Uadilifu Wa Maswahaba Na Utatanishi Wa Hadiyth Ya Hodhi

 

Uadilifu Wa Maswahaba Na Utatanishi Wa Hadiyth Ya Hodhi

 

Alhidaaya.com

 

Imekusanywa Na Kutarjumiwa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’ay (Rahimahu-Allaah)

Na Kupitiwa Na Abu 'Abdillaah

 

 

 

Yaliyomo:

 

Utangulizi 

 

 

Hadiyth Ya Hodhi 

 

 

Daraja Yao..

 

 

Sifa Zao Ndani Ya Qur-aan

 

 

Sifa Zao Ndani Ya Sunnah.

 

 

Katika Kauli Za ‘Ulamaa.

 

 

Wanafiki .

 

Wenye Shaka Na Iymaan Dhaifu.

 

 

Nani Atakayeondolewa? 11

 

 

Alikuwa Akiwajua. 15

 

 

Hitimisho. 18

 

 

Utangulizi:

 

Zipo baadhi ya Hadiyth zenye utatanishi au zenye kubeba maana zaidi ya moja, ambazo wakristo katika tovuti zao huzitumia kwa kuzifasiri Hadiyth hizo kwa maslahi yao, au kwa maana wanayoitaka wao, kinyume na maana yake ya kweli, kwa ajili ya kuupiga vita Uislamu.

 

 

Kinachoskitisha zaidi ni kuwa wapo baadhi ya wanaodai ni Waislamu ambao kwa kutaka maslahi yao, bila kujali athari wanayoiacha, utawakuta wakipoteza wakati wao mkubwa wakifanya utafiti na kunukuu Hadiyth za aina hizo huku wakitaja baadhi ya makosa ya kibin-Aadam yaliyowahi kutendwa na baadhi ya Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum), kisha wanayakuza makosa hayo na kuyafanya kuwa ni dalili ya ubaya wa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Yareti kama wakati wao wangeliupoteza katika kufanya utafiti juu ya maadui wa Allaah ('Azza wa Jalla) kama vile Abu Jahal au mnafiki Abdullahi bin Saluwl au Fir-‘auni au Haaman au Abu Lu'ulua al Majusiy, aliyemuuwa Khalifa wa pili wa Waislamu ‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu). Bali kinyume na hivyo, utawaona wanaunyamazia uadui wao watu hao, juu ya kuwa ukafiri wao umethibiti ndani ya Qur-aan tukufu na ndani ya mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na badala yake wanaziunguza juhudi zao katika kujaribu kuwapaka matope Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwa kufanya hivyo wanawapa makafiri silaha kali pamoja na ushahidi wanaoutaka katika kuupiga vita Uislamu na kuwapiga vita waliotuletea Dini hii, kwa sababu kwa kuwatuhumu Maswahaba bila ya uhakika wala ushahidi ulio wazi, ni kuutuhumu Uislamu waliotuletea Maswahaba hao (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) baada ya kuupokea kutoka kwa sahibu yao Muhammad Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hadiyth Ya Hodhi:

 

Miongoni mwa Hadiyth wanayoitumia katika ubabaishaji wao huo ni ile Hadiyth maarufu ya Hodhi, na namna Malaika watakavyowarudisha watu watakaotaka kunywa ndani ya hodhi hilo la Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakidai kuwa Hadiyth hiyo inawakusudia Maswahaba hawa (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) sahibu zake Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na marafiki zake na wenzake alioanza nao tokea siku ile ya mwanzo ya kuwalingania watu katika Dini hii tukufu.

 

 

Imepokelewa katika Hadiyth hiyo kuwa Siku ya Qiyaamah, wakati Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakapokuwa anawanywisha watu maji kutoka katika hodhi lake, watakuja Malaika na kuwaondoa makundi kati yao, na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakaposema: "Hawa ni katika Maswahaba wangu." Malaika watajibu: "Je Unajua waliyoyazua baada yako?”

 

Na katika riwaayah nyingine, Malaika watasema: "Walirtaddi hawa wakarudi nyuma."

 

 

Anasema Ibni ‘Abdil Barr: "Maana hasa ya Hadiyth hizi ni kuwa kila mwenye kuzusha mambo katika Dini, atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa penye hodhi ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)."

