Kunyonyesha Kupindukia Mipaka ya Miaka Miwili Inafaa?

 

SWALI:

Muda wa kunyonyesha ni miaka 2 nijuavo jee ukipitisha ikawa umenyonyesha mpaka miaka 2 na nusu inakuaje?

 

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kunyonyesha mtoto. Hakika ya muda ni kama ulivyosema, na hivyo ndivyo Alivyotuelezea Allaah Aliyetukuka:

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha” (2: 233).

Kwa mujibu wa Aayah hii tunafahamishwa kuwa mama anaweza kumnyonyesha mtoto wake mpaka miaka miwili.

Sasa kwa sababu moja au nyingine ikiwa mama amenyonyesha kwa zaidi ya miaka miwili itakuwaje. Jawabu kwa hilo linapatikana katika dalili zifuatazo:

  1. Ibraahiym bin ‘Uqbah alimuuliza Sa‘iyd bin al-Musayyab kuhusu kunyonyesha. Sa‘iyd akasema, “Yote ambayo yanafanyika katika miaka miwili ya mwanzo, hata ikiwa ni tone moja, inafanya kuwa haramu. Chochote kinachotokea baada miaka miwili, ni kama chakula kinacholiwa” (Maalik). Ibraahiym bin ‘Uqbah akasema: “Kisha nikamuuliza ‘Urwah bin az-Zubayr, naye akaniambia sawa na nilivyoambiwa na Sa‘iyd bin al-Musayyab”.

  1. Naaf‘iy amempokea ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) akisema: “Hakuna ukaraba kwa kunyonya ila kwa mtu aliyelelewa na kunyonya akiwa mdogo. Hakuna ukaraba kwa kunyonya kwa aliye na zaidi ya miaka miwili” (Maalik).

Kwa mujibu wa athari (masimulizi kutoka kwa Maswahaba) hizi kunakuwa hakuna tatizo ikiwa mtoto amenyonya kwa zaidi ya miaka miwili.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share