Hizbut-Tahriyr

Hizbut-Tahriyr

 

Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah)

 

Imetarjumiwa Na: Abuu Suhayl

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

 

 

“Shukrani njema zinamsathiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Tunamshukuru, tunataka msaada kwake na msamaha, tunataka hifadhi kwa Allaah Aliyetukuka kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu mabaya. Aliyemuongoa Allaah hakuna wa kumpoteza na Aliyempoteza hakuna wa kumuongoa. Nashuhudia kuwa hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah peke Yake asiye na mshirika wala msaidizi. Na nashuhudia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja wake na Rasuli Wake wa ukweli.

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٢﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi (mmeshakuwa) ni Waislamu. [Aal ‘Imraan: 102].

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١﴾

Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwachunga daima. [An-Nisaa: 1].

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli nyofu ya haki. Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu. [Al-Ahzaab: 70 -  71].

 

 

Ama baada ya hayo;

Hakika mazungumzo bora ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na bora ya uongofu ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na shari ya mambo ni ni yale yaliyozushwa, kila lililozushwa ni ni bida’a, na kila bida’a ni upotofu na kila upotofu ni motoni

 

 

Mbele yangu nina maswali mawili ambayo yote yamezunguka juu ya nukta moja, ambayo ni kuhusu Hizbut-Tahriyr.

 

 

Swali la kwanza linasema: Nimesoma sana kuhusu Hizbut-Tahriyr na mawazo yao mengi yamenivutia. Hivyo ningependa utueleze au utupe mukhtasari kuhusu Hizbut-Tahriyr.

 

 

Swali la pili linazungumzia kuhusu mada hiyo hiyo lakini alitaka maelezo zaidi anasema, Tungependa tupate maelezo ya kina toka kwako kuhusu Hizbut-Tahriyr malengo yake, mtazamo wao, makosa yao na kama makosa yao yamechupa mipaka na kusababisha uharibifu wa ‘Aqiydah.

 

 

Katika kujibu maswali haya mawili nasema, kundi  lolote na simaanishi Hizbut-Tahriyr  peke yao na kuyaacha makundi mengine au harakati nyingine au vijikundi vyengine – kundi lolote kati ya haya ambayo haya kuanzishwa kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah (Qur-aan) na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na pamoja na hivi vyanzo viwili nasema na njia ya wema waliotangulia… kundi lolote ambalo halikuanzishwa kwa mujibu wa Kitabu na Sunnah kwa ufahamu/njia ya wema waliotangulia bila shaka matokeo ya harakati zake yatakuwa ni khasara.

 

 

Hata kama watakuwa na ikhlaasw ya kiasi na namna gani katika Da’wah yao… na utafiti na majibu yangu yanahusu makundi haya ya Kiislamu ambayo yanaonekana kuwa na ikhlaasw katika Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na kuwa na ikhlaasw katika kuunasihi Ummah kama ilivyokuja katika Hadiyth sahihi ambayo inasema:

 

“Dini ni nasaha, Dini ni nasaha, Dini ni nasaha.” Swahaba wakasema: “Kwa ajili ya nani ee Rasuli wa Allaah?” Akasema “Kwa ajili ya Allaah, Kitabu Chake na viongozi wao na Waislamu wote.” [Muslim 205].

 

Kwa hiyo inapokuwa Da’wah ya yeyote katika haya makundi inapokuwa haipo katika Kitabu na Sunnah katika ufahamu wa wema waliotangulia, haiwezi kuzaa matunda yoyote isipokuwa khasara katika Da’wah yake. Hii ni kwa sababu Mola wetu amesema katika Qur-aani:

 

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا  

Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. [Al-‘Ankabuwt: 69].

 

 

 

Kwa hiyo yeyote atakayefanya jitihada kwa ajili ya Allaah na akawa anafuata Kitabu na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika ufahamu wa wema waliotangulia, hawa ndio wale ambao wanahusika na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ﴿٧﴾

Enyi mloamini! Mkisaidia kunusuru Dini ya Allaah, (Allaah) Atakunusuruni. [Muhammad: 7].

 

 

Narudia tena msingi huu mkuu ambao kilakundi katika Waislamu wanatakiwa walinganie kwa kuuzingatia; Kitabu, Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia.

 

 

Kwa hiyo jambo likiwa ni kama hivyo, nasema kwa kuzingatia  ujuzi wangu wa makundi yote na Madh-hab yote yaliyoanzishwa katika uso wa dunia ya Waislamu hivi sasa, nazungumzia makundi yote isipokuwa kundi moja, na sisemi (isipokuwa) Madh-hab moja kwa kuwa hili kundi halikugawanyika katika vikundi wala halikufanya muungano, wala uchama au kung’ang’ania makundi  isipokuwa kwa kuzingatia misingi tuliokwisha kuitaja ambayo ni Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ufahamu wa wema waliotangulia.

 

 

Najua vizuri kwamba hakuna yeyote zaidi ya kundi hili (la Ahlus-Sunnah Wal-Jama’aah) ambalo linalingania katika misingi hiii tuliyoielezea na ambayo nimerudia mara nyingi sana tena na tena kwenu ninyi. Zaidi (hayo makundi) mengine yanalingania watu warejee katika Kitabu na Sunnah tu, na hawamalizii neno letu tulililolitaja ambalo ni katika ufahamu na njia ya wema waliotangulia.

 

 

Kwa wakati huu umuhimu wa huu msingi wa tatu ‘katika ufahamu/njia ya wema waliotangulia’ utaeleweka vizuri kwenu, utaeleweka vizuri kwenu kutokana na ukweli wa hali halisi ya makundi haya, au Madh-hab haya tokea walipochipukia waanzilishi wake, au yalipoota pembe katika makundi ya mwanzo, tokea siku Makhawaarij walipotoka chini ya twa’a ya ‘Aliy bin Abi Twaalib, na tokea zama za Ja’ad aliyelingania wito wa Mu’utazilah na waliokuja baada yake wakimfuata katika I’itizaali na makundi mengine ambayo yalikuwa maarufu huko nyuma na mengine ambayo yanachipuka sasa kwa majina tofauti.

 

 

Makundi yote haya ya mwanzo na ya sasa, hakuna hata kundi moja kati yao linaloweza kupatikana ambalo linasema na kutangaza kuwa: “Hatufuati Kitabu na Sunnah.” Makundi yote kwa bila kuzingatia tofauti zao, ziwe ni katika ‘Aqiydah, misingi au katika mambo ya hukumu au katika mambo ya furu’i, wote hao ambao wamegawanyika katika Dini yao wanasema kama tunavyosema “Kitabu na Sunnah” lakini wanakhitilafiana nasi kwa kuwa hawatamki msemo wetu ambao ndio unaomalizia ulinganizi wetu: ‘…katika ufahamu/njia ya wema waliotangulia.”

 

 

Kitu gani kitakachoamua basi kati ya haya makundi wakati makundi yote yanadai katika Da’wah yao na matamshi yao kuwa wanafuata Kitabu na Sunnah? Kitu gani ambacho kitaamua kati ya makundi yote haya wenye madai sawa?