 

 

Tukiendelea na kuichambua Shub-ha hii inayowakanganya baadhi ya watu wakadhani kuwa watakaoondolewa penye hodhi ni hawa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliosimama naye tokea siku za mwanzo kisha wakaendelea kusimama naye katika shida zake zote na vita vyote dhidi ya makafiri; vita vya Badr, vita vya Bani Qaynuqaa, vita vya Uhud, vita Khandaq, Fat-hu Makkah, Hunayn na vita mbali mbali. Hawa ambao baada ya kufariki kwa sahibu yao Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliendelea kuisimamia Dini hii kidete na kuipigania kwa hali zao na mali zao mpaka ikaenea ulimwengu mzima.

 

 

Daraja Yao:

 

Daraja ya Maswahaba na heshima yao katika Dini ni jambo lisilokubali kujadiliwa na Muislamu yeyote mkweli mwenye kupenda haki, kwa sababu hawa ndio ambao Allaah ('Azza wa Jalla)  Aliwahusisha kwa kuwafanya kuwa sahibu zake Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakamsadiki na kumfuata na kumnusuru na wakaifuata nuru aliyokuja nayo, na wakafanya kila juhudi kwa kujitolea roho zao na mali zao kwa ajili ya kuipigania Dini hii tukufu mpaka ilipokamilika.

 

 

Hawa ndio wale waliosifiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  walipoambiwa kuwa wao ni umma bora kupita zote zilizoletwa kwa ajili ya watu. Na Allaah ('Azza wa Jalla)  Akaridhika nao.

 

 

Maswahaba ni waaminifu wa umma huu walioibeba Shariy’ah na kuieneza ulimwenguni kote mpaka ikatufikia sisi hivi sasa. Hii Qur-aan tuliyo nayo na haya mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yametufikia kupitia kwao (Radhwiya-Allaahu ‘anhum).

 

 

Kwa hivyo kitendo cha kuwatilia shaka Maswahaba hawa watukufu katika uadilifu wao ni katika kuipiga vita Dini na kuwafanya watu wasiamini masdari za Dini tulizopokea kutoka kwa Maswahaba hao watukufu (Radhwiya-Allaahu ‘anhum). Kwa sababu Qur-aan tukufu na mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yote tumeyapata kupitia kwao.

 

 

Ndiyo maana ‘Ulamaa wa Kiislamu wanatutaka tuwe na msimamo imara dhidi ya kila mwenye kuwatuhumu Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Inasikitisha kuona kuwa wapo miongoni mwa wanaodai kuwa ni Waislamu wenye kuwatuhumu baadhi ya Maswahaba, na wanafanya hivyo makusudi kwa ajili ya kukifikia kile wanachokitaka tu, na wakazitumia hizi Hadiyth za hodhi katika kujaribu kuwapaka matope Maswahaba hawa watukufu (Radhwiya-Allaahu ‘anhum).

 

 

Katika kujaribu kuharibu sifa za Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum), wakazitumia Hadiyth mfano wa hii inayosema: "Wakati mimi nimesimama, litakuja kundi, nitakapowajua, atatoka mtu kutoka kwangu na kusema: 'Twendeni', Nitasema: 'Wapi?' Atasema: 'Motoni wallahi.' Nitasema: 'Wana makosa gani?' Atasema: 'Hawa wamertaddi na kurudi nyuma baada yako." [Al-Bukhaariy  na wengineo]

 

 

 

Sifa Zao Ndani Ya Qur-aan:

 

‘Ulamaa wanasema:

Wa kwanza kutoa hukmu Yake kuwa Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum), ni watu waadilifu ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kama ilivyoandikwa ndani ya Qur-aan Tukufu na kama ilivyokuja kwa njia Mutawaatirah katika Sunnah ya Nabiy (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na miongoni mwa hukmu hizo ni kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliposema:

 

 

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا﴿٢٩﴾

Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Rasuli wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri; wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huo ni mfano wao katika Tawraat, na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake, liwapendezeshe wakulima, ili liwatie ghaidhi makafiri. Allaah Amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema miongoni mwao maghfirah na ujira adhimu. [Al-Fat-h: 29]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah: 100]

 

