Maana Ya Swawm Na Historia Yake

 

Maana Ya Swawm Na Historia Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

Maana ya kufunga (Swawm) ni kujizuilia. Neno Swawm kwa maana ya kujizuilia linaweza kutumika katika kujizuia kufanya jambo lolote la kawaida mtu alilozoea kulifanya. Katika Qur-aan tunafahamishwa kuwa Bibi Maryam baada ya kumzaa Nabiy ‘Iysaa (‘Alayhis- salaam) alijizuia (alifunga) ili asiseme na mtu neno lolote juu ya mtoto wake.

 

 ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا ﴿٢٦﴾

Na utakapokutana na mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri ya swawm kwa Ar-Rahmaan hivyo leo sitomsemesha mtu yeyote. [Maryam: 26].

 

Katika Uislaam kufunga (Swawm) ni kujizuilia kula, kunywa, kuvuta sigara, kuingiza kitu chochote katika matundu mengine mawili kama vile pua na masikio, kujizuia na kujamii, kujitoa manii kwa makusudi au kwa matamanio na kujizuia kujitapisha kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kwa kipindi cha kati ya Al-fajri ya kweli mpaka kuingia magharibi. Hii ndio maana ya nje ya Swawm katika Uislaam.

  

Kufunga katika Uislaam kuna maana ya ndani zaidi, ambayo kama haikufikiwa, kuzuilia kufanya vitendo hivyo vilivyoelezwa hakutakuwa na maana yoyote kwa mfungaji.

 

Kufunga kwa maana ya ndani ni pamoja kujizuilia kutenda maovu yote yaliyokatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Ili Swawm ya mfungaji iwe na maana na yenye kufikia lengo, hana budi kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake cha mwili - macho, ulimi, masikio, mikono na miguu- pamoja na fikra na hisia zake na matendo aliyokataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Funga ya macho ni kujizuilia na kuangalia aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa); Funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama vile kusengenya, kusema uwongo, kugombana na kadhalika, funga ya masikio ni kujizuia kufanya yale yote aliyoyaharamisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa); funga ya miguu ni kujizuilia na kuendea yale yote aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) funga ya fikra na hisia ni kujizuia na fikra na dhana mbaya ambazo zinampelekea kuvunja amri na makatazo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Ni katika maana hii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)anasema katika Hadiyth zifuatazo:

 

Abu Hurayrah amesimulia kuwa Nabiy wa Allaah amesema:

 

“Yule ambaye haachi kusema uwongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allaah hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake (yaani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hana haja na funga yake.” [Al-Bukhaariy].

   

Abu Hurayrah ameeleza kuwa Nabiy wa Allaah amesema:

 

“Ni wangapi wanaofunga lakini hawana funga ila kukaa na kiu tu ni wangapi wanao swali usiku ambao hawana Swalah ila huambulia kupoteza usingizi tu.” [Ad-Daarimiy].

 

Hadiyth hizi zinatuthibitishia kuwa ufungaji usioambatana na kujizuia na mambo maovu na machafu, haumpatii mfungaji faida yoyote.

 

Umuhimu Wa Funga Katika Uislaam

 

Funga ya Ramadhwaan ni miongoni mwa nguzo za Uislaam na ni faradhi kwa Waislamu kama inavyobainika katika aya ifuatayo:

 

  يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183]

 

Kama ilivyo katika nguzo nyingine za Uislaam, mtu atakapoivunja makusudi nguzo hii hatabakia kuwa Muislamu japo atajiita Muislamu na watu wakaendelea kumwita hivyo. Katika Hadiyth iliyopokelewa na Ibn ‘Abbaas, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Kuna viungo vitatu vinavyomuunganisha Muislamu na dini ya Uislaam na yeyote yule atakayevunja kiungo kimoja katika hivi atakuwa amekana Uislamu na kuuawa kwani ni halali. Viungo hivi ni: Kushuhudia kuwa hapana Mola ila Allaah, Kusimamisha Swalah tano na kufunga mwezi wa Ramadhwaan.”

 

Katika Hadiyth nyingine Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Yeyote yule atakaye acha makusudi kufunga siku moja ya mwezi wa Ramadhaan, hawezi kuifidia siku hiyo hata akifunga kila siku katika umri wake wote (uliobakia).” [Abu Daawuud]

 

Funga ni ibada maalum iliyo muhimu sana katika kumuandaa mja kuwa mcha Mungu kwa kule kukataa kwake matamanio ya kimwili. Hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa ukaribu wake ameahidi malipo makubwa kwa wenye kutekeleza ibada hii ili iwe motisha kwao ya kuwawezesha kutekeleza ibada hii kwa hima kubwa na kwa ukamilifu unaotakikana kama tunavyojifunza katika Hadiyth zifuatazo:

 

Abu Hurayrah amesimulia kuwa Nabiy wa Allaah amesema:

 

“Mwenye kufunga Ramadhwaan akiwa na imani na akawa na matumaini ya kupata malipo kutoka kwa Allaah dhambi zake zote zilizopita husamehewa, Na mwenye kusimama kwa Swalah (tarawehe) katika mwezi wa Ramadhwaan akiwa na imani na matumaini ya kupata malipo (kutoka kwa Allaah), dhambi zake zote zilizopita zitasamehewa. Na yule atakayesimama (kwa Swalah) katika usiku uliobarikiwa (Lailatul-Qadri) akiwa na imani na matumaini ya kupata malipo kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) dhambi zake zote zilizotangulia zitasamehewa.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Pia Abu Hurayrah ameeleza kuwa Rasuli wa Allaah amesema:

 