 

Jibu ni: “Kaatika ufahamu/njia ya wema waliotangulia.”

 

 

Kama wanavyosema sasa, swali linajitokea kuhusu baadhi ya watu nalo ni wapi wanapopata nyongeza hii: “Kwa ufahamu wa wema waliotangulia?”  Tunapata ziada hii katika Kitabu cha Allaah na kutoka katika Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na toka kwa Maimaam wema waliotangulia wa Ummah wa Ahlus-Sunnah Wal-Jama’aah.

Ushahidi wa kwanza ni maneno yake Allaah:

 

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿١١٥﴾

Na atakayempinga Rasuli baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini; Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Jahannam. Na uovu ulioje mahali pa kuishia [An-Nisaa: 115].

 

Mmesikia maneno yake Allaah katika Aayah hii:

 

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ

 

“Na atakayempinga Rasuli …”  Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) asingetaja 

 

وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ

“na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini” 

 

Kama Aayah ingekuwa “na yeyote atakayempinga Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kubainikiwa na uongofu tutamuelekeza anapoelekea na tutamuingiza Jahannam na ni marejeo mabaya kiasi gani? Da’wah ya yale makundi ya zamani na ya sasa wangekuwa hawajapoteza kitu kama hii sentensi katika maneno yake Allaah aliyetukuka 

 

وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ

“na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini”

 

 isingelikuweko. Kwani wenyewe wanasema ‘tupo katika kufuata Kitabu na Sunnah’ ni wajibu kufuata kwanza msemo huu kwa kufuata Kitabu na Sunnah kwa ukamilifu na pili kuutekeleza kwa vitendo.

  

 

Kwa mfano maneno yake Allaah ambayo yanafahamika sana na 'Ulamaa

 

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ .. ﴿٥٩﴾

 

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho.” [An-Nisaa: 59].

 

 

Wanaofuata kichwamchunga katika dunia ya Uislamu wanapoitwa katika Kitabu cha Allaah na Hadiyth za Rasuli Wake husema: “Hapana sisi tunafuta Madh-hab yetu.” Mmoja atasema: “Madh-hab yangu ni Hanafiy” na mwengine atasema: “Madh-habu yangu ni Shafi’iy” na kadhalika.

 

 

Je, hawa watu ambao wamejiwekea utaratibu wa kufuata kichwamchunga Maimaam wao mahali pa kufuata Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wameshaitekeleza hii Aayah niliyoitaja hapa, 

 

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ

“Na mkizozana katika jambo lirudisheni kwa Allaah na Rasuli Wake?”

 

 

Jibu ni kuwa, hawajatekeleza chochote katika hiyo Aayah hivyo kusema kuwa, “Tunafuata Kitabu na Sunnah” hakujawanufaisha chochote kwa kuwa hawatekelezi kwa vitendo Kitabu na Sunnah. Huu ni mfano ambao nimetaka niufafanue kwanza kwa kuwa ninazungumzia kufuata kichwamchunga kupitia mfano huu.

 

 

Ama kuhusu mjadala wetu wa mwanzo nilikusudia ma-Du’aat wa Kiislamu ambao wao si katika wanaofuata kichwamchunga, katika wale ambao wanatanguliza kauli za Maimaam ambao hawakuhifadhiwa na makosa juu ya maneno ya Allaah na Rasuli Wake ambaye amehifadhiwa. Hivyo kama jambo, litakuwa ni linalohusu ‘Aqiydah, ’Aqiydah inachukuliwa toka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah na yale ambayo wema waliotangulia (Salaf) walikuwa wakifuata, kwa kuwa Salaf ndio waliotajwa katika Aayah ya mwanzo: 

 

 

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿١١٥﴾

Na atakayempinga Rasuli baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini; Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Jahannam. Na uovu ulioje mahali pa kuishia.  [An-Nisaa 4: 115].

 

وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ

“Na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini.” 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Hakutaja maneno haya katikati ya Aayah hii hivi hivi tu, lakini ni kuifanya kuwa kanuni madhubuti kwayo, na kuweka msingi kwayo ambao ni katika kuelewa Kitabu cha Rabb wetu na Sunnah za Nabiy wetu hairuhusiwi kutumia akili zetu ambazo zimekuja mbeleni (baada ya Salaf) na ambazo zinatofautiana na ufahamu wa Salaf.

 

 

Muislamu atakuwa anafuata Kitabu na Sunnah katika kanuni na misingi watakapoongeza katika Kitabu na Sunnah ‘kwa ufahamu wa wema waliotangulia’ hii ni kwasababu mpangilio wa Aayah hii umeonyesha kuwa hatutakiwi kumpinga Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kufuata njia nyingine isiyokuwa ya Waumini. Hivyo sharti la mwanzo na la pili zilizotajwa katika Aayah hii zinamaanisha kwamba ni wajibu kwetu sisi kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kujiepusha na kumpinga kama ambavyo ni wajibu kwetu sisi kufuata njia ya Waumini na si kuwapinga.

 

 

Kwa kuzingatia Aayah tunasema: Ni juu ya kila kundi au Madh-hab kusahihisha misingi ya uanzishwaji wake kwa kutegemea Kitabu na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia. Hizbut-Tahriyr hawafuati shart hili kama sehemu ya fikra zake wala Ikhwaan Al-Muslimiyn wala makundi mengine kama wao. Na hapa tunakusudia makundi ya Kiislamu tu, kwa yale makundi ambayo yametangaza vita dhidi ya Uislamu kama Ba’ath na wakomunisti, hatuwazungumzii wao kwa sasa.

 

 

Kwa hiyo nukta ya msingi ni hii kanuni ya tatu kufuata njia ya Waumini, Hizbut-Tahriyr hawaifuati wala makundi mengine.

 

 

Jambo linapokuwa kama hivyo, ni lazima kila Muislamu mwanaume na mwanamke kujua kuwa njia inapopinda kuanzia mwanzo, inavyozidi kuendelea itaendelea kupinda na kuachana na njia iliyonyooka; njia ilinyooka ambayo Rabb wa ulimwengu wote Amesema katika Qur-aan:

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153].

 

 

Aayah hii inajieleze wazi na haina maana mbili kama Hizbut-Tahriyr, kutoka katika miongoni mwa mapote ya Kiislamu, wanavyosema daima katika Da’wah zao, vitabu na mihadhara yao ‘Aayah hii ina maana mbili.’

 

 

Hii ni kwasababu Aayah inasema njia inayoelekea kwa Allaah ni moja na njia zilizobaki zitamuweka mbali na njia ya Allaah: 

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ 

 

“Na kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia (nyinginezo) zitakufarikisheni na Njia Yake.” 

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  aliielezea na kuifafanua zaidi Aayah hii kama njia yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku zote na milele kama ambavyo Allaah ‘Azza wa Jalla Alivyotaja ndani ya Qur-aan tukufu:

 

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ﴿٤٤﴾

Na Tumekuteremshia Ukumbusho (Qur-aan) ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao huenda wakapata kutafakari. [An-Nahl: 44].

 

 

Kwa hiyo Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni maelezo yaliyokamilika kuhusu Qur-aan.

