Ummu Haraam Bint Milhaan (رضي الله عنها)

 

Ummu Haraam Bint Milhaan (رضي الله عنها)

Na Ukoo Wake

 

Na Muhammad Faraj Saalim As -Sa'iy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Haraam bin Milhaan na Sulaym bin Milhaan pamoja na dada zao Ummu Haraam bint Milhaan na Ummu Sulaym bint Milhaan (Radhwiya Allaahu 'anhum) ni ndugu wanne waliosilimu wote kwa pamoja tena siku moja mara baada ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwasili mji wa Madyinah.

 

Ndugu hawa walikuwa wakipendana sana na walikuwa wakimpenda sana Allaah na wakimpenda Rasuli Wake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na wote kwa pamoja walikuwa na shauku kubwa ya kufa kifo cha shaahid kwa ajili ya kupata ushindi wa kuingizwa katika Pepo ya Mola wao Subhaanahu wa Ta'aalaa. 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwapenda sana watu wa nyumba hii, na imepokelewa kuwa mara nyingi alikuwa akiwatembelea wakati wa mchana, akila na kuswali kwao swala za Sunnah.
Ndugu wa kike walipewa majina ya kubandika (kun-yah), wakaitwa Ummu Haraam na Ummu Sulaym ingawaje kwa uhakika wao hawakuwa mama wa Haraam wala wa Sulaym bali walikuwa dada zao.

 

 

Haraam Na Sulaym Bin Milhaan  (Radhwiya Allaahu 'anhumaa)

Kundi la mabedui lilikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtaka awape watu wende nao katika kijiji chao kwa ajili ya kuwafundisha dini ya Kiislamu. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akachagua watu sabiini watakaokwenda na watu hao, na wote sabini walikuwa katika waliohifadhi Qur-aan wakiongozwa na Swahaba huyu mtukufu Haraam bin Milhaan (Radhwiya Allaahu 'anhu).

Walipowasili katika kijiji cha mabedui hao wakatakiwa Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wasubiri nje, kisha wakaanza kuingizwa ndani mmoja mmoja. Wa mwanzo kuingia alikuwa Haraam (Radhwiya Allaahu 'anhu), na mara baada ya kuingia na kusimama mbele ya mkubwa wa kabila hilo, ikatolewa ishara ya mkono kuashiria kuwa kazi ianze. Kwa haraka sana mmoja katika maaskari waliosimama nyuma, alimrushia Haraam mkuki uliomchoma na kupenya mgongoni mwake, ukaingia na kuchomoza chini baina ya mapaja yake. Haraam (Radhwiya Allaahu 'anhu) alijaribu kusimama, lakini miguu yake haikuwa na nguvu ya kumzuwia, akaanguka chini huku akisema kwa sauti kubwa;
Allaahu Akbar! Fuztu wa Rabbil-Ka'bah”.
Na maana yake ni (Allaah ndiye mkubwa! – Nimefuzu (kuingia Peponi) Naapa kwa Aliyeiumba Al Kaaba).

Anasema Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye ni mwana wa Ummu Sulaym;
“Mjomba wa`ngu alipoanguka chini, alikuwa akiichota damu yake kwa mikono yake na kujipaka nayo usoni na kichwani kwa furaha huku akisema (Fuztu wa Rabbil-Ka'bah)”.

Kisha wakaingizwa ndani Maswahaba waliobaki mmoja baada ya mwengine akiwemo Sulaym bin Milhaan na kuuliwa wote sabiini isipokuwa mmoja tu anayesemekana kuwa alikuwa kiguru, akafanikiwa kukimbilia majabalini na kuweza kufika kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumfikishia habari hizo.

Kisa hiki kinatujulisha namna gani Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walivyoifikia daraja ya yakini, na namna gani walivyokuwa na shauku kubwa ya kufuzu kwa kifo cha Shaahid katika njia ya Allaah Subhanahu wa Ta'aalaa.

 

Hapana kilichokuwa kikimshughulisha Swahaba huyu (Radhwiya Allaahu 'anhu) pale alipokuwa anakufa isipokuwa kufuzu kwake kuingia Peponi. Alikuwa akiichota damu yake kwa mikono yake miwili na kujipaka nayo kichwani na usoni huku akitamani pale atakapokutana na Mola wake amwambie kwa furaha;
“Ee Mola wangu! Hii ni damu yangu iliyomwagika kwa ajili Yako”.
Ummu Haraam, dada yake shaahid huyu aliposikia habari za kufa kwa ndugu zake, alinyanyua mikono yake juu na kuomba;
“Mola wangu, na mimi niruzuku kifo cha shahada ili niweze kujumuika nao katika Pepo Yako”.

 

Haya ndiyo yaliyokuwa yakibeba vifua vya watu hawa. Je na wewe shauku gani uliyoibeba kifuani pako?