“Kila amali njema anayoifanya mwanaadamu italipwa mara kumi (Al-Qur-aan 6:160) mpaka kufikia mara mia saba (Al-Qur-aan 2:261). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) amesema: Ila kufunga kwa sababu funga ni kwa ajili Yangu, na ni mimi mwenyewe nitakayeilipa. Mwenye kufunga anakata matamanio yake ya kimwili na anaacha chakula kwa ajili yangu. Kwa mwenye kufunga kuna furaha mbili, furaha moja anaipata wakati wa kufuturu na nyingine wakati atakapokutana na Mola wake. Na hakika harufu ya mdomo wa mwenye kufunga ni bora mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuliko harufu ya miski. Na funga ni ngao. Kwa hiyo atakayefunga miongoni mwenu hataongea maneno ya upuuzi wala hatagombana. Kama itatokea achokozwe na yeyote, au mtu atakakupigana naye, na aseme: Nimefunga.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Historia Ya Kufunga

 

Funga, kama ilivyo katika ibada nyingine kama tulivyoona katika kusimamisha Swalah na kutoa zakat, imetekelezwa na Rusuli wote pamoja na umma zao. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ametukumbusha hili wakati alipotupa amri ya kutekeleza ibada hii maalum, kama tunavyorejea katika Qur-aan:

 

  يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183]

 

Katika historia tunajifunza kuwa, kila Nabiy alipoondoka, baada ya kipindi kupita, watu waliacha mafundisho yake na kuingia katika ushirikina. Lakini bado tunakuta funga, japo si katika madhumuni na asili yake iliyoachwa na Rusuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), imebakia katika jamii za kishirikina kwa kipindi chote cha historia. Hebu tuangalie mifano michache ya dini za ushirikina ambapo funga, kwa maana ya kushinda na njaa na kiu, imekuwa miongoni mwa ibada muhimu za dini hizo.

 

Jamii Ya Nabiy Ibraahiym

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) aliinuliwa katika jamii ya washirikina. Walikuwa wakiabudu jua, mwezi, nyota na masanamu chungu nzima waliyoyachonga wenyewe. Pamoja na ushirikina wao huo walikuwa wakifunga siku 30 mfululizo katika kila mwaka kwa heshima ya mwezi.

 

Wahindu (Hinduism)

 

Dini ya Kihindu ni miongoni mwa dini za kishirikina katika bara la India. Katika dini hii funga, ni kitendo kilichosisitizwa sana japo si lazima, katika siku maalum kama vile kupatwa kwa jua, kumbumbuku ya kuzaliwa mwanzilishi wa dini yao na kadhalika. Funga kwao ni kujizulia na kula na kunywa kuanzia alfajiri mpaka saa tisa mchana.

 

Mayahudi (Judaism)

 

Dini ya Kiyahudi ni dini waliyoibuni Mayahudi baada ya Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam) ambapo walimfanya Uzairi mwana wa Allaah. Pamoja na hivyo wachaji wa Kiyahudi walikuwa wakifunga Alhamisi na Jumatatu kama kumbukumbu ya kwenda na kurudi kwa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam) katika safari yake ya Sinai kwenda kuchukua Taurati. Kutokana na kumbukumbu ya historia, Nabiy Muwsaa alikwenda kwenye mlima Sinai siku ya Alhamisi na kurejea siku ya Jumatatu baada ya siku arobaini kupita.

 

Pia Mayahudi hufunga kwa saa 24 katika kila mwezi 10 Muharamu, kwa kumbukumbu ya siku Wanaisraili (Mayahudi) walipookolewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutokana na udhalimu wa Fir’awn. Siku hii ambayo hata Waislamu wamesuniwa kufunga huitwa siku ya ‘Ashuuraa.

 

Pamoja na funga hizi, pia Mayahudi wana tabia ya kufunga mara kwa mara kulingana na haja. Kwa mfano mtu anaweza kuamua kufunga siku kadhaa kama kumbukumbu ya matukio fulani katika maisha yake, au anaweza kufunga funga kama kitubio cha madhambi yake, au anaweza kufunga wakati akiwa na matatizo ili kupata huruma ya Allaah.

 

Ukiacha siku ya ‘Ashuuraa ambapo funga huchukua saa 24, funga za Mayahudi huanza alfajiri na huishia pale inapojitokeza nyota ya kwanza usiku.

 

Wakristo

 

Dini ya Ukristo imebuniwa baada ya Nabiy ‘Iysaa (‘Alayhis-salaam). Katika dini hii Nabiy ‘Iysaa (‘Alayhis-salaam) amefanywa mwana wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kwamba yeye ndiye mkombozi wa Wakristo. Pamoja na hivyo, Wakristo wanakiri kuwa kufunga ni kitendo cha uchaji - katika dini yao. Wakristo wa mwanzo walikuwa wakifunga siku 40 mfululizo kasoro siku za Jumapili kama kumbukumbu ya siku zile alizofunga Yesu (Nabiy ‘Iysaa ‘Alayhis-salaam) kama inavyobainishwa katika Biblia.

 

Historia inatuonyesha vile vile kuwa funga hizi za Washirikina zimetofautiana sana katika mfumo na funga ya Kiislamu aliyoiamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Ambapo Waislamu wakifunga hujizuia kula, kunywa na kujamii mchana kutwa kuanzia alfajiri mpaka kuchwa kwa jua, funga za washirikina zilichukua mifumo mbalimbali. Wengine walijizuilia kula na kunywa tu lakini waliendelea kujamii, wengine walijizulia kunywa na kula kuanzia alfajiri mpaka saa 9 alasiri, wengine walijizulia kula aina fulani tu ya chakula kama vile nyama, wengine walijizulia kwa kunywa tu maji yaliyochanganywa na chumvi au maji ya ndimu, na kadhalika.

 

Share