Mume Haelewani Na Nduguze, Kampa Talaka Yumo Ndani Ya Arubaini Je, Talaka Yake Imesihi?

SWALI:

 

assalaam alaykum warahmatullah wabarakaatuh, kwanza kabisa jazaakum allah kher kwa msaada wenu kwetu, inshaallah iwe kwenye mizani yenu siku ya kiama ameen yarabb. swali langu ni ndugu zangu na mume wangu walikuwa hawaelewani na sababu ni mume wangu, hali hiyo ilikuwa inasababisha ugomvi kati yangu na mume wangu. siku moja baada ya kujifungua mtoto wangu tulikuwa tunaongelea suala hilo hilo akakasirika na kuniacha hospitalini peke yangu baada ya mda akanipigia simu na akaniuliza nichagua kati yake na kaka zangu kabla sijamjibu kitu akanipa talaka, je hii talaka ni sahihi? Kwa kuwa hapakuwepo na mashahidi? na eda  yangu nikae vipi kwa kuwa mimi ni mzazi nisubri nikimaliza arubaini nianze eda ya talaka au nianze kuhesabia na arubaini?


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kupewa talaka kwa simu.

Mwanzo ni kuelewa talaka inapotamkwa na mume kwa sababu ya hasira au katika hali ya utulivu, mke akiwa katika hedhi au tohara, katika damu ya nifasi au nje yake, kukiwa na mashahidi au hakuna; talaka inakuwa imepita.

 

Kwa hiyo, wewe sasa umeachika pamoja na kuwa mume wako ana makosa na dhambi kwani alikuwa hafai yeye kukuacha katika hali ya kuwa uko katika damu ya uzazi. Kwa hali yoyote ile talaka imepita na ndio eda yako imeanza. Eda yako itamalizika pindi damu ya nifasi itakapokuwa haitoki tena, yaani damu ya nifasi ikisimama kutoka na eda yako itakuwa imemalizika.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share