 

 

Ummu  Sulaym Bint Milhaan  (Radhwiya Allaahu 'anhaa)

Ummu Sulaym (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwanza aliolewa na Maalik bin Nadhar aliyezaa naye mtoto waliyempa jina la Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu), na kwa vile Maalik huyu hakutaka kuingia katika Dini ya kiislamu ikabidi waachane wakati mtoto wao bado yungali mdogo na kwa ajili hiyo mtoto akabaki kwa mama yake.

Tokea Anas alipokuwa mtoto mchanga, Ummu Sulaym alikuwa akijitahidi sana kumfundisha mwanawe kutamka; “laa ilaaha illa Allaah”, jambo lililokuwa likimkera sana Maalik bin Nadhar aliyekuwa akiabudu masanamu.

Baada ya kuachana na Malik bin Nadhar, Ummu Sulaym akaposwa na Abu Talha al - Answaar, lakini kwa vile naye pia hakuwa Muislamu, Ummu Sulaym hakukubali kuolewa naye, akamwambia;
“WaLLaahi watu wenye mfano wako si wa kukataliwa wanapopeleka posa zao, lakini wewe ni kafiri na mimi ni Muislaam na haijuzu mimi kuolewa na wewe mpaka usilimu kwanza. Na kama utasilimu, basi mahari yako kwangu yatakuwa kusilimu kwako na wala sitotaka kitu kingine chochote zaidi kutoka kwako”.
Anasema Anas bin Malik (Radhwiya Allaahu 'anhu);
“Abu Talha akasilimu na akamuoa Ummu Sulaym na hapana mahari bora yaliyowahi kutolewa kuliko mahari hayo (ya kusilimu kwa Abu Talha)”.

 

 

Baadhi Ya Sifa Za Ummu Sulaym

Imepokelewa kuwa katika vita vya Hunayn, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitangaza kuwa yeyote atakayemuuwa kafiri achukuwe kila kitu chake, na kwamba Abu Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) siku hiyo aliwauwa makafiri ishirini na kuchukuwa walivyokuwa navyo. Abu Talha akamuona Ummu Sulaym katika uwanja wa vita akiwa amebeba jambia, siku ambayo wanaume kweli walikimbia uwanjani. Akamuuliza;
“Ewe Ummu Sulaym, nini hiki ulichobeba?”
Akajibu;
“Nilitamani waLLaahi wanisogelee baadhi yao ili niwapasue matumbo yao.”

Imeelezwa na Abu Daawuud kuwa siku hiyo watu waliobaki katika uwanja wa vita pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa Abu Bakr na 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa), na katika watu wa nyumba yake walikuwa 'Ally na Al-'Abbas na Abu Sufyan bin Haarith bin Abdul-Muttwalib pamoja na mwanawe Ja'far na Usaamah bin Zayd na Ayman mwana wa Ummu Ayman na Rabi'ah bin Al-Haarith na wachache wengineo (Radhwiya Allaahu anhum).

Ama katika wanawake aliyebaki uwanjani ni huyu Ummu Sulaym (Radhwiya Allaahu 'anhaa) akiwa ameshika kamba za ngamia wa mumewe Abu Talha Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) huku amebeba jambia.

 

Ummu Sulaym na Abu Talha (Radhwiya Allaahu 'anhaa) wakajaaliwa kupata mtoto waliyempa jina la 'Umayr, na alipotimia umri wa miaka tisa mtoto huyo aliumwa sana, na Abu Talha aliyekuwa akimpenda sana mwanawe huyo akawa anamuuguza huku akimuonea huruma sana na hakutaka kuondoka karibu yake. Ummu Sulaym alipomuona mumewe katika hali ile akamwambia;
“Nenda wewe kafanye shughuli zako na mimi nitamuuguza mtoto”.

Abu Talha akakubali na mara baada ya kutoka nyumbani mtoto wao akafariki. Ummu Sulaym akamfunika vizuri mwanawe na aliporudi mumewe hakumwambia kuwa mtoto wao keshakufa.

Mumewe akauliza;
“Vipi hali ya mtoto wetu?”
Akajibu;
“Ametulia sana”, yeye akimaanisha kuwa mtoto wao keshakufa, wakati mumewe akidhani kuwa mtoto keshalala.
Ummu Sulaym akajipamba vizuri kwa ajili ya mumewe usiku huo, akampikia chakula kizuri, na baada ya kula chakula cha usiku akalala naye na usiku huo akashika mimba nyingine. Walipoamka asubuhi Ummu Sulaym akamwambia mumewe;
“Mume wangu, unaonaje ikiwa jirani yetu ametuazima chombo na tukabaki nacho chombo hicho kwa muda wa miaka tisa, kisha jirani huyo akataka tumrudishie mwenyewe chombo chake, je tumkatalie?”
Mumewe akajibu;
“Laa, hapana, lazima tumrudishie”.
Ummu Sulaym akasema;
“Basi Allaah keshaichukua amana Yake Aliyotukabidhi, mshukuru Mola wako kwani mtoto wetu keshafariki”.
Abu Talha (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikasirika sana kwa kitendo hicho akaondoka na kwenda moja kwa moja mpaka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumshitakia.  Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasema;
“Ulilala naye usiku huu?”
Talha  akajibu;
“Ndiyo ewe Rasuli wa Allaah”.
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;
“Mola wangu wabarikie katika usiku wao”.

