Ramadhwaan Imemalizika Lakini Allaah Yupo Hai Kuabudiwa

 

Ramadhwaan Imemalizika Lakini Allaah Yupo Hai Kuabudiwa

 

Sulaymaan Ibn ‘Abdir-Rahmaan

 

Alhidaaya.com

 

 

Watukufu waislamu tumemaliza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhwaan na sote ni mashuhuda wa nafsi zetu namna tulivyokuwa tukijipinda katika kuyaendea mambo ya kheir na kuyaacha mambo mabaya Aloyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Aidha kila mmoja alijibadilisha mwenyewe kimatendo, tabia, mavazi, ibada na kadhaalika, aidha kila mmoja, alikuwa Muislamu hasa kwa muonekano wa nje na pia muonekano wa ndani, nyoyo zilikuwa safi, huruma zilitujaa, tuliacha matamanio ya nafsi zetu kwa ajili ya Allaah,  wema ulituvaa na kumsaidia tumjuaye na tusiyemjua.  Tulifanya hivi tukiamini ni wajibu wetu kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kisawasawa na kwa namna ile Anayotaka Yeye Allaah, kwani Yeye ndiye Aliyetuumba na Ametuumba ili tumuabudu, hivyo ilikuwa ni haki yetu kuhakikisha  lazima tumuabudu kama Alivyoagiza.

 

Ikiwa hivi ndivyo tulivyokuwa ndani ya mwezi wa Ramadhwaan, hili khaswa ndio lengo la Ramadhwaan, kama Alivyoainisha mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwamba lengo la Ramadhwaan ni kuwafanya waumini wawe wacha Allaah, Allaah anasema katika Qur-aan:

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah:183]

 

Ama kweli tulikuwa wacha Allaah, tuliacha matamanio ya nafsi zetu kwa ajili ya Allaah, (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tungeweza kufanya lolote kama vile kula, kunywa, kufanya uzinifu, kulewa, kustarehe na wake zetu, na kufanya mengine kadhaa ya halali na ya haramu, lakini tulijizuia sisi wenyewe, bila kusimamiwa na nguvu yoyote ile, kila mtu aliichunga nafsi yake kuhakikisha hafanyi ila Aliloruhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na kila la Alilolikataza tuliliacha bila kulazimishwa na mtu ama kusimamiwa na nguvu  yoyote, hapa yafaa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na tumuombe Aikubali ibada yetu ya Ramadhwaan na zinginezo.

 

Ninachokusudia katika waraka wangu huu, ni kuwanasihi na kuwauisa kama ninavyo jinasihi mimi mwenyewe kuwa, Ramadhwaan imekwisha   na imeshaondoka, lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Yupo hai, halali wala hasinzii. Ashuhudia kila tunachofanya na tunachosema, hivyo Yeye ndio wakuogopwa na wa kuheshimiwa.

 

Aidha, anasema mmoja katika watu wema: “Ewe ndugu yangu, tutajibu nini tutakapoulizwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hali ya kuwa Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ashuhudia kila tufanyalo, tumegahfilika na kufuata maamrisho Yake na kuacha makatazo Yake,  kama tunazo akili madhubuti, sasa ndio wakati wa kufanya maandalizi mazuri, na kutumia umri wetu huu ulobaki katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)”

 

Anakusudia msemaji kutukumbusha kuwa kuutumia vema umri wetu huu katika kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Enyi ndugu zangu, tutambue yakuwa, haya maisha ya dunia ni mpito, hivyo tuiandaye safari yetu. Watukufu Waislamu, ieleweke ule ucha Allaah tulokuwa nao ndani ya Ramadhwaan ndio iwe dira ya mfumo wetu wa maisha yetu ya kila siku, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Anatutaka tuishi vile na si venginevyo.

