'Aqiydah (Itikadi ) Ya (Maimaam) Ar-Raaziy Wawili

‘Aqiydah (Itikadi) Ya (Maimaam) Ar-Raaziy Wawili

 

(Matni Inayozungumzia Asili (Msingi) Wa Sunnah Na Itikadi Ya Dini)

 

Imaam Abuu Zur’ah (Aliyefariki 264 H)

Na

Imaam Abuu Haatim (Aliyekufa 277 H)

 

Imefasiriwa Na: Abu Nawwaaf

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Hii ni itikadi ya (Maimaam) Ar-Raaziy wawili, Imaam Abuu Zur’ah (aliyekufa mwaka wa 264H) na Imaam Abuu Haatim (aliyekufa mwaka wa 277H), (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) wawili; imesimuliwa na Imaam Abuu Haatim Ar-Raaziy (Radhwiya Allaahu ‘anhu)

 

 

 ‘Aqiydah yenyewe: Amesema Imaam Abuu Muhammad ‘Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim: “Nilimuuliza baba yangu na (nilimuuliza pia) Abuu Zur’ah (Rahimahuma-Allaah) kuhusiana na madhehebu ya Ahlus-Sunnah katika misingi ya Dini, na yale ambayo wamewadiriki (wamewakuta) ‘Ulamaa katika miji yote na yale ambayo wanayaitakidi (wawili hao) katika hiyo misingi. Wakasema:

 

 

“Tuliwadiriki 'Ulamaa katika miji yote; katika miji ya Hijaaz, ‘Iraaq, Misri, Shaam, na Yemen. Ikawa miongoni mwa madhehebu zao ni kuwa: 

 

 

1. Iymaan ni maneno na vitendo; inaongezeka na inapungua.

 

 

2. Na Qur-aan ni maneno ya Allaah; haijaumbwa kwa namna yoyote ile.

 

 

3. Na Qadar, kheri na shari yake, (vyote) vyatoka kwa Allaah (‘Azza wa Jalla).

 

 

4. Na walio bora katika ummah huu baada ya Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Abuu Bakr Asw-Swiddiyq, kisha ‘Umar bin Al-Khattwaab, kisha ‘Uthmaan bin ‘Affaan, kisha ‘Aliy bin Abi Twaalib; (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Na hao ndio Makhalifa waongofu wenye kuongoza.

 

 

5. Na kuwa wale (Swahaba) kumi ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwataja, na akawashuhudilia wao Jannah (Pepo), (Nasi pia tunashuhudia) juu ya yale ambayo aliyoyashuhudilia kwayo (Nabiy), na maneno yake (Nabiy) ni ya haki (kweli).

 

 

6. Na kuwatakia rahmah (za Allaah) Swahaba wote wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); Na kujizuia juu ya yale yaliyoleta ugomvi (mzozo) baina yao.

 

 

7. Na kwamba Allaah (‘Azza wa Jalla), yuko juu ya ‘Arsh Yake, hali ya kuwa amejitenga na uumbaji Wake; kama Alivyoisifia nafsi Yake mwenyewe katika Kitabu Chake na kwa kupitia ulimi wa Nabiy Wake; bila ya kuuliza (huo uwepo au ukaaji wake katika ‘Arsh) ukoje.

 

 

8. Amekizunguka kila kitu kwa elimu. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

أَلَا إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُّحِيطٌ﴿٥٤﴾

Tanabahi! Hakika Yeye kwa kila kitu ni Mwenye kukizunguka kwa ujuzi Wake [Fusw-Swilat: 54]

 

 

 

9. Na kwamba Allaah, Azza wa Jalla, Ataonekana Aakhirah. Watu wa Peponi watamuona Yeye kwa macho yao.

 

 

10. Na watasikia maneno Yake vile Anavyotaka Yeye (Allaah) na kama Anavyotaka.

 

 

 

11. Na Jannah na Moto ni kweli (vipo). Navyo viwili hivyo (Jannah na Moto) vimeumbwa, havitokuwa ni vyenye kuisha (vitadumu). Jannah ni malipo kwa vipenzi vyake (Allaah) na Moto ni adhabu kwa watu wenye kumuasi Yeye; ila wale ambao (Allaah) Atawarehemu.

 

 

 

12. Na Swiraatw ni haki (ipo).

 

 

 

13. Na Miyzaan yenye pande mbili, kwa Miyzaan hii matendo ya waja yatapimwa, mazuri yao (waliyoyafanya) na mabaya yao (waliyoyafanya), ni kweli (ipo).

 

 

 

14. Na hawdh (birika) ambalo kwalo Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amepewa heshima, ni kweli (lipo).

 

 

 

15. Na Ash-Shafa’ah (uombezi) ni kweli (utakuwepo). Na kwamba watu wa Tawhiyd (wenye kumpwekesha Allaah) watatoka katika Moto kwa Ash-Shafa’ah (uombezi wa Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni kweli.