Ummu Sulaym alipojifungua, wakamchukuwa mtoto wao na kumpeleka moja kwa moja mpaka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na katika riwaya nyingine akenda kuitwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihinwa sallam) na alipowasili akachukua tende na kuitafunatafuna na baada ya kulainika akamlisha mtoto huyo (kitendo hiki kinaitwa Tahanik), kisha akampa jina la AbduLLaah. Anasema Ibni Ayinah kuwa AbduLLaah huyu alijaaliwa kupata watoto tisa na wote walihifadhi Qur-aan yote.

Bibi huyu ni mfano bora kwa wale wanawake wanaopiga kelele na kuomboleza wakati wa misiba na kusema maneno yasiyokuwa na maana yoyote, na mfano mwema wa mwanamke anayefahamu vizuri wajibu wake nyumbani kwake na katika kuisimamia dini ya Mola wake.

 

 

Ummu Haraam Binti Milhaan (Radhwiya Allaahu 'anhaa)

Imepokelewa katika Al - Bukhaariy na Muslim na Muwatta na kutoka kwa Ibni Mardawia na wengine kuwa siku moja Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda kumtembelea Ummu Haraam aliyekuwa mke wa Swahaba maarufu 'Ubaadah bin Asw-Swaamit (Radhwiya Allaahu 'anhum), na baada ya kula chakula alichokaribishwa, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akaegemea ukutani kwa ajili ya kujipumzisha - usingizi ukamchukuwa, kisha ghafla akaamka huku akiwa anacheka.
Ummu Haraam (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alipomuona katika hali ile akamuuliza;
“Kipi kilichokufurahisha ewe Rasuli wa Allaah?”
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;
“Nimeoneshwa (Nimeoteshwa) watu katika ummati wangu, watakaopigana Jihaad katika njia ya Allaah, wataivuka bahari na kuiteka miji mfano wa wafalme watakaokaa juu ya vitanda vyao (Peponi) bila shaka yoyote ile”.
Ummu Haraam akasema;
“Ewe Rasuli wa Allaah, muombe Allaah Anijaalie niwe mmoja wao”.
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;
“Wewe ni katika wa mwanzo wao”.

Baada ya kupita zaidi ya miaka ishirini tokea Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihinwa sallam) alipooteshwa ndoto hiyo, wakati wa ukhalifa wa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu), jeshi la mwanzo la baharini la Waislamu liliundwa chini ya uongozi wa Mu'awiyah bin Abi Sufyaan (Radhwiya Allaahu 'anhu). Jeshi hilo liliondoka kuelekea nchi ya Cyprus akiwemo ndani yake Ummu Haraam pamoja na mumewe 'Ubaadah bin Asw-Swaamit (Radhwiya Allaahu 'anhum), na baada ya vita vikali likafanikiwa kukiteka kisiwa cha Cyprus.

Siku moja alipokuwa katika shughuli za kuwahudumia wanaopigana Jihaad, na katika riwaya nyingine, siku ile alipokuwa akiteremka pwani mara baada ya kuwasili Cyprus, Ummu Haraam alianguka kutoka juu ya mnyama aliyekuwa amempanda na kufariki dunia hapo hapo.

Bishara ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikatimia na Ummu Haraam (Radhwiya Allaahu 'anhaa) akawa mtu wa mwanzo kufariki dunia juu ya ardhi ya kisiwa hicho.

Ama kuhusu kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema;
“Mfano wa wafalme watakaokaa juu ya vitanda vyao (Peponi) bila shaka yoyote ile”
Hii ni tafsiri ya kauli yake Subhanahu wa Ta'aalaa aliposema;

 

عَلَىٰ سُرُرٍ مَّوْضُونَةٍ ﴿١٥﴾

 (Watakuwa) Juu ya makochi ya fakhari yaliyotonewa kwa ustadi, vito (vya thamani).

مُّتَّكِئِينَ عَلَيْهَا مُتَقَابِلِينَ ﴿١٦﴾

 Wakiegemea juu yake wakikabiliana.
[Al-Waqi'ah: 15-16]

 

 

Utukufu Wa Mwanamke Katika Uislaam 

Tulisoma siku za nyuma kuwa wa mwanzo kuingia katika Uislamu ni mwanamke – Bibi Khadiyjah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) mke wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam).

Shahidi wa mwanzo katika Uislamu ni mwanamke – Sumayyah (Ummu 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhaa)).

Na mwanamke wa mwanzo kufa shahidi katika nchi za ulaya (Europe) akiwa katika Jihaad ni mwanamke huyu Ummu Haraam (Radhwiya Allaahu 'anhaa).

Kaburi lake liko mpaka leo kisiwani Cyprus limeandikwa juu yake;
“Hili ni kaburi la mwanamke mchaji Allaah Ummu Haraam.

 

 

Share