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَـٰكِنِ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ جَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ ۚ وَأُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْخَيْرَاتُ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٨٨﴾

Lakini Rasuli na wale walioamini pamoja naye, walifanya jihaad kwa mali zao na nafsi zao. Na hao watapata khayr nyingi. Na hao ndio wenye kufaulu. [At-Tawbah: 88]

 

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا﴿١٨﴾

Kwa yakini Allaah Amewawia radhi Waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chini ya mti, (Allaah) Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao; basi Akawateremshia utulivu, na Akawalipa ushindi wa karibu. [Al-Fat-h: 18]

 

 

 

 

Sifa Zao Ndani Ya Sunnah:

 

Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Kheri ya watu ni wa karne yangu kisha wanaowafuata kisha wanaowafuata." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliposema:

"Msiwatukane Swahaba wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya Allaah kugawa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao lao." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na akasema:

"Allaah Allaah! (nakuusieni) juu ya Swahaba wangu. Msiwageuze kuwa malengo yenu baada ya kuondoka kwangu. Kwani mwenye kuwapenda basi kwa kunipenda mimi (ndiyo) amewapenda, na mwenye kuwachukia basi kwa kunichukia mimi (ndiyo) amewachukia. Na mwenye kuwaudhi ameniudhi (na) mimi, na mwenye kuniudhi mimi amemuudhi Allaah, na mwenye kumuudhi Allaah, anakaribia Kumnyakua." [At-Tirmidhiy]

 

 

Zipo Hadiyth nyingi za namna hii zenye kuwasifia na kueleza juu ya fadhila zao mbali mbali na mitihani waliyopambana nayo, na kututaka wafuasi wa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaheshimu na kuwakirimu na kutowaudhi wala kuwageuza kuwa ni malengo yetu tunayoyatumia kila tunapotaka kuipitisha batil yetu. Na nasaha zote hizi zinatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kwa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

 

Katika Kauli Za ‘Ulamaa:

 

Amesema Imaam Ibn Najjaar:

"Aliyesifiwa namna hii na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Itakuwaje tena asiwe muadilifu. Ikiwa mbele ya mahakama wanatosha mashahidi wawili tu kuthibitisha uadilifu wa mtu, itakuwaje basi ikiwa ushahidi unatoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi (Subhaanahu wa Ta’aalaa)." [Sharhi ya Kawkab Al-Muniyr (2/475)]

 

 

Anasema Al-Khatwiyb Al-Baghdaadiy:

"Usafi wa Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) na uadilifu wao hauna lazma ya kusifiwa na wana Aadam baada ya kusifiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyeangalia ndani ya nafsi zao Akatujulisha juu ya ukweli wao.

Na hata kama Allaah ('Azza wa Jalla)  Asingetujulisha juu ya sifa zao na kuridhika Kwake nao, basi kule kupigana kwao Jihaad kwa mali zao na nafsi zao, wamewaua baba zao na watoto wao waliopigana upande wa makafiri, haya yanatokana na yakini waliyokuwa nayo ndani ya nyoyo zao juu ya nusra ya Allaah iliyowajia." [Al-Kifaayah fiy ‘Ilm An-Nihaayah: 48-49]

 

 

Kwa hivyo kuzichukulia zile Hadiyth za hodhi kuwa waliokusudiwa ni hawa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliomsadiki na kumuamini, wakamsaidia na kumnusuru, kunakuwa ni kuzikataa aya zote na riwaya zote zilizo sahihi zenye kutubainishia fadhila zao na heshima yao mbele ya Allaah ('Azza wa Jalla) na mbele ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kuwatuhumu Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) ni mfano wa kuukataa ushahidi wa Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa sababu itakuwaje Allaah ('Azza wa Jalla)  Atujulishe juu ya watu Alioridhika nao na kutujulisha juu ya fadhila zao na kwamba Atawaingiza katika Jannah Yake, kisha Asijuwe kuwa watu hao siku moja watakuja kurtaddi na kubadilisha na kuzua nk.

