063-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Jiepushe Na Shaka, Kwani Halaal Na Haraam Imebainishwa, Moyo Ni Mfalme Wa Viungo

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 63

Jiepushe Na Shaka, Kwani Halaal Na Haraam Imebainishwa, Moyo Ni Mfalme Wa Viungo

Alhidaaya.com

 

 

           

عَن النُّعْمَانَ بْنَ بَشِيرٍ (رضي الله عنهما) قَال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ:  ((الْحَلاَلُ بَيِّنٌ وَالْحَرَامُ بَيِّنٌ، وَبَيْنَهُمَا مُتَشَابِهَاتٌ لاَ يَعْلَمُهَا كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ، فَمَنْ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ اسْتَبْرَأَ  لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ،  وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ وَقَعَ فِي الْحَرَامِ،  كَالرَّاعِي يَرْعَى حَوْلَ الْحِمَى َيُوشِكُ أَنْ يَرْتَعْ فِيهِ، أَلاَ وَإِنَّ لِكُلِّ مَلِكٍ حِمًى،  أَلاَ وَإِنَّ حِمَى اللَّهِ مَحَارِمُهُ، أَلاَ وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّه، وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ أَلاَ وَهِيَ الْقَلْبُ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa An-Nu’maan bin Bashiyr  (رضي الله عنهما) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Hakika halaal iko wazi na haraam iko wazi. Baina ya mawili hayo mna yenye kutia shaka. Wengi miongoni mwa watu hawayajui. Basi atakayejiepusha yenye kutia shaka, atakuwa amejiepushia shaka katika Dini yake na heshima yake. Na Atakayetumbukia katika yenye kutia shaka, ataingia kwenye haraam. Kama mchunga anayechunga kando ya mipaka, ni haraka kulisha humo [mpaka mwingine wa watu]. Zindukeni!  Kila mfalme ana mipaka. Zindukeni! Kwa yakini mipaka ya Allaah ni haraam Alizoziharamisha. Zindukeni! Kwa yakini katika mwili mna kinofu [cha nyama], kinapokuwa sahihi, mwili wote unakuwa sahihi. Kinapoharibika, mwili wote unaharibika. Zindukeni! Kinofu hicho ni moyo)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Dini ya Kiislamu imefunza na kubainisha kila jambo na shariy’ah zake. Hakuna jambo lililoachwa. 

 

 

Rejea pia: An-Nahl (16: 89).

 

 

 

2. Himizo la kufuata yaliyo halaal na kujiepusha na yaliyo haraam.

 

 

3. Kutokufuata matamanio ya nafsi na kujiepusha na mambo yenye shaka kwani huenda yakampeleka mtu kuingia katika ya haraam. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٧

Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayaat zenye maana wazi, hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo zisizokuwa wazi maana zake. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitnah (upotofu) na kutafuta maana zake zilofichika, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu husema: “Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Rabb wetu.” Na hawakumbuki ila wenye akili. [Aal-‘Imraan (3: 7)]

 

 

4. Muumin afuate yaliyo na dalili na aache yasiyokuwa na dalili ili ajiepushe na uzushi.

 

 

5. Allaah (سبحانه وتعالى) Ameweka mipaka ya shariy’ah Zake katika kila kitu na Ametahadharisha anayevuka mipaka. Mifano yake ni katika: Al-Baqarah (2: 187), (229), (230), An-Nisaa (4: 13), Al-Mujaadalah (58: 4), At-Twalaaq (65: 1).

 

 

6. Wito wa kuisalimisha nafsi kwa undani nao ni moyo, uwe ni wenye iymaan, taqwa, amani na uliosalimika na kila ovu, kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Atatazama katika nyoyo za watu. 

 

Rejea Hadiyth namba (1)

 

 

Rejea pia: Ash-Shu’araa (26: 88-89), Aal-‘Imraan (3: 91), Ghaafir (40: 19), At-Taghaabun (64: 4), Al-Mulk (67: 13).

 

 

7. Moyo ni mfalme wa viungo vyote, hivyo Muislamu anapaswa kuchunga moyo wake daima asifuate matamanio ili athibitike katika yanayomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى). Na hilo litaweza kupatikana tu lau tutayaendea ya ‘Ibaadah na kujiepusha ya haraam.

 

 

8. Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuzitakasa nyoyo zetu.

 

 

 

Share