Sayyid Al-Istighfaar (Bwana Wa Du'aa Zote Za Tawbah)

 

Du'aa - Adhkaar

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu-Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Allaah Anasema:

 

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾

Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua [Al-‘Imraan: 135]

 

Imesimuliwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Allaah huifurahia toba ya mja wake kuliko mmoja wenu anapokuwa juu ya mnyama wake jangwani akamuangusha na kumkimbia." [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

Na katika riwaya ya Muslim na wengine:

 

"Allaah huifurahia toba ya mja wake kuliko mmoja wenu anapokuwa juu ya mnyama wake jangwani akamuangusha na kumkimbia. Mnyama huyo akiwa amebeba chakula chake na maji yake, kisha mtu huyo akakata tamaa, akauendea mti na kuegemea chini ya kivuli chake akiwa keshakata tamaa ya kumuona mnyama wake tena. Na anapokuwa katika hali hiyo, ghafla anamuona mnyama wake mbele yake. Akazishika hatamu zake, kisha akasema kwa furaha: "Rabb wangu Wewe ni mja wangu na mimi ni Rabb wako". Alikosea kwa wingi wa furaha."

 

Na maana ya Allaah kuifurahia toba hiyo ni kuwa anaridhika na nia ya mja wake huyo juu ya kuwa alikosea kutamka.

 

Miongoni mwa du’aa za kuomba maghfira, ni hii du’aa inayoitwa 'Sayyidul-Istighfaar' (Du’aa bora ya kuomba maghfira kupita zote) aliyotuusia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Du’aa ambayo ndani yake imekusanya maana zote za tawbah na kukiri, na kwamba hapana mwenye kusamehe makosa isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Imeposimuliwa kutoka kwa Shaddaad bin ‘Aws (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Bwana wa kuomba maghfira ni kusema:

 

اللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي لا إِلَهَ إلا أَنْتَ خَلَقْتَنِي وَأَنَا عَبْدُكَ وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اسْتَطَعْتُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي فَاغْفِرْ لِي فَإِنَّهُ لا يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلا أَنْتَ.

Allaahumma anta Rabbiy laa ilaaha illa Anta. Khalaqtaniy wa ana ‘abduka. Wa ana ‘alaa ‘ahadika wa wa’adika ma statwa’atu. A’udhu bika min sharri ma swana’atu. Abu-u laka bini’imatika ‘alayya wa abu-u laka bidhanbiy, faghfirliy, fainnahu laa yaghfiru dhunuuba illaa anta."

 

Akasema: "Atakayesema hayo wakati wa mchana akiwa na yakini juu yake akafa siku hiyo kabla ya usiku kuingia, huyo ni katika watu wa  Jannah (Peponi). Na atakayesema hayo wakati wa usiku akiwa na yakini juu yake akafa kabla ya asubuhi kuingia, huyo ni katika watu wa Jannah (Peponi)." [Imepokewa na Al-Bukhaariy, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na wengine]

 

 

Maana Yake

 

 

Ee Allaah. Wewe ni Rabb wangu hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Wewe

اللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي لا إِلَهَ إلا أَنْتَ

Umeniumba na mimi ni mja Wako

خَلَقْتَنِي وَأَنَا عَبْدُكَ

Na mimi nimo katika kutekeleza maamrisho Yako na waadi Wako niwezavyo

وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اسْتَطَعْتُ

Ninajikinga Kwako na kila shari niliyoitenda

أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ

Ninakiri Kwako kwa neema Zako juu yangu

أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ

Na ninakiri Kwako juu ya dhambi zangu

وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي

Kwa hivyo unisamehe kwa sababu hapana mwenye kusamehe madhambi isipokuwa Wewe

فَاغْفِرْ لِي فَإِنَّهُ لا يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلا أَنْتَ

 

 

Share