 

 

Na huko pia ni kuzikanusha kauli za Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyetujulisha juu ya kuridhika na Swahibu zake na kuwabashiria Jannah aliposema:

"Abu Bakr (yuko) Jannah (Peponi), na ‘Umar (yuko) Jannah, na ‘Uthmaan (yuko) Jannah na ‘Aliy (yuko) Jannah na Twalhah (yuko) Jannah na Az-Zubayr (yuko) Jannah na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (yuko) Jannah na Sa’ad (yuko) Jannah na Sa’iyd (yuko) Jannah na Abu ‘Ubaydah (yuko) Jannah " [Muslim na At-Tirmidhiy na Imaam Ahmad na wengine]

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki dunia akiwa ameridhika nao.

 

Na akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

"Haingii Motoni aliyeshiriki katika vita vya Badr." [Imam Ahmad na At-Twabaraaniy na wengine]

 

 

 

Hivyo kweli inawezekana maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yapingane yenyewe kwa yenyewe? Leo amuambie kuwa wewe utaingia Jannah (Peponi), na kesho amkute katika watakaorudishwa mbele ya hodhi?

 

 

Huku ni kukanusha wazi wazi maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tutakwenda wapi na ile riwaayah ya Attwabaraniy kutoka kwa Abu Dar'daa (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa alimuambia Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"Ee Rasuli wa Allaah! Muombe Allaah anijaalie nisiwe katika hao. Akasema: "Wewe si katika hao."

 

 

Je, inawezekana kweli Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asijuwe hali ya Maswahaba wengine akaweza kujua hali ya Abu Dar'daa alipomjulisha kuwa hatokuwa miongoni mwa watakao ondolewa penye hodhi?

 

 

 

Wanafiki:

 

Waliowahi kuonana na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawakuwa watu wa aina moja. Wapo miongoni mwao waliokuwa wanafiki waliokuwa wakijidhihirisha kinyume na walivyo, juu ya kuwa walikuwa wakishiriki vitani.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ﴿١﴾

Watakapokujia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wanafiki wakisema: Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Rasuli wa Allaah. Na Allaah Anajua kuwa wewe ni Rasuli Wake, na Allaah Anashuhudia kuwa hakika wanafiki ni waongo. [Al-Munaafiquwn: 1]

 

 

 

Na wanapokuwa vitani huwa wakisema:

 

لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ ۚ وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿٨﴾

Tutakaporudi Madiynah, mwenye hadhi zaidi bila shaka atamfukuza humo aliye dhalili. Na ilhali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui. [Al-Munaafiquwn: 8]

 

 

 

Wenye Shaka Na Iymaan Dhaifu:

 

 

Walikuwepo pia waliokuwa wakitia shaka, na pia walikuwepo wenye Iymaan dhaifu miongoni mwa mabedui ambao wengi wao walirtaddi baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki dunia.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَمِمَّنْ حَوْلَكُم مِّنَ الْأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ ۖ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ ۖ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لَا تَعْلَمُهُمْ ۖ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ ۚ سَنُعَذِّبُهُم مَّرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَىٰ عَذَابٍ عَظِيمٍ﴿١٠١﴾

Na katika Mabedui wanaokuzungukeni wako wanafiki. Na katika watu wa Madiynah (pia) walibobea katika unafiki. Huwajui (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Sisi Tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili; kisha watarudishwa katika adhabu kuu. [At-Tawbah: 102]

 

 

Hadiyth zimeeleza wazi wazi wasfu na sababu za watu watakoondolewa penye hodhi, na wasfu huo haukubaliani na wasfu wa Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) waliolelewa na kufundishwa na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mpaka alipofariki dunia alikuwa radhi nao.

 

Na hii ni dalili kuwa Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) hawana uhusiano wowote na Hadiyth hizi, kwani hapana Swahaba hata mmoja aliyertaddi wala aliyezusha.

 

 

‘Umar na ‘Uthmaan (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa) wanaowatuhumiwa kuwa walizusha, wao walichofanya ni kuhuisha Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wala hawajazusha jambo jipya katika Dini. Na hao tulisema kwamba tumeamrishwa na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufuata mwenendo wao.