 

 

Qur-aan ndio mzizi/msingi, ndio mwongozo wa Muislamu, na Sunnah ndio inayofafanua na kuisisitiza. Pasina ya kulinganisha lakini katika namna ya kuelezea (ninachokusudia) katika mizani ya kidunia Qur-aan ni kama mwongozo na Sunnah ni kama sheria zinazoifafanua mwongozo.

 

 

Kutokana na sababu hiyo Waislamu wote wanakubaliana kuwa haiwezekani kuielewa Qur-aan pasina ufafanuzi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hili ni jambo ambalo limekubaliwa kwa kauli moja. Lakini kitu ambacho Waislamu wanatofautiana na ambacho makundi yote potofu ya zamani na ya sasa hayajazingatia msingi wa tatu ‘Ufahamu wa wema waliotangulia’ na kwa kufanya hivyo wanaipinga Aayah ambayo nimekwishaitaja tena na tena.  Baada ya hapo wanaipinga njia ya Allaah, kwa kuwa njia ya Allaah ni moja na ndiyo iliyotajwa katika Aayah iliyopita: 

 

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153].

 

 

Ninasema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliifafanua zaidi Aayah hii kiasi Swahaba wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehadithia; Swahaba aliyekuwa akifahamika kwa elimu yake. Abdullaah bin Mas’uwd aliposema: Siku moja (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichora mstari ulionyooka kisha akachora vijistari vidogo kuuzunguka, kisha akanyoosha kidole chake kitukufu kwenye mstari ulionyooka.

 

 

Kisha akasoma Aayah hii: 

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153].

 

 

Alisema hali ya kuwa anapitisha kidole juu ya mstari ulionyooka “Hii ndio njia ya Allaah” kisha akasema hali ya kuwa ananyoosha kidole chake kwenye vijistari vifupi “Hizi ndio njia (nyingine) katika kila kichwa cha njia (kileleni mwake) kuna shaytwaan anayewaita watu kuielekea. Hadiyth hii pia inaielezea Hadiyth nyingine (ambayo nitaitaja).

 

 

Hadiyth hii nyingine pamoja na hiyo ya njia ilinyooka ndio huchukuliwa kuwa zimeifasiri Aayah kuhusu njia ya Waumini. Nayo ni ile Hadiyth ambayo kundi la wapokezi kama Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy na wengine katika Maimaam wa Hadiyth toka katika kundi la Swahaba kama Abu Hurayrah, Mu’aawiyah, Anas bin Maalik na wengineo kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

“Mayahudi waligawanyika makundi sabini na moja, na Wakristo waligawanyika makundi sabini na mbili na Ummah wangu utagawanyika katika makundi sabini na tatu. Makundi yote yataingia motoni isipokuwa moja. Wakasema: “Akina nani ee Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Watakaokuwa katika yale niliyokuwa nayo mimi na Swahaba zangu.”

 

 

Hadiyth hii inatufafanulia njia ya Waumini iliyotajwa katika Aayah hapo mwanzo. Waumini wapi waliokusudiwa? Ni wale ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewataja katika Hadiyth ya makundi alipoulizwa kuhusu kundi litakalookoka, njia yake, sifa zake, na mwanzo wake, alisema:

 

“Ni lile litakalokuwa katika yale niliyokuwa nayo mimi na Swahaba zangu.”

 

“Ni lile litakalokuwa katika yale niliyokuwa nayo mimi na Swahaba zangu.” nataka muwe makini, kwa kuwa jibu la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  kama  si wahyi toka kwa Allaah itakuwa ni ufafanuzi wa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu ‘njia ya Waumini’ iliyotajwa katika maneno ya Allaah, ambayo nimekutajieni mara nyingi muda si mrefu.

 

 

Ambapo Allaah amemtaja Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Aayah na pia akaitaja njia ya Waumini. Hivyo hivyo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatafautisha kundi litakalookoka ambalo haliko katika makundi sabini na mbili yaliyopotea, akaonyesha alama yake kuwa ni: ‘litakuwa katika yale Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyokuwa nayo na Swahaba.’

 

 

Hivyo tunakuta katika Hadiyth hii yale tuliyoyakuta katika Aayah. Kama ambavyo Aayah haikuishia kumtaja Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake vilevile Hadiyth haikuishia kumtaja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake, bali Aayah imetaja njia ya Waumini na vivyo hivyo Hadiyth imewataja Swahaba wa Rasuli mtukufu, hivyo Hadiyth imeafikiana barabara na Qur-aan. Hii ndiyo sababu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

“Nimewaachieni vitu viwili, hamtopotea kamwe mtakapokuwa mmeshikamana navyo: Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu, havitatengangana kamwe mpaka vitakapokuja kwangu katika Hawdh.”

 

 

Makundi mengi za zamani na ya sasa hayazingatii sharti zilizotajwa katika Aayah wala Hadiyth hii kuhusu makundi sabini na tatu. Ambapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alielezea sifa za kundi litakalookoka, na tofauti ya kundi litakalookoka ni kuwa litakuwa katika yale aliyokuwa nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba.

 

 

Hadiyth inayolingana na hiyo kidogo ni Hadiyth ya Al-‘Irbaadh bin Saariyah, naye ni katika Swahaba wa Rasuli wa Allaah, katika watu wa Suffaa, ambaye alikuwa maskini ambao siku zote walikuwa Msikitini, siku zote yupo katika darsa za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye alikuwa akichukua elimu toka Kitabu cha Allaah na toka mdomoni mwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  moja kwa moja. Al-‘Irbaadh amesema:

 

“Alituwaidhia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mawaidha yaliyozifanya nyoyo kuingia khofu na macho yakatokwa na machozi. Tukamwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Yaonyesha kama haya ni mawaidha ya kuaga, basi tuusie.” Akasema: “Nawausia kumcha Allaah, Kwani hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni kufuata Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa walioongoka, yashikeni kwa magego mambo yao. Jiepusheni na mambo ya kuzua, kwani kila yenye kuzuliwa ni bid’ah, na kila bid’ah ni upotevu.” [Abu Daawuwd, Ahmad, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ad-Daarimiy].

 

 

Hakuna katika wanaadamu aliye na hekima kuliko Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa ajili hiyo ndiyo maana akasema “Atakayeishi miongoni mwenu ataona khitilafu nyingi...” Akajibu swali la msingi (ambalo linafuatia katika sentensi hiyo) ambalo ni tufanye nini ee Rasuli wa Allaah, akasema: “Jilazimisheni na Sunnah zangu…” Lakini hakutosheka na na kuamrisha watakaoishi zama za kutofautiana kama zama zetu, hakuridhika na msemo wake: “Jilazimisheni na Sunnah zangu...” tu aliongeza juu ya msemo huo: “Na Sunnah za Makhalifa wangu waongofu…”

 

 

Hivyo, Muislamu muadilifu aongeze katika ‘Aqiydah yake (sharti hili) kwamba ni lazima kurejea katika Kitabu cha Allaah, Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na njia ya wema waliotangulia. Ushahidi juu ya hili ni Aayah, Hadiyth kuhusu makundi (73) na Hadiyth ya Al-‘Irbaadh bin Sariyyah. Huu ni msingi ambao kwa masikitiko makubwa makundi yote katika Uislamu hawaujui, hasahasa Hizbut-Tahriyr ambao wamejitafautisha na makundi mengine kwa kuipa akili ya mwanaadamu nafasi kubwa zaidi ya ile iliyopewa na Uislamu. Tunajua kwa uhakika kuwa Allaah Mtukufu Anapozungumza na watu huwa Anazungumza na wale wenye akili, Wanawachuoni, Anazungumza na wale ambao wanafikiri na kutafakari, lakini pia tunajua kuwa ufahamu wa mwanaadamu hutofautiana. Akilli zipo za aina mbili; akili za Kiislamu na akili za kikafiri.

