Zingatio: Kila Kiumbe Kimeumbwa Kwa Hikmah

 

Zingatio: Kila Kiumbe Kimeubwa Kwa Hikmah

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kwa hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameiumba dunia na vilivyomo ndani yake kwa hikmah Yake na kwa kuwapatia mazingatio wale ambao wanawaza na kufikiria Ukubwa wa Rabb Wake.

 

Ndio wale ambao wanapokaa, wanaposimama na wanapolala kila wakati huwaza na huwazua ni kwa namna gani Allaah Ameweza kuwaumba viumbe wote kwa hikmah Yake isiyo kifani. Hili ndilo kundi la Waislamu ambao kwayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewatambua kuwa ni wacha wa Allaah:

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto. [Al-‘Imraan: 191]

 

Rabb Atujaalie nasi tuwe ni miongoni mwa hao wacha wa Allaah – Aamiyn.

 

Kwa kuangalia umbile, rangi na hulka ya kiumbe mmoja kumlinganisha na mwengine, basi Muislamu anaweza kupambanua ujuzi wa Muumba. Mfano wa baharini, kuna viumbe ambao ni wakubwa sana (mfano nyangumi) hadi samaki wadogo wadogo (kama vile dagaa), ambao juu ya tofauti yao basi tundu waliyopewa ya kuvutia pumzi haina tofauti sana, isipokuwa kwa ukubwa wa umbile la samaki husika. Pamoja na aina nyengine ya samaki, wote wamepatiwa njia za kuishi na halikadhalika kutafuta riziki zao. Humuoni nyangumi akapita njia za kawaida anazopita samaki dagaa wala kinyume chake.

 

Tuwaangalie wanyama wanaofugwa majumbani, iwapo ni kuku au kondoo au mbuzi n.k. wote wanapotolewa katika mabanda yao nyakati za asubuhi, katu hawatajizonga kutafuta chakula katika sehemu moja, kila mmoja atamuachia mwenziwe hatua kadhaa baina yake na mwenziwe – mmoja ataenda kulia na mwengine kushoto, huku Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) akiwafungulia riziki Zake zisizo na mipaka. Cha kujiuliza ni nani Aliyewafunza hili? Hapana mwengine isipokuwa ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Basi ni kwa ukubwa gani Aliokuwa nao Rabb Muumba kwa kiumbe mfano wa kinyonga, anayebadilika rangi kulingana na mazingira aliyopo! Dakika hii ni mweusi, mara ghafla amebadilika na kuwa mweupe na mfano wa hayo. Huyu kinyonga amejibadilisha mwenyewe? Je, tumepata kuwaza ni kwa namna gani kinyonga huyu anatii amri za Rabb Muumba na kwa wakati huo huo kuwa ni ruwaza njema kwa Waumini?

 

Hatujaingia bado katika wale viumbe ambao Rabb (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewaumba kwa miguu tofauti, lakini juu ya hayo wote wamepatiwa mwendo wa kuweza kwenda kumzidi mwenziwe. Tumuangalie kangaroo anavyorukaruka kwa miguu yake miwili kisha mulinganishe na simba anayekimbia kwa miguu minne – mwendo wa kangaroo unamtosha sana kukimbia kutokana na maumbile yake na zaidi kwa kangaroo jike ambaye ana sehemu ndani ya mwili wake ya kumlea mwanawe mfano wa mfuko. Tofauti na simba ambaye amepatiwa miguu minne, madhubuti kabisa kutokana na mazingira yake ya kuwinda wanyama wenziwe. Je, kangaroo aliumbwa na miguu minne, akaitoa miwili na kumpatia simba? Watueleze wale ambao mungu wao ni ‘Nature’? Hakuna wasiwasi wowote kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Aliyemuumba kangaroo/simba na kumjaalia miguu miwili/minne kutokana na Hikmah zake Rabb Mlezi.

 

Maelezo yote hapo juu yanathibitishwa kwa uwazi kabisa ndani ya Qur-aan kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاللَّـهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِّن مَّاءٍ ۖ فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ أَرْبَعٍ ۚ يَخْلُقُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤٥﴾

Na Allaah Ameumba kila kiumbe kinachotembea kutokana na maji. Basi miongoni mwao wanaotembea juu ya matumbo yao, na miongoni mwao wanaotembea kwa miguu miwili, na miongoni mwao wanaotembea juu ya minne. Allaah Anaumba Atakavyo. Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Muweza.

 [An-Nuwr: 45]

 

Hapana shaka yoyote kwamba mifano ni mingi kupita maelezo, na hatuwezi kuyaeleza wala kuyamaliza yote. Isipokuwa tu tumalizie kwa kusema – Ametakasika Rabb Ambaye Ameumba kila kiumbe kwa Hikmah Yake isiyokuwa na mfano.

 

 

Share