Anasema Imaam Al-Khutwaabiy: "Hapana hata Swahaba mmoja aliyertaddi, bali waliortaddi ni makabila ya kibedui wasiowahi kuipigania Dini, na kwa ajili hiyo haipasi kuwatuhumu Maswahaba wale maarufu." [Fat-hul-Baariy 00/385]

 

 

Anasema Imaam Al-Baghdaadiy: “Wamekubaliana ‘Ulamaa wote wa Kisunni ‘Ijmaa’ kuwa waliortaddi baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki dunia walikuwa ni watu wa kabila la Bani Kindah na Haniyfah na Fizaarah na Bani Asad na Bani Bakar bin Waail. Hawa hawakuwa miongoni mwa watu wa Madiynah wala watu wa Makkah kabla ya kutekwa mji wa Makkah. Na ki-shariy’ah wanaoitwa Muhaajiriyn ni wale tu waliohaajir kwa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya Fat-h Makkah." [Al-Farqu baynal Firaq]

 

 

Nani Atakayeondolewa?:

 

 

Wamekhitalifiana ‘Ulamaa juu ya nani atakayeondolewa penye hodhi la Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya wote kukubaliana kuwa waliokusudiwa si Maswahaba hawa tunaowajua sisi.

 

 

Kwanza: Amesema Imaam An-Nawawiy (Rahimahu-Allaah) katika kuisherehesha Hadiyth hii ambayo ndani yake imo kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: "Unajua namna waliyozusha baada yako?" 'Waliokusudiwa ni wanafiki waliortaddi na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakapowaita ataambiwa: "Hawa sio uliahidiwa, kwani hawa walibadilisha." [Sharh ya Muslim 3/136 -137]

 

 

Pili: Rai nyingine inasema kuwa watu hao ni wale waliokuwa Waislamu wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kisha wakartaddi baada ya kufariki kwake. Na atakapowaita, ataambiwa kuwa walirtaddi baada yake.

 

 

Tatu: Rai ya tatu ni kuwa; hawa ni watu waliotenda maasi makubwa na Bida'h wakafariki kabla ya kutubia, juu ya kuwa walikuwa Waislamu.

 

Kauli kama hizi pia alizitaja Al-Qurtuby katika Al-Mufhim 1/503.

 

Ikajulikana kuwa Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) hawamo katika wasfu huu. Na kama mtu atarudi kusoma wasfu wa nani Swahaba uliotajwa na ‘Ulamaa mbali mbali atauona uhakika wa hayo.

‘Ulamaa wanasema kuwa Swahaba ni: "Mtu aliyemuona Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa Muislamu na akafariki dunia akiwa katika hali hiyo."

 

 

Wasfu huu unawatoa wanafiki na waliortaddi, kwani wao si Maswahaba aslan. Watakuwaje Maswahaba wakati Maswahaba ni maadui wa waliortaddi na maadui wa wanafiki. Waliwapiga vita mpaka Allaah ('Azza wa Jalla)  Alipowapa ushindi juu yao. Na haya yalitokea baada ya kufariki dunia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakati waliportaddi makabila mengi ya Kiarabu.

 

 

Na pia kuhusu kitendo cha Bida'h, ambayo ni sababu mojawapo ya kuondoshwa hodhini. Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum) walikuwa msitari wa mbele kupiga vita kila aina ya Bida'h, bali matendo ya Bida'h hayajaenea isipokuwa baada ya kumalizika zama zao Maswahaba hawa (Radhwiya-Allaahu ‘anhum), na dalili ya maneno haya ni kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: "Nyota ndizo zinazolinda mbingu, zitakapoondoka, mbingu zitajiwa na kile kilichoahidiwa, na mimi ni mlinzi wa Swahibu zangu, nitakapo ondoka watakuja Swahibu zangu. Na Swahibu zangu ni walinzi wa ummah wangu, watakapoondoka, umati wangu utajiwa na kile walichoahidiwa." [Muslim, Imaam Ahmad, At-Tirmidhiy na wengine].

 

 

 

Anasema Imaam An-Nawawiy kuhusu kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Na Swahibu zangu ni walinzi wa ummah wangu, watakapoondoka, ummah wangu watajiwa na kile walichoahidiwa.” Maana yake ni kuwa baada ya kuondoka Maswahaba watakuja wazushi na fitan ..."