 

 

Hii akili ya makafiri si akili, inaweza kuwa ni werevu, ujanja lakini si akili. Kwa sababu neno akili katika Kiarabu humaanisha kumzuia mtu, kumshikamanisha na kumzuia kwenda kulia au kushoto. Haiwezekani kwa mtu mwenye akili kutoyumba kwenda kushoto au kulia isipokuwa kwa kufuata Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Sunnah za Rasuli wa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwa ajili hiyo Allaah amesema kuwa makafiri na washirikina watakubali ukweli wa hali zao pale walipoelezewa kama alivyosema Allaah katika Qur-aan.

 

يَعْلَمُونَ ظَاهِرًا مِّنَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ عَنِ الْآخِرَةِ هُمْ غَافِلُونَ ﴿٧﴾

Wanajua yaliyo dhahiri ya uhai wa dunia, lakini wao wameghafilika na Aakhirah. [Ar-Ruwm: 7].

 

 

Watakubali kuwa ingawa walikuwa wanajua mambo ya dunia yao lakini hawakuwa na akili (ambacho kinaonekana) katika kauli yao aliyotusimulia Mola wetu:

 

وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١٠﴾

Na watasema: Lau tungelikuwa tunasikiliza au tunatia akilini, tusingelikuwa katika watu wa motoni.  [Al-Mulk: 10].

 

 

Kwa hiyo kuna akili za namna mbili; akili halisi na akili za bandia.

 

 

Akili ya kweli ni ile ya Muislamu aliyemuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama akili ya bandia, ni ile akili ya makafiri. Kwa sababu hiyo Allaah Aliyetukuka Amesema ndani ya Qur-aan kama mlivyosikia:

 

وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١٠﴾

Na watasema: Lau tungelikuwa tunasikiliza au tunatia akilini, tusingelikuwa katika watu wa motoni. [Al-Mulk 67: 10].

Na amesema kuhusu makafiri kwa ujumla, 

 

 لَهُمْ قُلُوبٌ لَّا يَفْقَهُونَ بِهَا ﴿١٧٩﴾

Wana mioyo lakini hawatambui.. [Al-A’araaf:179].

 

 

Kwa hiyo, wana mioyo lakini hawauelewi (ukweli) kupitia mioyo yao, hawautambui ukweli kwa mioyo yao. Tutakapouelewa huu ukweli, ukweli ambao sidhani kama watu wanaweza kutofautiana au mafahali wawili watabishana kwa sababu upo wazi ndani ya Qur-aan na katika Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini nataka kuhama toka ukweli huu kwenda kwenye ukweli mwingine ambao ndiyo nukta ya msingi hasa ninayotaka kuielezea kwa sasa. Kwa kuwa akili au ufahamu wa wa kafiri si akili au ufahamu wa sawa hivyo hivyo akili za Waislamu zipo za aina mbili; akili ya Mwanachuoni na akili ya mjinga. Akili au ufahamu wa Muislamu aliye mjinga haiwezi kuwa sawa na akili ya Mwanachuoni, haziwezi kamwe kuwa sawa zitakapolinganishwa. Ndio maana Allaah aliyetukuka Amesema: 

 

وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ ﴿٤٣﴾

Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu. Lakini hawaifahamu isipokuwa wenye elimu. [Al-‘Ankabuwt: 43].

 

 

Kwa hiyo, haifai kwa Muislamu wa kweli anayemuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kikweli na Rasuli Wake kuipa akili yake mamlaka ya kuhukumu, lakini anatakiwa aifanye akili yake ijisalimishe kwa aliyoyasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Ni kutoka hapa nataka niseme nukta muhimu kuwa Hizbut-Tahriyr waliathiriwa na Mu’tazilah mwanzo wao kabisa katika njia yao ya kuamini, baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na kiongozi wao Taqiyuddin An-Nabahaani Allaah Amghufurie vimepewa jina: ‘Njia ya kuamini’. Nilikutana naye mara kadhaa na namfahamu vizuri sana. Na ninafahamu kwa undani waliyonayo kundi la Hizbut-Tahriyr. Kwa ajili hiyo, ninazungumza kwa ujuzi (kundi ninalolijua vizuri) In Shaa Allaah ambapo Da’wah yao imesimamia. Hivyo hili kosa la kwanza dhidi yao, kuwa wameipa akili nafasi kubwa zaidi ya inavyostahili.

 

 

Narudia kusema niliyoyataja mwanzo, sikatai kwamba akili ina umuhimu kama nilivyotangulia kusema, lakini si kazi ya akili kukihukumu Kitabu na Sunnah bali inatakiwa itumike kuelewa yaliyokuja katika Kitabu na Sunnah. Ni kutoka hapa Mu’utazilah walipotea huko nyuma, walizikataa hukumu nyingi za kishari’ah kwa sababu tu walizipa akili zao nguvu juu ya Kitabu na Sunnah ambapo matokeo yake waliziharibu na kuzibadilisha kama walivyosema Wanachuoni wema waliotangulia, “Waliachana na maandiko ya Kitabu na Sunnah” nataka mzingatie nukta hii: “Inatakiwa akili ya Muislamu ijisalimishe katika maandiko ya Kitabu na Sunnah baada ya kuwa imeelewa Kitabu na Sunnah.”

 

 

Hivyo muamuzi ni (maneno) Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake, (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) si akili ya mwanaadamu kwa sababu tuliyoitaja kwamba akili ya mwanaadamu inatofautiana; akili ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu zinatofautiana, akili za Waislamu zinatofautiana; ile ya mwenye elimu inatofautiana na ile ya mjinga, kwani uelewa wa Mwanachuoni unatofautiana na uelewa wa Muislamu mjinga. Hiyo ndio maana Mola aliyetukuka amesema na hakuna ubaya kurudia (tuliyoyasema mwanzo) kwa sababu najua mada hii mamilioni kwa mamilioni ya Waislamu wanaume hawajaisikia achilia mbali wanawake. Kwa sababu hiyo ninawajibika kurudia nukta hizi na uthibitisho huu: 

 

وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ ﴿٤٣﴾

Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu. Lakini hawaifahamu isipokuwa wenye elimu.” [Al-‘Ankabuwt: 43].