 

Kama uliacha kula chakula cha halali umehangaika wewe mwenyewe kukitafuta, lakini ukaacha kula mchana wa Ramadhwaan wewe mwenyewe kwa nafsi yako, ulifanya hivyo kwa ajili ya kutekeleza amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), uliacha kustarehe na mwenza wako wa halali, sababu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), basi elewa huyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ndiye Yule Yule ambaye Amekutaka uache kila Alichokukataza  katika maovu ya dhahiri na ya siri, madogo ama makubwa, almuhimu Yeye Amekataza usifanye hilo. Ifahamike dogo ama kubwa ulifanye mafichoni ama hadharani, yote utakabidhiwa wewe mwenyewe na utakiri kuwa ulilifanya utalipwa kwayo, kama kheir ni pepo na kama ni maovu utalipwa moto, tutahadhari.

 

Naomba hapa niweke kisa kilicho simuliwa na Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba kuna jambo dogo tu, watu wawili huko nyuma mmoja ameingia jannah na mwengine ameingia motoni kwa jambo dogo hilo, na ukisha soma utatambua ama kweli hili ni dogo lakini kumbe ni zito mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Naliweka hapa ili tupate mazingatio kwamba uidharau kosa hata dogo vipi, huenda waliona dogo lakini ni kumbwa mbele ya Maalikul-Muluuk, nacho ni hiki:

 

Amesema Twaariq bin Shihaab Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ametusimulia kwamba, kumchinja inzi kumesababisha mtu mmoja aingie jannah na mwengine aingiye motoni, Swahaba wakastaajabu, kuchinja inzi, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema naam. Ilikuwa hivi, kuna watu walikaa njiani ambapo hapiti mtu ila wamtaka achinje kutaswadaq kwa ajili ya sanamu lao walokuwa nalo, asipofanya hivyo humuua, akapita mtu wa kwanza akasema mimi sina kitu niachieni tafadhali,  wakamwambia chinja japo inzi almuhimu utaswadaq, Yule bwana akachinja inzi na kutaswadaq  wakamwachilia huru, ikawa ni sababu ya Yule mchinjaji kuingia motoni. Akapita mtu wa pili, wakamwambia chinja na utaswadaq kwa sanamu letu hili, akasema miye siwezi chinja na kutaswadaq kwa asiye kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwani kuchinja ni ibada na haitakiwi afanyiwe ibada yeyote ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), wakamwambia chinja japo inzi, akasema hata iwe kidogo kiasi gani siwezi chinja kwa asiye kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), wakaamuua ikawa ndiyo sababu ya kuingia jannah Yule bwana. Hivyo watu wawili mmoja aingia motoni na mwengine peponi kwa sababu ya kuchinja inzi.

 

Hadiyth hii ameipokea [Imaam Ahmad], hii ni katika Maraasili Swahaabiy kwani Twaariq hakumsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini kwa mujibu wa Ahlul-Hadiyth, Maraasili Swahaabiy hukubalika. Rejea kisa hiki katika kitabu Sharhu Tawhiyd Majmu’ Al-‘Ulamaa.

 

Hivyo, na sisi tusidharau baya vyovyote litavyokuwa hata kama machoni mwako waliona dogo, lakini kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni kubwa hilo. Allaah naye Anasema:

 

وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

Mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno. [ An-Nuwr: 15]

 

Hivyo Waislamu tujitahidi kila Alichotukataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tusikifanye.

 

Pia yafaa tufahamu yakwamba Yule Yule tulomtumikia Ramadhwaan Ndiye huyo huyo Aliyetuamrisha tujipambe na haiba ya Uislaam, silka, tabia, mwenendo, maadili na tamaduni za Kiislamu. Na Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hufurahi kila Akuonapo umejipamba na sifa hizo, enyi Waislamu na tujipambe vazi la Uislaam Alotuvisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

صِبْغَةَ اللَّـهِ ۖ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ صِبْغَةً ۖ وَنَحْنُ لَهُ عَابِدُونَ ﴿١٣٨﴾

(Dini yetu ni) Dini ya Allaah na dini gani yaweza kuwa bora zaidi kuliko Dini ya Allaah? Na sisi ni wenye kumwabudu Yeye Pekee. [Al-Baqarah: 138]

 

Hivyo Muislamu atakiwa kwa nje na ndani ajipambe na vazi alovishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ukilivuwa ni wewe mwenyewe ndiye wajitesa.