 

 

Misimamo imara kama hii ya Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum), ambao baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki dunia, walipopambana na maadui, na wakati huo huo walipambana na waliortaddi, na wakati huo huo  walifungua nchi nyingi na nyoyo nyingi, yote haya ni dalili kuwa wao ndio hasa wanaostahiki kunywa maji ndani ya hodhi.

 

 

Inawezekana pia kuwa watakoondolewa penye hodhi ni watu wenye wasfu ule wa kurtaddi, kwa sababu katika Hadiyth Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Nitaambiwa kuwa hawa walirtaddi baada yako."

 

 

Ikiwa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa sababu ya kuondoshwa penye hodhi ni kwa kurtaddi na kufanya matendo ya Bida'h, kwa hivyo bila shaka yoyote watakaoondoshwa hapo ni wale waliortaddi na waliozusha, na hapana hata mmoja kati ya Maswahaba hawa aliyenukuliwa kuwa alirtaddi.

 

 

Anasema Imaam Ibni ‘Abdil-Barr: "Yeyote atakayezusha (atakayeingiza Bida'h yake) katika Dini, atakuwa miongoni mwa watakao ondoshwa penye hodhi."

 

 

Amesema Al-Qurtuby katika At-Tadhkirah 1/348: "‘Ulamaa wetu wote wamesema kuwa; kila aliyertaddi katika Dini au aliyezusha Bida'h yake, kile asichokitolea amri Yake Allaah ('Azza wa Jalla) huyo atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa penye hodhi."

 

 

Alikuwa Akiwajua:

 

Kule kusema kuwa alikuwa akiwajua, si lazima kumaanishe kuwa aliwahi kuwaona, bali aliwajua kwa alama maalum kama ilivyokuja katika Swahiyh Muslim kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Watarudishwa katika ummah wangu ninaowajua kama mtu anavyowajua ngamia wake." Wakamuuliza: "Utatujua?" Akasema: "Ndiyo, mtakuwa na alama hawana alama hizo wengine isipokuwa nyinyi. Mtarudishwa kutoka kwangu mkiwa weupe hamna madoa kwa athari ya Wudhuu, na wengine miongoni mwenu watazuiliwa hawatoweza kunifikia. Nitasema: "Ee Rabb wangu! Hawa ni Swahibu zangu." Atanijibu Malaika: "Unajua waliyozua baada yako?"

 

 

Kwa hivyo pale Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:"Miongoni mwenu", alikusudia 'miongoni mwa ummah wake', na maana yake ni kuwa; watafufuliwa ummah wake wote kwa alama za Wudhuu, na maana yake ni kuwa watafufuliwa pamoja na Waislamu wenzao, na Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atawajua kutokana na athari yao ya Wudhuu.

 

 

Nne: Riwaayah hizi zimepokelewa kutoka vitabu Swahiyh kutoka kwa hao Maswahaba (Radhwiya-Allaahu ‘anhum), akiwemo ‘Umar na Abuu Hurayrah na ‘Aaishah na Ummu Salamah na Hudhayfah na Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy na Ibni Mas’uwd na Anas na Sahal bin Sa’ad na Ibn ‘Abbaas na Mu'aawiyah na wengine (Radhwiya-Allaahu ‘anhum).

 

 

Sasa ikiwa hawa ndio waliokusudiwa kuwa ndio watakaofukuzwa penye hodhi, inaingia akili kweli waje kutuhadithia na kutuhakikishia kuwa maneno haya wameyasikia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), juu ya kuwa ndani ya Hadiyth hizi wanatuhumiwa kuwa watakuja kurtaddi na kubadilisha na kuingiza Bida'h?

 

 

Tano: Wangelikuwa waliokusudiwa katika Hadiyth hizi ni Maswahaba ambao Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwahutubia na kuwahadithia juu ya matukio haya, asingelikuwa na haja ya kusema: "Watarudishwa makundi ya watu kutoka kwangu." Au "Watu miongoni mwa Swahibu zangu watarudishwa penye hodhi."  Au akasema: "Kisha atachukuliwa mmojawapo miongoni mwa Swahibu zangu." Badala yake angeliwaambia moja kwa moja bila kuwaficha, akawaambia kwa mfano: "Mtaondolewa penye hodhi, na kupelekwa mbali nami." Au "Fulani na fulani mtaondolewa penye hodhi." Na maneno yenye mfano huo, hii ikiwa ni dalili nyingine kuwa Maswahaba sio hawa waliokusudiwa katika riwaayah hizi.

