Kukimu Katika Swalaah ya Faradhi Na Sunnah

SWALI LA KWANZA:

 

Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh,Sheikh  shukran kwa majib ya maswali yangu niliyouliza inshaallah Mwenyezi Mungu Azza Wa Jalla awalipe mema hapa duniani na huko Akhera kwa kazi yenu ya kujitolea ya kutuongoza.

 

Sheikh sikuwa na nia ya kurudi tena hapa lkn kwa ihsani yako naomba unitupie jicho kidogo utata nilionao, kwani sikupata majibu yake ktk viungo ulivyonitumia.  

 

kwanza, kuhusu Iqama Je hii iqama ni kwa ajili tu ya kuswali swala ya fardhi au unaqimu unaposwali sunna Mfano,mimi ninapoanza kuswali sunna kablia ya adhuhuri hukimu,na nikianza rakaa nyengine 2 hukimu, nanikiswali rakaa4 fardhi hukimu na naendelea hivyo kukimu rakaa2 za sunna. Je ndivyo au nakosea

 

SWALI LA PILI:

 

Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh inshaallah Mwenyezi Mungu awalipe mema kwa kazi yenu ya kutuelimisha Suala langu ni kuhusu Iqama. Je iqama ni kwa ajili ya swala za sunna na za fardhi, mfano kama naswali swala ya adhuhuri na sunna zake inanibidi kila nikitoa salaam nikianza swala nyengine nikimu


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu kukimu katika Swalaah tofauti – za faradhi na Sunnah.

 

Hakika ni kuwa Iqaamah ni kwa ajili ya Swaalah ya faradhi peke yake na si Sunnah, kwani kinachotakikana ni kuwa Swaalah hiyo ya faradhi ijulishwe kuwa itayari na watu nao waanze kujipanga kwenye Swafu.

 

Ama Swaalah za Sunnah kila mtu huswali peke yake, na ni uzuri mtu kuziswalia nyumbani kwake hivyo hakuna haja ya Iqaamah kwani hakuna mwenye haja ya kujulishwa kujitayarisha au kupanga Swafu kwani kila mtu anajiswalia peke yake.

 

Inatakiwa baada ya Kuadhiniwa ndio unaswali Qabliyah, kisha baada ya hapo ukifika wakati wa Kuqimiwa kunaqimiwa na kuswali Swalaah ya faradhi. Na baada ya Swalaah ya fardh unafanya dhikr kisha unaswali Swalaah ya ba’adiyah kama ni Adhuhuri au Magharibi au ‘Ishaa.

 

Na hata ikiwa Swalaah ya Sunnah inaswaliwa kwa Jama’ah kama vile Swalaah ya Taraawiyh, hakuna Iqaamah kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya hivyo au kutufundisha sisi tufanye hivyo.

 

Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate manufaa zaidi:

 

Swalah Ya Safari Inaadhiniwa na Kukimiwa?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share