 

 

 

16. Na adhabu ya kaburini, ni kweli (ipo).

 

 

 

17. Na Munkar na Nakiyr (Malaika wawili wenye kutoa adhabu kaburini), ni kweli (wapo).

 

 

 

18. Na Malaika watukufu waandishi (wa matendo ya waja), ni kweli (wapo).

 

 

 

19. Na ufufuo baada ya kufa ni kweli.

 

 

 

20. Na watu wenye madhambi makubwa wako chini ya matakwa (mashiy-ah) ya Allaah (‘Azza wa Jalla). Hatuwakufurishi watu wa Qiblah (Waislamu) kutokana na madhambi yao; na tunayaacha mambo yao ya siri (wayafanyayo) kwa Allaah (‘Azza wa Jalla).

 

 

 

21. Na tunasimamisha (tunaamini) fardhi ya Jihaad pamoja na Hjjah chini ya viongozi wa Waislamu, katika kila zama.

 

 

 

22. Wala hatuoni sisi kutoka (kuasi) juu ya viongozi wetu, wala kupigana katika fitnah (machafuko ya Waislam kwa Waislam). Na tunasikiliza na tunatii yule ambaye Allaah (‘Azza wa Jalla) amempa majukumu ya kutuongoza katika mambo yetu; Wala hatuondoshi mkono (wa utiifu) kutoka katika twaa (utiifu) ya Kiongozi.

 

 

 

23. Tunafuata Sunnah na Jamaa’ah, na tunajiepusha na kujitenga na Jamaa’ah, na kugawanyika (katika makundi), na kufarakana.

 

 

 

24. Na Kwamba Jihaad ni ya kale, tangu Allaah (‘Azza wa Jalla) Alipomleta Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (na ni yenye kuendelea) mpaka Qiyaamah itakaposimama, pamoja na wale ambao wana mamlaka juu yetu katika Viongozi wa Waislamu, hakuna chenye kuibatilisha (Jihaad itapiganwa chini ya mtawala wa Kiislamu). Vivyo hivyo kwa Hijjah.

 

 

 

25. Na kutoa Swadaqah (Zakaah) kutokana na vyenye kutakikana kutolewa Zakaah, kuwapelekea walio na mamlaka katika Viongozi wa Waislam.

 

 

 

26. Na watu ni Waumini katika hukumu zao na urithi wao; wala hawajui mambo yao mbele ya Allaah (‘Azza wa Jalla). Yule atakayesema kuwa yeye ni Muumin wa kweli (kisawa sawa), yeye ni mzushi. Na mwenye kusema kwamba yeye ni Muumini mbele ya Allaah, basi yeye ni katika waongo. Na mwenye kusema: “Mimi ni mwenye kumuamini Allaah,” basi huyo yuko sawa (kapatia).

 

 

 

27. Na Murji-ah[1] ni wazushi na wapotevu.

 

 

 

28. Na Qadariyyah[2] ni wazushi (na) wapotevu. Na mwenye kupinga miongoni mwao kwamba Allaah anayajua yale yatakayokuwa (yatakayotokea) kabla ya kutokea kwake, basi huyo ni kafiri.

 

 

 

29. Na kwamba Jahmiyah[3] ni makafiri.

 

 

 

30. Na Maraafidhah (Mashia), wameukataa Uislamu.

 

 

 

31. Na Khawaarij[4] wametoka (katika Uislam).

 

 

 

32. Na mwenye kudai kuwa Qur-aan ni kiumbe, basi yeye amekufuru, ukafiri unaomtoa katika mila (Dini ya Uislam). Na mwenye kutilia shaka ukafiri wa mtu huyu, miongoni mwa wanaolifahamu hili, basi naye ni kafiri.

 

 

 

33. Na mwenye kuwa na shaka katika maneno ya Allaah, na akasimama katika hayo maneno hali ya kuwa ni mwenye shaka; Akasema: Sijui, yameumbwa au hayakuumbwa, basi huyo ni Jahmiy (kafiri); Na mwenye kusimama juu ya Qur-aan kwa ujinga (kutoijua), atafundishwa, ataingizwa katika bid’ah (kwa kutokujua kwake), na hatokufurishwa.

 

 

 

34. Na mwenye kusema: Matamshi yangu ya Qur-aan ni yenye kuumbwa, au, Qur-aan kwa lafdhi (matamshi) yangu ni yenye kuumbwa, basi huyo ataingia katika kundi la Jahmiy.

