Fatwa ya Mufti Kuruhusu Kutokufunga Ramadhaan Kulinganisha Mpira na Jihadi

SWALI:

 

asaslam alaikum warahmatullahi wa barakatu, ndugu zangu sheikh, mimi ni nasuali lifuatalo: juzi ijuma ya tariki 15 ramadhani yaani 05/09/2009 mufti wa nchi ya rwanda alikamata FATWA dhidi ya swaumu, yaani aliwapa RUHUSA wa jeza mpira wa miguu katika team ya taifa ya rwanda RUHUSA YA KULA Mchana kwa kisingizio eti nao katika kucheza mpira ni kama kuwa wako MUJIHADI.

ndugu zangu naomba mnijibu kama kweli uyu mufti wa rwanda anao haki ya kukamata fatwa kama iyi, aya mambo yalipita kwenye RADIO CONTACT kwenye habari za mpira, ambapo watangazaji walisema kuwa TUNAMUSHKURU MUFTI WA RWANDA KUWA ALIPATIYA RUHUSA YA KULA MCHANA WACHEZA MPIRA WA KIISLAM........


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu fatwa iliyotolewa kuhusiana na ruhusa kwa wachezaji wa mpira kula Ramadhaan.

Kwanza ikiwa ni kweli hayo uliyoyaeleza, hakika ni makosa kwa Mufti au Shaykh yeyote yule kufananisha mpira na Jihaad. Hayo ni mambo mawili ambayo hayalingani kabisa. Huwezi kulinganisha watu wenye kwenda kutoa roho zao kwa ajili ya kuihami Diyn ya Allaah na watu wenye kukimbizana uwanjani wakiufukuza na kugombaniana mpira.

 

Kwa hakika si sawa Waislamu kuacha kufunga Ramadhaan kwa ajili ya mechi ya mpira. Ni makosa ambayo Mufti huyo amefanya na inafaa arudi kwa Allaah Aliyetukuka na kuomba msamaha.

Mambo ya mpira si masuala ya kuwashughulisha Waislam hata kufikia hali ya kuacha 'Ibaadah zao takatifu kama Swawm au Swalaah. Wengi Waislamu wamepumbazika na upuuzi huo kiasi cha kuacha wajibu wao katika kuitumikia Diyn yao.

Hata hivyo, hakuna ubaya mtu kucheza mpira kwa kuuweka mwili wake katika hali ya ukakamavu maadam atachunga nyakati za Swalaah na kujistiri mwili wake vizuri anapocheza na bila kuingia kwenye michuano au mashindano yenye kusimamiwa au kudhaminiwa na mambo ya haraam kama kampuni za pombe, kamari, na njia zozote za chumo la haraam. Au hata kuvaa fulana za kutangaza mambo kama hayo ya pombe, kamari, benki za ribaa na mfano wa hayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share