NA MAUDHI YAKE NA NIKIWAMBIA WAZEE WAKE ANAGEUZA MANENO NA KUZIDI KUNITUKANA. JEE KUNA DUA YA KUMFANYA ATOWE TALAKA KWA HIYARI YAKE? MAANA AMESEMA HANIACHI LABDA ANITIE KILEMA KWANZA AU ANIHARIBIE MAISHA KWANI SISI TUNAISHI XXXXX  . AHSANTE


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu shida na maudhi unayopata kutoka kwa mumeo.

Hakuna du’aa ambayo tumeipata au kuiona au kuipitia inayomfanyia usahali mke anaposumbuliwa na mumewe aisome ili apate talaka kwa usahali.

 

Hata hivyo, Uislamu umeweka mipango kabambe ya kuweza kutatua matatizo hayo ya kinyumba. Lile ambalo unatakiwa kufanya ni kuitisha kikao ambamo wazee wako nao watakuwepo pamoja na wazee wake na yeye mwenyewe mumeo. Inatakiwa katika kikao hicho uelezee wazi wazi kuhusiana na anayoyafanya mumeo. Ama kama ulivyosema kuwa hapo mlipo ni Ulaya na huenda hamna wazee karibu, basi japo jamaa zenu wa karibu mnaweza kuwashirikisha na ikiwa hukupata natija yoyote ile inafaa uende kwa Qaadhi au Shaykh au Imaam na umwasilishie mashtaka yako, Qaadhi ndiye atakayeweza kukuachisha kwani sababu zote za nyinyi kutokuweza kuishi pamoja zipo wazi kabisa.

 

Tunakuombea kila la kheri katika juhudi zako hizo za kutaka kusalimika na mume ambaye hafuati hata Dini.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share