 

 

Tutasimama hapa kwa muda, ni akina nani Wanachuoni? Je, Ni Wanachuoni wa kikafiri? Hapana! Hatuwapi uzito wowote kwa sababu tuliyoitaja kuwa wao hawana akili, ukweli ni kwamba wao ni werevu/wajanja kwa sababu wamevumbua na kuzusha n.k. na wameendelea katika mambo ya kidunia zaidi ya wote (lakini hawana akili). Kadhalika akili au ufahamu wa Waislamu, hii akili kila mmoja anayo na zinatofautiana hivyo ufahamu wa Mwanachuoni si sawa na ufahamu wa mtu wa kawaida.

 

 

Na nitasema kitu kingine, akili ya Mwanachuoni anayetenda kulingana na elimu yake si sawa na akili ya Mwanachuoni ambaye hatendi. Hawawezi kuwa sawa kamwe.

 

 

Kwa sababu hii Mu’tazilah walipotea katika misingi mingi waliyojiwekea ambayo kwayo walipingana na njia za kishari’ah kuhusiana na Kitabu, Sunnah na njia ya wema waliotangulia. Hii ni nukta ya kwanza. Hizbut-Tahriyr kutegemea akili zao zaidi ya ilivyotakiwa. Nukta ya pili ambayo imezalikana kutokana na nukta ya kwanza kwa mtazamo wangu, wameyagawanya maandiko ya Kitabu na Sunnah katika sehemu mbili kutegemeana na upokezi/usimulizi na ushahidi unaotolewa/unaochukuliwa kutokana navyo (Kitabu na Sunnah). Katika upokezi wamesema: inawezekana kuthibitishwa kuwa na maana moja na pia inaweza kuwa na maana iliyojificha; na kwa jinsi hiyo ushahidi unaotoka katika Hadiyth unaweza kuwa na maana ya dhahiri na unaweza kuwa na maana iliyojificha. Hatujadili maneno haya kwa sasa kwani hali ni kama ilivyosemwa, kila watu wanaweza kutumia maneno wanayotaka lakini tunachojadili ni nini kitatokea vitu vingine vinapoongezwa katika maneno haya ambavyo vinapingana na yale waliyokuwa nayo Waislamu wa mwanzo.

 

 

Na kutokana na hili umuhimu wa kufuata njia ya Waumini utakuwa wazi kwenu. Kwa sababu Wanachuoni wa Kiislamu achilia mbali Waislamu wa kawaida, wameamrishwa kutokuyaacha maandiko ya Kitabu na Sunnah kwa kutumia istilahi kama hizi. Matokeo ya maneno  maana ya “dhahiri” na “iliyojificha” kama ni kuhusu mnyororo wa upokezi au maana inayochukuliwa toka katika maandiko yametokea yafutayo, wamesema: “Kama maandiko yakija katika Qur-aan tukufu bila shaka kwa mujibu wa istilahi zilizopita yatachukuliwa katika hukumu yake ya dhahiri,” (wanasema) yakija maandiko katika ambayo hukumu (ujumbe unaofikishwa) yake haiko wazi si wajibu kwa Muislamu kuchukua ujumbe wa Aayah hiyo kwani hiyo ni maana ya ya dhahiri tu (kuna maana iliyojificha), na kwamba haijuzu kwa Muislamu kuchukua mafunzo ya ki’-Aqiydah toka katika Aayah ambayo maana yake ya dhahiri haijathibiti  ila ni maana ya kudhaniya katika yale inayoeleza.” Na vilevile kinyume chake ni sahihi kwao. Kwamba dalili inapokuja ambayo iko wazi katika maana inayofikishwa lakini kuthibiti kwake hakuko wazi (kama wanavyosema) hawawezi kuchukua mafunzo ya ki-’Aqiydah.

 

 

Kutokana na sababu hii ndio wakaja na ‘Aqiydah ambayo haikufahamika na wema waliotangulia. Wakajiwekea istilahi mpya, na vitabu vyao vinafahamika vizuri na ninaposema vitabu vyao nakusudia vitabu vyao vya mwanzo kwani wamevifanyia mabadiliko na mimi ni katika watu ambao ninayajua mabadiliko hayo vizuri sana, lakini kiuhalisia ni mabadiliko ya kimuundo tu. Na hata kama wakikiri (kuwa mabadiliko yamefanyika) hiyo itathibitisha tu wamejichanganya kwenye ‘Aqiydah yao kwani wanasema: “‘Aqiydah haipatikani isipokuwa kwa ushahidi ambao umethibiti wazi na wenye maana iliyo wazi.”

 

 

Kwa hiyo ‘Aqiydah yao imejengwa juu ya msingi huu; kwamba, ‘Aqiydah haichukuliwi kutoka kwenye Hadiyth iliyo na maana iliyo wazi katika matini lakini inatakiwa iwe sahihi katika msururu wa wapokezi wake (hawakubali Hadiyth sahihi kuwa iko wazi hata kama maana ya Hadiyth ipo wazi kabisa).

 

 

Ndio maana huwa tunawauliza katika mijadala yetu na majibizano yetu tuliyokuwa nayo, “Huu msingi mmeupata wapi?” Na huu ni msingi unaohusu ‘Aqiydah nyie mmeupata wapi?  Ushahidi kwamba hairuhusiwi kwa Muislamu kuchukua ‘Aqiydah yake kutoka katika Hadiyth ambayo ni sahihi lakini upokezi wake si Mutawaatir (kama wanavyodai) ambazo ndiyo zinafaa kuchukuliwa ushahidi? Wamepata wapi hili?

 

 

Hakuna ushahidi wa hili si kutoka katika Qur-aan wala katika Sunnah wala toka kwa yale waliyokuwa nayo Salaf. Yale waliyokuwa nayo Salaf yanapingana na yale waliyokuja nayo wa baadaye, toka kwa Mu’utazilah mpaka kwa wafuasi wao wa sasa, Hizbut-Tahriyr.

 

 

Nitataja kitu sasa na pengine nitakitaja kwa haraka ili tuendelee na somo letu. Wote tunajua Allaah Alipomtuma Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama mbashiriaji na muonyaji Alisema: 

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ  ﴿٦٧﴾

Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako.. [Al-Maaidah:67].

 

 

Wote tunajua kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifikisha ujumbe wake yeye mwenyewe ambapo alikuwa akienda katika mabaraza yao na mikutano yao na kuongea nao moja kwa moja. Wakati mwingine alikuwa akituma mjumbe toka upande wake kuwaita washirikina kumfuata katika Dini yake, na wakati mwingine alikuwa akituma barua kama inavyojulikana katika historia ya maisha yake kwa Mfalme Heraclius wa Roma na Kisra Mfalme wa Fursi na kwa machifu wa Waarabu kama yalivyoelezwa katika Siyrah yake.

 

 

Miongoni mwa wajumbe waliotumwa alikuwepo Mu’aadh bin Jabal, Abu Muwsaa Al-Ash’ariy na ‘Aliy bin Abi Twaalib kwenda Yemen, na Dihya al-Kalbiy alitumwa Roma n.k.