 

 

Sita: Lafdhi zilizokuja katika riwaayah hizi kama vile 'Rahtw'   رهط  na maana yake ni kikundi cha watu wasiotimia kumi nk. Ni dalili kuwa watakaoondolewa ni wachache sana.

 

 

Saba: Wengine wakatoa hata majina ya baadhi ya Maswahaba watakaotolewa penye hodhi. Na sisi tunawauliza; Wametoa wapi kauli za kuwahusisha baadhi ya Maswahaba kuwa wao ndio watakaoondolewa penye hodhi, na kwamba wao ndio waliortaddi na kuzusha mambo katika Dini, kisha wakawapangia wengine kuwa hao hawataondolewa? Wakati Hadiyth hazikutaja kwa majina yupi ataondolewa na yupi atakayebaki. Ushahidi walioutumia dhidi ya wenzao unaweza pia kutumiwa dhidi ya wanaowataka wao, juu ya kuwa sisi hatusema hivyo, hasa kwa vile hapana nassw inayoeleza kwa uwazi kuwa fulani ataondolewa na fulani atabaki.  Hadiyth Swahiyh zimetuthibitishia kusifiwa kwa Maswahaba wote kwa ujumla, na kututhibitishia pia kuwa wao ni watu wa Jannah (Peponi).

 

 

Kwa hivyo tunasema; Hao Maswahaba mnaowadhania kuwa watarudishwa penye hodhi, zipo dalili nyingi sana kutoka kwenye Qur-aan na Sunnah zenye kuwasifia na kuwatakasa kwamba wao ndio walioamini hasa na kututhibitishia kwa dalili isiyokuwa na shaka kuwa wao ni watu wa Jannah.

 

 

Kutokana na haya, haki inadhihiri, na utatanishi unatoweka kwa sababu ya ushahidi usikuwa na uzito wowote.

 

 

Tunamuomba Allaah ('Azza wa Jalla)  Atupe mwisho mwema na Atufufue chini ya bendera ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake watukufu (Radhwiya-Allaahu ‘anhum).

 

 

Hitimisho:

 

 

Kwa kumaliza tunasema:

 

Kwanza; waliokusudiwa kuwa ni Maswahaba katika Hadiyth hizi si Maswahaba bali ni wanafiki waliokuwa wakijifanya Waislamu mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَمِمَّنْ حَوْلَكُم مِّنَ الْأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ ۖ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ ۖ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لَا تَعْلَمُهُمْ ۖ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ ۚ سَنُعَذِّبُهُم مَّرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَىٰ عَذَابٍ عَظِيمٍ﴿١٠١﴾

Na katika Mabedui wanaokuzungukeni wako wanafiki. Na katika watu wa Madiynah (pia) walibobea katika unafiki. Huwajui (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Sisi Tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili; kisha watarudishwa katika adhabu kuu. [At-Tawbah: 102]

 

 

 

Pili;  Waliokusudiwa ni wale waliortaddi baada ya kufariki dunia Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inajulikana kuwa wengi miongoni mwa makabila ya Kiarabu yalirtaddi baada ya kufariki dunia Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hawa ndio kwa ajili yao Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atasema: "Swahibu zangu hawa." Na ataambiwa: "Hujui wewe waliyozusha baada yako. Waliendelea hawa kurtaddi tokea ulipofariki dunia."

 

 

Tatu; Inaweza kumaanisha pia kuwa kila aliyemuona Rasuli wa Allaah (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama hakuwa Swahaba kwa maana ya neno hilo, na dalili ni yule mkuu wa wanafiki ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluwl aliposema:

 

 

 لَئِن رَّجَعْنَا إِلَى الْمَدِينَةِ لَيُخْرِجَنَّ الْأَعَزُّ مِنْهَا الْأَذَلَّ ۚ وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿٨﴾

Tutakaporudi Madiynah, mwenye hadhi zaidi bila shaka atamfukuza humo aliye dhalili. Na ilhali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui. [Al-Munafiquwn – 8]

 

 

 

 

 

 

 

Share