Nimeolewa Huku Nina Mimba Nini Hukumu Ya Mtoto Wa Kitendo Cha Zinaa?

 

SWALI:

 

Asalaam Aleikum! 

Naomba kuelimishwa kuhusu yafuatayo:-

1)  Mimi nimeolewa na mimba ya miezi mitatu ya bwana huyo huyo alienioa:-

a)   Je, mtoto wangu halali au si halali?

b)   Kwa kuwa mtoto huyo ni wa kike, inshallah akijaaliwa kuolewa, huyu baba anaweza   kumuozesha?

c)   Je, mtoto huyu anaweza kurithishwa mali ya baba huyu?

Huyu mume wangu tangu tuoane, huu ni mwaka wa 19 na bado naishi nae na tushazaa watoto wengine wa kiume wawili.

Nitashukuru kwa kujibiwa masuala yangu. Wabillahi Taufiq.

  


JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

  

Shukran kwa swali lako  ambalo linahusiana na tatizo zito ovu lililoenea sana katika jamii yetu. Na ili sisi kuweza kuyaondoa ni lazima turudi vilivyo katika dini kwa kufuata Qur-aan  Tukufu na Sunnah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) la si hivyo basi tutakuwa na maisha ya dhiki hapa ulimwenguni na adhabu kali inatungoja kesho Akhera. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuwekea kanuni za kuweza kuingiliana baina ya mume na mke, nje ya mahusiano hayo inakuwa ni haramu.

 

Jambo la kwanza ambalo tunafaa kuelewa ni kuwa mwanamke hawezi kuolewa akiwa ana mimba mpaka azae kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kumwaga mbegu za uzazi juu ya mbegu nyengine. Na ikiwa mwanamke ana mimba anaweza kuwa ameipata hiyo mimba ima kwa sababu alikuwa na mume au zinaa. Ikiwa alikuwa ana mume, na mume ameaga dunia au amemtaliki ni lazima azae, na huko kusubiri azae ndiyo eda yake.

 

a.  Sasa kwa kuwa bwana huyo alikuoa ukiwa una mimba yake ambayo umeipata kabla ya ndoa, huyo mtoto utakayempata atakuwa ni wa zinaa. Na ilikuwa inatakiwa ndoa ifanyike baada ya kuzaa kwako. Kuolewa huko na hali una mimba ni makosa.

 

b.  Kishariy’ah kwa mujibu wa Wanachuoni wengi, huyu mtoto anayezaliwa akiwa ni msichana au mvulana si wa baba na akiwa ni wa kike baba huyo wa kidamu hawezi kutoa idhini ya kumuozesha.  

Lakini baadhi ya Wanachuoni wanaonelea kuwa mtoto bado atakuwa ni wa baba yake maadam anafahamika baba yake kiusahihi.

 

c.  Kwa mujibu wa Wanachuoni hao wanaoonelea kuwa mtoto ni wa mama, wanasema, baba na mtoto wa zinaa hawarithiani kabisa. Baba hamrithi mtoto wala mtoto hamrithi baba. Lakini mtoto anamrithi mama yake na mama anamrithi mtoto wake.

 

Jambo linalofaa nyinyi kufanya kwa sababu mumemkosea Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kuingia katika madhambi ni kurudi kwake na kumuomba msamaha, kuweka Niyah ya kutorudia tena kosa hilo na kufanya mema.

 

Na kadhalika ni kufunga ndoa upya kwa masharti yake kama yalivyo masharti ya ndoa.

Na tufahamu ya kwamba Allah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mwingi wa Kusamehe.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share