 

Hawa wote walitumwa peke yao na ambao upokezi wao hauwakilishi upokezi wa kutegemea (kwa mujibu wa kanuni za Hizbut-Tahriyr) kwa sababu wote walitumwa kila mmoja peke yake. Mu’aadh alikuwa sehemu moja, Abu Muwsaa sehemu nyingine, ‘Aliy sehemu nyingine (upokezi huu si Mutawaatir) na muda unatofautiana kama ambavyo sehemu zinatofautiana.

 

 

Ipo Hadiyth katika sahihi mbili ambayo imepokelewa Kwa usahihi kabisa toka kwa Anas bin Maalik kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mu’aadh kwenda Yemen alimwambia 

“Liwe jambo la kwanza kuwalingania ni La illaaha illa Allaah (kukiri kuwa hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah).”

 

 

Katika Waislamu nani atakayetia shaka kuwa ushahidi huu ni wa nguzo ya kwanza ya Uislamu? Kwamba hii ni nukta ya kwanza ambapo imejengwa juu yake imani juu ya Allaah, na Malaika Wake na vitabu Vyake na Rusuli Wake, hivyo alipokwenda Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwalingania na kuwaita Waislamu, samahani washirikina kuingia katika Dini ya Uislamu… mnafikiriaje?

 

 

Je, huu ni ushahidi kuwa walifikishiwa hoja alipowalingania Mu’aadh bin Jabal kuingia katika Uislamu na kuwaambia kuwa Rasuli wa Allaah amewaamrisha waswali Swalah tano kila siku na kwamba Swalah ya kwanza ina rakaa mbili, na nyingine rakaa tatu na zilizobakia rakaa nne na maelezo mengine tunayoyajua waliLLaahil-Hamd? Na alipowaamrisha kutoa Zakaah akawatajia hukumu za Zakaah, inayohusiana na fedha, dhahabu, inayohusiana na matunda na mboga, inayohusiana na ng’ombe na mbuzi n.k.?

 

 

Je, ushahidi kuhusu Uislamu ulisimamishwa kwa hawa washirikina kupitia Mu’adhi peke yake?

 

 

Kwa mujibu wa Hizbut-Tahriyr, ni kuwa hawa washirikina hawakusimamishiwa hoja kwa kuwa ushahidi ni wa mtu mmoja ambaye kama wanavyosema inawezekana akadanganya, sisi tunasema uongo uko mbali na Swahaba. Kisha kinachowezekana kusema kuwahusu ni kuwa wanaweza kukosea au kusahau

 

 

Wamekuja na falsafa hii: Kuwa, hatuwezi kuchukua ‘Aqiydah toka katika Hadiyth sahihi. Kwa maana hiyo  Mua’adh alipowalingania watu wa Yemen kwenye Uislamu, na bila shaka jambo la kwanza kuwalingania lilikuwa ‘Aqiydah, kwa mujibu wa maneno yao ni kuwa hoja toka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hazikuwafikia watu wa Yemen ambao walikuwa wakiabudu masanamu, wala Wakristo na Majusi -hawakusimamishiwa hoja za Allaah kuhusu ‘Aqiydah.

 

 

Lakini kuhusu hukmu za kishari’ah- Hizbut-Tahriyr wanasema kama wanavyosema Waislamu wengine kwamba hukumu za kishari’ah zinaweza kuchukuliwa toka katika Hadiyth ambayo ni Aahaad lakini mambo yanayohusu ‘Aqiydah hayawezi kuchukuliwa toka katika Hadiyth ambayo ni Aahaad. (Hapa tunaona) Mua’adh akiwakilisha ‘Aqiydah ya Uislamu (kwani alikuwa mwenyewe akilingania katika mambo yote yanayohusu Uislamu Yemen) katika mambo ya kimsingi, mambo ya kifuru’i, ‘Aqiydah na hukumu, sasa ni wapi wamepata hii hukumu?

 

إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ ۚ .. ﴿٢٣﴾

Hayo si chochote isipokuwa ni majina mmeyaita nyinyi na baba zenu, wala Allaah Hakuyateremshia dalili yoyote.. [An-Najm:23].

 

 

Na nitamalizia kwa masimulizi yanayosemwa kuhusiana na msingi waliouanzisha kuhusu Hadiyth Aahaad ambao wanautumia kuzikataa makumi ya Hadiyth sahihi za Rasuli wa Allaah kwa madai yao kwamba ‘Aqiydah haiwezi kuchukuliwa toka katika Hadiyth Aahaad.

 

 

Kuna mtu amehadithia kisa kifuatacho, wanadai kwamba mlinganiaji mmoja wa Hizbut-Tahriyr alikwenda Japan na kufanya darsa na moja ya somo lilikuwa ni “Njia ya Iymaan” na akaelezea katika njia hii kuwa ‘Aqiydah haiwezi kuchukuliwa toka katika Hadiyth Aahaad.

 

 

Alikuwepo kijana mmoja aliyekuwa makini na akili nyepesi akasema kumwambia “Ee mwalimu, umekuja kutulingania hapa Japan nchi ya ukafiri na ushirikina kama ulivyosema ukiwalingania katika Uislamu na unasema, “‘Aqiydah haiwezi kuchukuliwa kupitia Hadiyth Aahaad” na unasema kuwa ni sahihi kutochukua ‘Aqiydah toka kwa mtu mmoja. Sasa wewe unatulingania katika Uislamu na uko peke yako. Mafundisho yako yanatakiwa yazingatie msingi huu, urudi nchini kwako uwachukue watu wengi kama wewe miongoni mwa Waislamu ambao wanaafikiana na unayoyasema hivyo masimulizi yako yatakuwa Mutawaatir na tutachukua ‘Aqiydah toka kwako.

 

 

Hivyo ikawa ni khasara moja kwa moja.

 

 

Huu ni mfano unaoonyesha mwisho mbaya kwa wenye kupingana na njia ya wema waliotangulia.

 

Shaykh Al-Albaaniy akaendelea, “Katika yale ambayo Waislamu tunayajua, na nakusudia hapa kwa wanafunzi, na nategemea hao mabinti wanaosikiliza muhadhara huu ni katika wanafunzi -kwamba katika Swahiyh Al-Bukhaariy katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 “Anapokaa mmoja wenu kwenye tashahhud ya mwisho atake hifadhi kwa Allaah kutokana na mambo manne…”

 

 

Hii ni Hadiyth Aahaad, lakini ni Hadiyth ya aina yake kuhusiana na falsafa ya Hizbut-Tahriyr -kwa sababu upande mmoja inakusanya hukumu ya kishari’ah (hukumu ya kishari’ah ni ile amri ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusoma du’aa hii katika tashahudi ya mwisho katika Swalah na hii amri haihusiani na ‘Aqiydah) na kwa mujibu wa Hizbut-Tahriyr  hukmu ya kishari’ah inaweza kuchukuliwa toka katika Hadiyth Aahaad. Ukiitazama Hadiyth hii kwa mtazamo huo, wanakubali kwamba ni wajibu kuifanyia kazi kwani inaeleza hukumu ya kishari’ah, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

 “Atake hifadhi kutokana na mambo manne katika tashahhud ya mwisho.”