  

 

Amesema Abuu Muhammad, naye ni ‘Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim: “Nimemsikia baba yangu (Allaah Awe radhi naye) akisema: “Alama za watu wa bid’ah (wazushi katika dini): Ni kuwatukana watu wa athar (watu wa Sunnah).”

 

 

Na alama za wazandiki (waharibifu wa dini): Ni kuwaita Ahlul-Aathaar (watu wa Sunnah) kuwa wao ni Hashwiyyah (watu wasio na maana au elimu na wanaochukua ufahamu juu juu), wanakusudia kuzipinga athar (Hadiyth).

 

 

Na alama za Jahmiyyah: Ni kuwaita kwao watu wa Sunnah (Ahlus-Sunnah) kuwa ni mushabbihah (wanaomfananisha Allaah na viumbe Vyake).

 

 

Na alama za Qadariyyah: Ni kuwaita kwao Ahlus Sunnah (watu wa Sunnah) kuwa wao ni mujbirah (wanaosema kuwa ayafanyayo mtu katika matendo si kwa khiyari yake).

 

 

Na alama za Murji-ah: Ni kuwaita kwao Ahlus Sunnah kuwa wao ni wapinzani (mukhaalifah) na ni naqswaaniyyah (watu wanaosema kuwa Iymaan hupungua).

 

Na alama za Raafidhwah (Mashia): Ni kuwaita kwao Ahlus-Sunnah kuwa wao ni Naasibah (watu wanaowachukia watu wa nyumba ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (Ahlul-Bayt).

 

 

Na hakuna jina linalowafaa Ahlus-Sunnah isipokuwa jina moja, na haiwezekani kuwakusanyia majina yote haya.”

 

 

Amesema Abuu Muhammad: “Nimemsikia baba yangu na Abuu Zur’ah wakiamrisha kuwahama watu wazushi na wapotevu, na kuwa wakali katika hilo, na kupinga kutunga vitabu kwa rai pasi naathari (Hadiyth).

 

 

Na wanakataza (wawili hao) kukaa na watu wa kalaam (watu wa falsafa), na kuvisoma vitabu vya watu wa kalaam. Na wanasema (wawili hao), Katu, hawatofaulu watu wa kalaam (wanafalsafa) kamwe.

 

 

Na Himdu zote anastahiki Allaah, Rabb wa viumbe wote, na Swalaah na salaam ziwe juu ya bwana wetu Muhammad na Aali zake.”

 

 

Amesema Abuu Muhammad: “Zingatia ninayoyasema.”[5]

 

 

 

 

[1] Murji-ah: Ni pote linaloitakidi kuwa iymaan ni moyoni na kuitamka tu, na haithibitishwi kwa matendo.

 

[2] Qadariyyah: Ni kundi linalopinga Qadar (nguzo ya sita ya iymaan ya Kiislamu).

 

[3]  Jahmiy: Ni mfuasi wa Jahm bin Safwaan; miongoni mwa itikadi zao potofu ni kuwa Qur-aan imeumbwa. Na huu ni ukafiri wa wazi.

 

[4]  Khawaarij: Waliomuua ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Khalifa wa tatu wa Uislamu na wakajitenga na kundi la ‘Aliy na Mu’awiyyah. Miongoni mwa itikadi zao ni kuwa madhambi makubwa yanamdumisha mtu motoni, na kwamba Qur-aan imeumbwa.

 

[5] Imepokelewa na Imaam Al-Laalikaaiy katika Sharh Uswuwl I’tiqaad Ahlis-Sunnah wal Jama’ah (276/1, namba 321) kwa ukamilifu wake, na Imaam Abuu A’laa Al-Hamdaaniy katika Fataawa fiy Dhikril I’tiqaad (uk. 90, namba 30), na Imaam Ibn Qudaamah katika Ithbaatul ‘Uluww (uk. 125, namba 110), na ametaja Imaam Naswr Al-Maqdisiy katika Mukhtaswar Kitaabil Hujjat ‘Alaa Taariki Al-Mahajjah (618/2,  namba 376), na Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah katika Bayaan Talbiysil Jahmiyyah (40-41/2) na katika Dur’u Ta’aaridh An-Naql wa Al-‘Aql (257/2) na katika Majmuw’ Al-Fataawa (222/3), na Imaam Ibn Qayyim Al-Jawziy katika Ijtimaa’ul Juyuushil Islaamiyyah (uk. 233) na katika Asw-Swawaa’iqul Mursalah (1291/4), na Imaam Adh-Dhahabiy katika Al-’Uluw lil ’Aliyyi Al-‘Adhwiym (466), na katika Siyar A’alaam An-Nubalaa (84/13), nayo ni sahihi yenye kuthibiti kutoka kwa hao wawili kama ilivyo katika Mukhtaswar Al-‘Uluww (204) Imaam Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy (Allaah Awarehemu wote).

 

 

Share