Ana Uzito Kufuata Maamrisho Ya Allaah, Vipi Anaweza Kurekebisha Iymaan Yake

SWALI:

Asalam Aleykum,

 Natumaini wote Mwenyezi Mungu amewajali afya njema kabisa.

Nipo katika mtihani mkubwa sana wa kujenga imani yangu. Katika kitu ambacho huwa naomba kila sk ni kuwa na Imani iliyokamili na yenye kumtumikia ALLAH ipasavyo. Tatizo linalonipata ni uzito wa moyo wangu katika kufata amari za Mwenyezi Mungu ikiwemo SWALA TANO na nguzo zinginezo. Nimejaribu kujifunza kusoma Kiarabu (Lugha Tukufu ya Qur-an) kupitia mtandao wa quranitukufu na alhamdulillah kidogo napata kuelewa.

Swali langu: Tafadhali naomba uniambie namna ambayo ni rahisi kubadilisha imani yangu kwani nahitaji sana kurudi katika Maamrisho ya Mwenyezi MUNGU.

 Natumaini nitapata jibu.asante.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema zamstahikia Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Rehma na amani zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako.

Kwa kweli hakuna kitu chenye kuitwa namna rahisi ya kubadilisha Iymaan. Kama ulivyosema kuna uzito wa moyo katika kufuata amri za Allaah hasa hasa Swalah tano na hii inathibitisha kuwa bado unahitaji kazi kubwa kuifanya ili kuweza kwa msaada wa Allaah kufikia kuwa na Iymaan yenye kupenda kutekeleza amri za Allaah, na hilo si jepesi kwani Allaah Anasema:

 

Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu, Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika watarejea Kwake” Al-Baqarah: 45-46

 

Unachotakiwa kujifunza sio lugha tu bali Iymaan na yakini kuwa hakika unahitaji kutekeleza amri za Aliyekuumba na kuwa na yakini kuwa utakutana Naye na Kwake Yeye utarejea na kuwa hapa duniani ni pahala pa kupita na salama ya mwanaadamu ni kutekeleza aliyoamrishwa na Mola wake.

 

Unachohitaji ni kumpenda Mola na Mtume Wake jambo ambalo litaweza kukusaidia kukufikisha pahala pa kupenda kutekeleza armi Zake Mola. Kupenda kitabu Chake ni jambo litalokupelekea kupenda kukisoma na kutekeleza unachokisoma; kuwapenda wenye kumpenda Allaah na Mtumewe ni jambo litalokusaidia kuweza kufikia kuwa tayari kuwasikiliza na kupenda kukaa nao na kuwa karibu nao wakati mwingi.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

Swalah, Umuhimu Wake, Fadhila Na Hukmu Ya Mwenye Kuacha 

Imani Yangu Inapungua Nakhofu Kupotoka Nifanyeje?

Anaomba Toba Kisha Anarudia Tena Kufanya Kosa Kila Mara. Vipi Aweze Kuimarika Bila Kurudi Makosani?

Nataka Kutubu Lakini Shaytwaan Kanivaa Nifanye Nini?

Nataka Kutubia...Lakini!!

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share