Uzazi Wa Kupandikiza Wa Chupa (Test Tube) Unafaa?

 

SWALI:

Nnapenda kujua kuwa ni halali au haramu kwa mwanamke ambaye  hakujaaliwa kuzaa kwa njia ya kawaida,akafanyiwa njia ya kitaalamu ya  kuwekewa mbegu za kiume ili kupata uja uzito?

 


 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kutokana na  Baraza la Sheria la Kiislam     (Fatawa ya Islamic Fiqh Council)  katika mwaka 1404  Hijriyah  wameruhusu kufanyika uzazi wa njia hii ya kitaalamu kwa kuweka shuruti zao na maoni yao kama haya : 

Kuchukua mbegu ya mwanamke na mwanamume ambao ni mume na mke ili kufanya 'vitro-fertilization' ya mbegu hizi kabla ya kuipandikiza katika fuko la uzazi la mwanamke ambalo ndipo ilipochukuliwa mbegu yake, imekubaliwa katika Islam, lakini huenda kukaa na mashaka kutokana na taratibu zake.  Kwa hiyo kwanza kabisa, aina hii ya uzazi Isiwe Inapendekezeka kutendwa isipokuwa tu ikiwa hakuna budi.  Na pindi ikibidi kutendeka basi shuruti hizi zihakikishwe kuwa zinafuatwa:

  1. Mwanamke asionyeshe kabisa sehemu zake za siri "private part"  isipokuwa kwa mumewe, ila tu ikiwa hakuna budi .

  2. Kwa hiyo kwanza kabisa ajaribu mwanamke kutafuta Daktari Mwanamke Muislam, ikiwa hakupatikana basi atafutwe Daktari Mwanamke Asiye Muislam, ikiwa hakupatikana basi atafutwe Daktari Mwanamume Muislam mwenye kuaminika na kama hakupatikana basi Daktari Mwanamume asiye Muislam muaminifu.  Mpango huu wa kufuatana kutafuta Daktari ni wa kisheria ya Kiislamu katika kufanya matibabu ya mwanamke. Na ufanyike kwa jitihada hasa katika kufanya aina ya taratibu ya kizazi cha aina hii na matibabu yoyote yanayomuhusu mwanamke kwa magonjwa ya kike. 

  3. Ikiwa hakupatikana Daktari mwanamke basi haifai mwanamke kuweko peke yake na Daktari mwanamume, itabidi lazima aweko mumewe au aweko mwanamke mwenzake katika jamaa zake.

  4. Operesheni 'Surgery' lazima ifanywe na madaktari walio na ufundi huo 'professionals' ambao wameruhusiwa kufanya kazi hiyo ili kuhakikisha kuwa ni kazi ya uhakika na kutumainika, ukamilifu wake na usalama wa utaratibu wake. 

Jambo muhimu la kuzingatia na lenye kukhofiwa katika aina hii ya uzazi ambalo kama halikuhakikishwa litasababisha  hatari kubwa ya kutoka nje ya sheria ya Kiislamu. Nalo ni kuhakikisha kuwa mbegu za uzazi 'sperm' zitakazowekwa katika fuko la uzazi la mwanmke ni mbegu hakika za mumewe na si za mtu mwingine.

Khofu  za Maulamaa wanaopinga jambo hili ni kama zifuatazo:

  1. Khofu kwamba pengine mtoto akawa kilema, hivyo itakuwa mashaka kwa wazazi na mtoto, badala ya furaha na kinyume na matarajio.

  2. Uwezekano wa shaka kwamba  Daktari pekee ndiye atakaye hakikisha kuwa amefanya sawa sawa bila ya kufanya khiana katika upandikizaji wa mbegu ya mwanamke na mbegu ya mumewe kwani pengine Daktari huyo kama si muaminifu huenda akafanya khiana kwa kumuonea huruma mwanamke mwengine ambaye labda ni mgonjwa wake wa siku nyingi mwenye kutamani sana kizazi na kumpa au kupandikiza mbegu hizo za mwengine kwake au hata kuziuza kwa wengine wenye mahitajio hayo, ndio maana ni muhimu sana kutafuta Daktari Mwanamke kwanza wa Kiislamu anayeaminiwa kufanya mpango huu wa uzazi.

  3. Shaka na rai mbali mbali za maulamaa kuhusu  mume mwenye  mbegu kidogo ambazo zinabidi kwanza kuweka katika banki ya kuhifadhi na kukuza mbegu hizo . 

 

  • Kundi la mwanzo la  wataalamu wanaona kuwa inakubalika ikiwa kuhifadhi mbegu na kutungwa huko (kwa mimba) kutafanyika wakati mume yuko hai bado, kwani huchukua muda.  

  • Kundi la pili  wameona kuwa inakubalika hata baada ya kufa mume lakini kabla ya mwanamke kumaliza Eda yake.  

  • Kundi la tatu  wameona kuwa mbegu hizo ziharibiwe  na zisiwekwe kwa kutumika tena.  Hii inapasa pia kuharibiwa na mbegu za mwanamke hali kadhalika ikiwa kabla ya utungisho (wa mimba) au hata baada ya kuwa utingisho 'fertilized'. 

     Sababu ya kukataza jambo hili ni kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganyika mbegu hizi katika banki hizo zinazohifadhi na kukuza mbegu, au hata zinaweza kuchukuliwa na kutumika isivyopasa kama kumtumilia mgonjwa ambaye ni mwenye mahitajio makuu (desprate) ya kutaka uzazi kwa hiyo ikawa imeanguka pengine na kukapatikana uchanganyikaji wa nasaba na ikawa ni katika dhambi kubwa.

Wa Allaahu A'alam

 

Share