 Aidha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), anasema:

 

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ 

Kwa yakini Tumeumba Jahannam kwa ajili ya wengi katika majini na wana Aadam. [ Al-A’raaf: 179].

 

Hii ni kwa sababu viumbe hawa:-

 

Ø      Tumewapa nyoyo za kuweza fahamu na kuelewa mambo kwamba hili ni batili na hili na sawa, lakini viumbe hawa hawataki kuzingatia kwa kutumia ufahamu tulowapa, kwa sababu ya kutotumia vizuri ufahamu tulowapa na wakafanya wanavotaka wao, tumewaandalia moto, hivyo unawasubiri,

 

Ø      pia viumbe hawa tumewapa macho (uoni), ambayo kwayo wanatakiwa kuona haki na kuifuata na kuiona batili na kuiacha, lakini viumbe hawa hawako tayari kutumia macho yao sawasawa, haki wanaiona hawaifuati, batili wanaiona na wanaijua lakini ndo wanajipamba nayo, hivyo tumewaandalia moto,

Ø      na vilevile tumewapa masikio (usikivu) ili wasikie haki waisimamie na waifuate na waisikie batili waiache, lakini viumbe hwa, hawataki kutumia vizuri kiungo hiki wanajifanya viziwi, hawasikii kuisikia haki wakaifuata, hivyo tumewaandalia moto.  Unawasubiri, muda si mrefu.

 

Ø      Akamalizia kwa kusema kuwa, watu ambao hawataki kuvitumia viungo hivi sawasawa, ni kama wanyama, na wanyama ni bora kuliko wao.”

  

Ee ndugu yangu, unaona makemeo ya Yule Yule tulokimtumika Ramadhwaan, ambaye tulijipamba na silka ya Uislaam, vazi la Uislaam, haiba ya Uislaam, mtu akikuona tu ajua huyu ni Muislamu bila shaka. Tuliyafanya haya ili kupata radhi zake na rehma Zake. Nawausia, na kuwanasihi kama ninavyoinasihi nafsi yangu, tuwe na nyoyo zenye kuzingatia, tuwe na macho yenye kuona na tuwe na masikio yenye kusikia ili tukazipate radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Kama hatukutumia vizuri ogani hizi, ina maana sisi na wanyama bora wanyama, kisia wewe ufananishwe na mnyama yeyote umjuaye awe mdogo ama mkubwa, utaridhika? Sasa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atufananisha bali wanyama ni bora zaidi, kwa sababu tu ya kutotumia vema ogani za utambuzi wa haki na batili. Ee ndugu na tuzinduke, tumtumikie Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Enyi ndugu zangu, tuelewe, kila tufanyacho, tusemacho, tunong’onacho kinarikodiwa na tutajaoneshwa, na kuulizwa kwacho, hivyo basi tuishi kama tulivyoishi Ramadhwaan ili tupate radhi za muumbaji wetu.

 

Tukumbuke, kwamba kama hatutaki kuswali, ipo siku tutaswaliwa Swalah ambayo haina rukuu wala sijdah, kama hatutaki kuvaa mavazi ya Uislamu kama ilivyoamrishwa, tukumbuke ipo siku utavishwa nguo ambazo zitafunika mwili mzima lakini hazina mikono wala fasheni yoyote na wala hazivutii.

 

Tujipinde katika ibaadat kama vile Swalah na zingine, na pia dada zetu mjiheshimu kwa kuvaa vile alivyofundisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), usisubiri sanda ije kukufunika hali ya kuwa ulikuwa huipendi.

 

Zaidi ya yote, tujipambe na haiba, silka, tamaduni na mwenendo wa Kiislamu kama tulivyokuwa tumejipamba katika mwezi wa Ramadhwaan, ili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa rehma na fadhila Zake Atukirimu jannah Yake yenye neema.

 

 

Wabillaahi At-Tawfiyq

 

 

Share