 

Kwa upande mwengine inakusanya nukta ya ‘Aqiydah kwamba kaburini kuna adhabu na kuna fitna ya Masiyh Ad-Dajjaal lakini Hizbut-Tahriyr  hawaamini kuwepo adhabu za kaburini na hawaamini fitna za Masiyh Ad-Dajjaal ambazo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amezizungumzia katika Hadiyth nyingi ikiwemo aliposema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Hakuna fitnah mbaya toka kuumbwa kwa Aaadam mpaka kusimama Qiyaamah kwa Ummah wangu zaidi ya fitnah ya Masiyh Ad-Dajjaal.”

 

 

 

Hawaamini kuhusu Dajjaal kwa sababu Hadiyth zinazomhusu si Mutawaatir. Sasa tunawauliza mtafanyaje na Hadiyth ya Abu Hurayrah (kuhusu kuisoma hii du’aa katika tashahhud ya mwisho) kwa kuwa kwa upande mmoja imekusanya hukumu ya kisharia’h kwamba katika mwisho wa Swalah unatakiwa kusema “Na najikinga kwako kutokana na adhabu ya kaburi.” Je, utaomba hifadhi na adhabu ya kaburini wakati huiamini?

(Ufafanuzi wa Mfasiri: kwa maana, Unaamini kwamba inatakikana kusoma du’aa hii kwenye Swalah kwa kuwa kuisoma du’aa hii ni hukumu ya kishari’ah ambayo kwa mujibu wa Hizbut-Tahriyr inaweza kuchukuliwa toka katika Hadiyth Aahaad lakini ambacho mnachokisema katika du’aa hii yaani kuomba hifadhi kwa Allaah na adhabu ya kaburini ni jambo la ki-’Aqiydah ambalo kwa mujibu wa maelezo yenu haliwezi kuchukuliwa toka katika Hadiyth hii hii ambayo ni Aahaad sasa mtakubalije kuisoma du’aa hii halafu wakati huohuo hamuiamini?)

 

 

Vitu viwili vinavyopingana haviwezi kuwa pamoja.

 

 

Hivyo wametujia na vitimbi ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  amekataza vitimbi. Kwanini? Wanasema tunasema kwamba adhabu za kaburini ni kweli lakini hatuziamini. Falsafa mpya na ya ajabu. Kwanini wamefanya hivi? Kwa kuwa wamekuja na falsafa moja ambayo imewaingiza katika falsafa nyingine nyingi kiasi kwamba imewatoa katika njia ambayo walikuwa nayo Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Sasa nitaendelea na kama nilivyosema hii mada ni ndefu… kueleza kuwa Da’wah ya Hizbut-Tahriyr ambayo wamekuwa wakizungumza ni kuwa wanataka kusimamisha utawala wa Allaah duniani. Nitangulie kusema kwamba si wao peke yao wenye Da’wah hii, makundi na Madh-hab yote lengo lao kuu ni hili yaani kusimamisha utawala wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) duniani, hivyo hawako peke yao.

 

 

Swali limenijia sasa hivi na nilitaka kulichelewesha kwani linaweza kuuvuruga mtiririko wa uwakilishaji wangu lakini sitoliruka hili swali na nitalijibu nalo ni: Kuna Hadiyth ambayo inasema kwamba Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) alulizwa kuhusu kundi litakalookoka akasema wao ni “Jama’aah”.

 

 

Hadiyth hii ni sahihi na tunaiamini, lakini Hadiyth hii “Jama’ah” imefafanuliwa na Hadiyth tuliyoitaja.

 

 

Tutamaliza kikao hiki kwa kulijibu swali la mwisho. Na ninasema kuna Hadiyth mbili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa kuhusiana na kundi litakalookoka alijibu kwa masimulizi mawili. Kwanza ni hii niliyoitaja mda mchache kuwa ni “Watakaokuwa katika yale niliyokuwa nayo mimi na Swahaba wangu” na masimulizi mengine ni haya ambayo yamezaa swali, “Wao ni Jama’aah.”

 

 

Lakini nafikiri muulizaji anadhani kwa kuzingatia yale aliyoyasoma toka katika vitabu vya Hizbut-Tahriyr kwamba masimulizi haya yaani haya yanayotaja Jama’aah yanapingana na huo usimulizi mwingine nilioutaja.

 

 

Hivyo namwambia alikaribishe jibu hili karibu na nyumbani; hakuna kupingana katika masimulizi haya mawili. Hebu kwa mfano tuseme Hadiyth inayosema “Watakaokuwa katika yale niliyokuwa nayo mimi na Swahaba wangu” si sahihi na kwamba sahihi ni upokezi wa “Jama’aah” sasa je, Jama’aah ni kundi gani sasa hivi? Ni Hizbut-Tahriyr? Ni Ikhwaan Al-Muslimiyn? Ni Jama’aat At-Tabliygh?

 

 

Jibu ni:

“Jama’aah ni ile iliyosimuliwa kiusahihi toka kwa Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Yeyote atakayekuwa katika Haqq hata kama atakuwa ni mtu mmoja tu.” [Imepokelewa na At-Tirmidhiy].

 

  

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) alipotuma Rusuli na Manabii kuwabashiria watu na kuwaonya, walikuwa ni wao wenyewe lakini walikuwa ni Jama’aah. Ibraahiym alikuwa ni Ummah akiwa peke yake. Kwa hiyo alikuwa yeye mwenyewe kiuhalisia lakini alikuwa Jama’aah katika Da’wah yake na yeyote atakayefuata mwenendo wake, akapita katika njia yake atakuwa ni Jama’aah hata kama akiwa mtu mmoja peke yake. Kwa munasaba wa mjadala na tukiifanya kuwa Hadiyth iliyoelezea kundi litakalookoka haikuwepo kabisa, Jama’aah ni njia ya Waumini, Jama’ah ni Jama’aah ya Makhalifa waongofu.

 

 

Kwa hiyo Hadiyth ya Al-‘Irbaadh bin Saariyyah si simulizi mbili kama hizi tunazojadili wala haina shaka kwani mtu anaweza kuitilia shaka upokezi wake “Watakaokuwa katika yale niliyokuwa na Swahaba zangu.” Jama’aah ni njia ya Waumini ambayo nimekwishaielezea toka katika Kitabu na Hadiyth. Sasa kuna ubaya gani tukiielezea Jama’aah kwa maana ya Hadiyth ya kwanza: “Watakaokuwa katika yale niliyokuwa na Swahaba zangu?”

 

 

Kwa sababu Swahaba wake, (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio Waumini ambao atakayewapinga ameahidiwa kuingia motoni katika Aayah niliyoitaja hapo nyuma ambapo nilisema haitoshi kufuata Kitabu na Sunnah tu bali pia njia ya Waumini iliyotajwa katika Aayah inabidi iongezewe (kwenye Kitabu na Sunnah).

 

 

Kwa hiyo yeyote atakayedai Jama’aah iliyotajwa katika Hadiyth ya kundi litakaookoka ni kundi lake bila ya kuleta dalili ya Kitabu na Sunnah kuthibitisha hilo; kuthibitisha kwamba yupo katika yale waliyokuwa nayo Waumini wa mwanzo atakuwa ameifasiri isivyokuwa sahihi na atakuwa ameitafsiri Hadiyth hii vibaya.

