Hana Muda Wa Kujipamba Mbele Ya Mume Akijipamba Wakati Mwengine Inafaa?

 

Hana Muda Wa Kujipamba Mbele Ya Mume Akijipamba Wakati Mwengine Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalamu alaykum warahmatullah wabarakatuh.

 

Ningependa kumshukuru Allaah kwa kuwapa nguvu na mafanikio katika kuiendesha Alhidaaya. Mimi ni msomaji mkubwa na nimefaidika sana na website hii. Allah aienzi Alhidaaya.

 

Ndugu zangu waislam nina swali kuhusu kujipamba kwa ajili ya mume. Mimi ni mwanamke ninaye enda kazini na nina watoto ambao nikirudi jioni ni lazima kuwahudumia. Nikiingia nyumbani nashughulika na kazi. Mume wangu yuko nje. Akija ni saa tatu, nimechoka hata wakati mwengine huwa nimelala. Mwisho wa wiki nikiwa nyumbani yeye hutoka, hata saa nyengine humwambia akae ili nipate kujipamba lakini hakai. Jee, nikijipamba na yeye hayupo ni sawa? Na je nisipojipamba itakuwaje? Naomba ufafanuzi ndugu zangu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ni kuwa mume anafaa ajipambe kwa ajili ya mkewe na vile vile mke kwa ajili ya mumewe. Hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma).

 

 

Kulingana na swali lako japokuwa ni la upande mmoja inaonyesha kuna tatizo baina yako na mumeo. Itabidi mwanzo mkae na kulizungumzia swali hilo kwa kina na uwazi. Hujasema ikiwa mumeo anafanya kazi hadi saa hizo, au ana mizunguko yake tu.

 

 

Wanandoa na haswa ikiwa mke pia anafanya kazi wasaidiane ili kuweka hali kuwa nzuri katika mazingira ya nyumbani. Ndio Allaah Aliyetukuka Akatuambia:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ

Na shirikianeni katika wema na taqwa,...[Al-Maaidah 5: 2].

 

 

Haifai kabisa kwa mume kuchelewa kuja nyumbani pasi na udhuru wa aina yoyote, na hata ikiwa ni mwisho wa wiki asiwe ni mwenye kutoka nje ilhali mke atamtaka abakie naye.

 

 

Ama kujipamba kwako kwa Niyah ya kumpambia mume ni ‘Ibaadah, ikiwa atakuwepo nyumbani au hatokuwepo. Wewe unahitajika kufanya hivyo ili upate thawabu kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na huenda pia kufanya hivyo kukamvutia mumeo akawa anarudi mapema na kuwa karibu zaidi nawe.

 

 

Itabidi mkae kitako kama wanandoa mjadili mahusiano yenu ya kinyumba na mrekebishe kasoro zozote zile. Ikiwa mtachelewa kuyazungumzia hayo machache, bai yanaweza kulimbikizana matatizo na kukazuka matatizo makubwa zaidi ambayo yanaweza kukosa suluhisho.

 

 

In shaa Allaah tunamuomba Allaah Awafanyie wepesi na Awaweke karibu zaidi katika ndoa yenu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share