Israa Na Mi'iraaj: Kisa Cha Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه)

 

Israa Na Mi’iraaj:Kisa Cha Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Muhammad Faraj (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Mara baada ya kurudi katika safari ya Miraji aliyopelekwa ndani yake mpaka mbingu ya saba, kisha akasogezwa mahali panapoitwa ‘Sidratul Muntaha na kuzungumza na Rabb wake Subhaanahu wa Ta’aalaa, kisha akarudishwa ardhini katika usiku huo mmoja, na kabla ya kumhadithia mtu yeyote juu ya safari yake hiyo adhimu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa kimya nje ya msikiti wa Al-Kaabah, na Abu Jahal alipomuona katika hali ile akamuendea na kuanza kumkejeli huku akimuuliza.

 

 

"Enhe! Vipi pana habari yo yote mpya kutoka mbinguni leo?"

 

Kwa utulivu na upole Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu:

 

"Ndiyo, nilipelekwa usiku wa leo mpaka Baitul Maqdis (Palestina)."

 

Abu Jahal: "Na asubuhi hii ukarudi Makkah?"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Naam, na nilisali na ndugu zangu Rusuli huko."

 

Abu Jahal akapiga ukelele kama mwenda wazimu na kuwaita jamaa zake.

 

"He! Amma leo Muhammad ametia fora"

 

Akaanza kuwahadithia yale aliyoyasikia kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), jambo lililowafanya hata baadhi ya waliosilimu karibuni wastushwe na habari hizo na kurudi nyuma kidogo.

 

Washirikina wa Kiquraysh wakaona kuwa leo ndiyo siku ya kumfedhehesha Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtenganisha na sahibu yake Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), wakaanza kusemezana;

 

"Abu Bakr anajua kuwa inachukua miezi mingi kusafiri kutoka Makkah hadi Sham, mahali ulipo msikiti huo wa Baytul Maqdis, maana kesha safiri kwenda huko mara nyingi, na leo Muhammad anasema eti amesafiri hadi huko ndani usiku mmoja tu"

 

Wakenda mpaka nyumbani kwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kumgongea mlango huku wakimwita kwa sauti kubwa: "Abu Bakr!",

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akauliza: " Kuna nini tena?"

 

Maquraysh: "Rafiki yako Muhammad …"

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Amefikiwa na jambo lolote?"

 

Maquraysh:" "Eti anasema kuwa amesafiri usiku wa leo kutoka Makkah hadi Baytul Maqdis na kurudi."

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Ni yeye Mwenyewe aliyesema hayo?"

 

Maquraysh: " Ndiyo! Tena tumemsikia kwa masikio yetu!"

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Ikiwa Yeye Mwenyewe amesema hivyo, basi mimi namsadiki. Mimi namsadiki kwa mambo makubwa kupita hayo. Nasadiki kuwa anapata Wahyi unaotoka mbinguni, basi nisimsadiki juu ya kwenda hapo Baytul Maqdis?"

 

Hii ndiyo Imani ya Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambayo ikiwekwa upande mmoja wa mizani na zikiwekwa Imani za watu wote upande wa pili, basi imani ya Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) itazidi uzito.

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akavaa nguo zake, akatoka na kwenda kumtafuta Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliyemkuta amekaa kimya peke yake nje ya Al-Kaabah, akamsogelea na kumkabili, kisha kwa utulivu na khushuu akamkumbatia na kumwambia;

 

"Wa-Allaahi wewe husemi uwongo na mimi nakusadiki, Wa-Allaahi nakusadiki."

 

 

Share