 

 

Shaykh al-Albaani akaendelea: “Na nitamalizia mazungumzo yangu kwa kuwasimulia mjadala kati ya Salafi mmoja (akimaanisha yeye Shaykh Al-Albaaniy) na mtu mwengine aliyekuwa akilingania katika Kitabu na Sunnah lakini akawa hajui kuhusu nyongeza hii, yaani, ‘Kufuata njia ya Waumini’. Da’wah ya makundi ya Kiislamu haiwezi kuwa sahihi isipozingatia hili katika ‘Aqiydah yake na kisha kuitekeleza katika vitendo.

 

 

Nilimwambia: Jibu lako lina upungufu.

 

Akasema: Kwanini?

 

Nikamwambia: Kwa sababu kila Muislamu bila kujali amepinda kiasi gani au amenyooka kiasi gani husema ‘Mimi ni Muislamu’. Kwa mfano tutaanza na lililo rahisi kwanza. Anayefuata Madh-hab ya Hanafi akiulizwa wewe ni Madh-hab gani na akawa hataki kuingia kwenye malumbano atasema: ‘Madh-habu yangu ni Uislamu’, na anayefuata Madh-hab ya Ash-Shaafi’iy atasema hivyo hivyo ‘Mimi ni Muislamu…’ n.k.

 

 

Lakini wanaofuata Madh-hab ya Hanafi wanasema iymaan haiongezeki wala kupungua, wanaofuata Madh-hab ya Ash-Shaafi’iy wanasema iymaan inaongezeka lakini haipungui n.k. Hivyo jibu lako kuwa wewe ni Muislamu na jibu la mwengine anayesema yeye ni Muislamu halifafanui Madh-hab yako kwa ukamilifu. Hivyo alielewa akasema: ‘Basi nasema mimi ni Muislamu ninayefuata Kitabu na Sunnah.’

 

 

Nikamwambia: Vilevile Waislamu wengine wote wanasema hivyo hivyo hata hao niliowataja katika mfano niliokuonyesha, je, kuna anayefuata Madh-hab ya Hanafi anayesema, ‘Mimi ni Muislamu lakini sifuati Kitabu na Sunnah?’

 

 

Je, kuna Muibadhi miongoni mwa Makhawaarij waliopo zama hizi katika ardhi za Waislamu anayesema ‘Sifuati Kitabu na Sunnah?’ Au kuna Mshia yeyote; kuna Raafidhah yeyote anayesema ‘Sifuati Kitabu na Sunnah?’

 

 

Waislamu wote pamoja na khitilafu kubwa na nyingi walizo nazo wote husema, ‘Tunafuata Kitabu na Sunnah,’ lakini hakuna mwenye kusema, ‘Katika njia ya wema waliotangulia’ isipokuwa wale wenye kuifuata Manhaj ya wema waliotangulia. Na tunapoulizwa tunasema kuwa, “Mimi ni Salafi” mwisho wa mambo. Kwa sababu maana ya ‘Salafi’ ni kufuata Kitabu na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia. Nilipomueleza hili nikamwambia haitoshi kusema kuwa nafuata Kitabu na Sunnah kwa sababu makundi yote yanadai yanafuata Kitabu na Sunnah.

 

 

Akasema: Sasa nasema nafuata Kitabu na Sunnah…’ Kwa kuwa baada ya mhadhara huu alikubaliana nami hivyo akasema: “Nafuata Kitabu na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia.”

 

 

Nikamwambia nikijua kuwa yeye ni mwandishi wa vitabu, je hupati neno lolote la kiarabu ulilojifunza au kuandika linaloweza kufupisha majibu yako haya: “Nafuata Kitabu na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia?” Akanyamaza. Nikamwambia tunaposema, ‘Mimi ni Salafi’ haifupishi maelezo yako marefu ‘Nafuata Kitabu na Sunnah na…?’ Akajibu kuashiria kukubali.

 

 

Huo ndio ukweli kuhusu Salafi na hayo ndiyo makosa ya Hizbut-Tahriyr na makundi mengine yote… na mzunguko wa Da’wah yetu ndio mpana zaidi ya makundi mengine yote yaliyopo katika uso wa dunia.

 

 

Najua kuwa mfumo wa Hizbut-Tahriyr ni kwamba mwanachama wao akiwa na mtazamo tofauti na mtazamo wa kundi ukawa unapingana na mafundisho ya Hizbut-Tahriyr atafukuzwa na ataambiwa: “Wewe si katika sisi.’

 

Sisi hatusemi hivyo.

 

Najua kwa mfano, katika sera za Hizbut-Tahriyr mwanamke ana haki ya kupiga na kupigiwa kura, hivyo huwezi kukuta mwandishi miongoni mwa waandishi wa Hizbut-Tahriyr anayesema kuwa si katika majukumu ya mwanamke kujishughulisha na mambo hayo ambayo siku hizi huitwa siasa na kwamba anatakiwa ajifunze mambo yanayohusiana na jinsia yake ambayo yanaendana na maumbile yake, huruma yake n.k. Ama kuhusiana na kupiga na kupigiwa kura mwanachama wa Hizbut-Tahriyr  akiwa na mtazamo tofauti na huo atafukuzwa. Lakini sisi tunawakubali Hizbut-Tahriyr, Ikhwaanul Muslimiyn na Jama’aat At-Tabliygh lakini katika msingi wa:

 

 

 قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ ﴿٦٤﴾

Sema: Enyi Ahlal-Kitaabi! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, kwamba tusiabudu isipokuwa Allaah Pekee, na wala tusimshirikishe na chochote, na wala wasichukue baadhi yetu wengine kuwa miola badala ya Allaah. Wakikengeuka; basi semeni: Shuhudieni kwamba sisi ni Waislamu. [Aali-‘Imraan: 64]

 

 

Tunawalingania Waislamu wote kukubali msingi huu, na kuna makundi mengi yaliyotoka katika msingi huu, mengi sana. (Kama watakubali) watakuwa pamoja nasi, labda wanaweza kutofautiana nasi katika utekelezaji kwa sababu utekelezaji unahitaji elimu.

 

 

Tunasema kwa masikitiko makubwa makundi ya Kiislamu hayaipi elimu ya Kitabu na Sunnah umuhimu pamoja na hayo wanataka kusimaisha dola ya Kiislamu hali ya kuwa ni wajinga wa Uislamu wao. Hivyo tunasema:

 

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi. [Al-Ahzaab: 21]

 

 

Rasuli wa Allaah alianza kwa kuwafundisha watu na kuwaita katika ‘Aqiydah kwanza, kisha kwenye mambo ya ‘ibaadah na kuzijenga tabia zao na ndio historia hii inatakiwa kujirudia.

 

 

Na mpaka hapa inatosha, Wal-HamduliLLaahi Rabbil-‘Aalamiyn.

 

[Mawsu’atul-Allaamah, Al-Imaam, Mujaddidil-‘Aswr, Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy, cha Shaykh Shady Nu’maan, juz. 1, uk. 230-254.]

 

 

 

 

Share