Zingatio: Ikhlaasw Sahihi Ndio Kutakabaliwa ‘Ibaadah

 

Zingatio: Ikhlaasw Sahihi Ndio Kutakabaliwa ‘Ibaadah

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ikhlaasw ni kumuabudia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) peke Yake bila ya kumshirikisha na yeyote au chochote kwa lengo la kupata radhi za Muumba wala si vyenginevyo. Kinyume na hapo basi hiyo siyo ‘Ibaadah kwani itakuwa inakwenda kinyume na mafundisho sahihi ya Qur-aan na Sunnah ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ikhlaasw ndio mzizi wa ‘Ibaadah, hivyo kwa kila tendo tunalolitenda ni wajibu kuliunganisha kwa ajili tu ya kupata ridhaa za Rabb wetu (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Muislamu anawajibika pindi anaposwali, kuswali tu kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Halikadhalika, katika harakati za maisha, yahitajika kufanya bidii ya kutafuta riziki kwa njia ya Ikhlaasw, nako ni kutafuta riziki katika njia za halali pamoja na kuwa mbali kabisa na hali yoyote inayoelekea kwenye haramu.

 

Kwa wakati wa leo, hatuna budi pia kukumbushana kuhusiana na akiba za fedha zilizo halali. Hili linaenda sambamba kwa kuchukua au kulipa mikopo. Yahitajika kwa kila Muislamu kuelewa kwamba ni wajibu wake hata kwa fedha anazozitunza, iwapo ni shilingi (ndogo) au riyali (kubwa) wa kadhalika, zote aziweke kwa ikhlaasw, huku ni kuweka akiba hizo bila ya kuingiziwa chumo la haramu kama vile ribaa.

 

Mikopo pia ni moja wapo ya ‘Ibaadah, iwapo tu pale inapoegemezwa kwa kupata ridhaa za Rabb wetu (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hapa anawajibika Muislamu kuhakikisha anachukua mkopo huo kwa njia ya uadilifu, na kuirejesha amana hiyo mara tu muda wake unapowadia. Naye, kwa mkopeshaji, analazimika kutoingiza wala kuchukua ribaa kwa lengo tu la ikhlaasw (kupata ridhaa ya Allaah). Hapo ikhlaasw itakuwa sahihi na ‘Ibaadah kutimia, ambayo bila ya shaka yoyote itakuwa na malipo mema mbele ya Muumba.

 

Kinyume cha hapo, ni mikopo ya ribaa, kama vile mortgages, mikopo mepesi ya kipebari/kimasomo soft loans, ambayo takriban kwa asilimia kubwa ina ribaa ya kumuumiza mkopaji, na hasara iliyoje kwa mkopaji huyu duniani na akhera. Amekosa ‘mtoto na maji ya moto’, duniani atateseka kwa kujilimbikiza mali isiyomalizika na kujitia mashakani kwa madeni ya watu/taasisi za benki, halikadhalika kwa Akhera naye atakutana na hali ngumu ya kushindwa kujitetea ni kwa hoja gani aliikubali riba hiyo, hali ya kuwa Allaah Ameshatangaza vita kwa kila mwenye kula ribaa: 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴿٢٧٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na acheni yaliyobakia katika ribaa ikiwa nyinyi ni Waumini. [Al-Baqarah: 278]

 

Ikhlaasw ndani ya ‘Ibaadah ina mifano mingi sana, ambayo tukitaka kuziorodhesha hapa, haitatosha wala haitakuwa na natija nzuri. Cha muhimu ambacho Muislamu anawajibika kuelewa kwamba, ili tendo lolote liweze kulipwa kwa thawabu, ni lazima liegemee katika ikhlaasw sahihi bila ya kusahau kwamba, tendo hilo ni lazima liendane kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Qur-aan na Sunnah. Mfano wa tendo la ndoa, litakuwa na malipo mema pale tu linapotendeka ndani ya ndoa, kinyume na hivyo (yaani litakapotendeka nje ya ndoa), halitakuwa na malipo yoyote, bali litalipwa kwa malipo ya dhambi.

 

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) juu ya kufanya ‘Ibaadah zisizoendana na mafunzo sahihi, kama vile kutokuwa na ikhlaasw: 

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan: 23]

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Atakayetenda kitendo kisichokuwa na mafunzo ya Dini yetu basi kitarudishwa.” [Al-Bukhaariy]

 

Twamuomba Rabb atupe muangaza wa kuiona haki tukaifuata, na tukaiona batili tukaweza kuiacha.

 

 

 

Share