064-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Wema Ni Tabia Njema, Na Dhambi Ni Yenye Shaka Katika Nafsi Na Kuchukizwa Na Watu

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 64

Wema Ni Tabia Njema, Na Dhambi Ni Yenye Shaka Katika Nafsi Na Kuchukizwa Na Watu

 

 Alhidaaya.com

 

 

 عَنْ النَّوَّاسِ بْنِ سِمْعَانَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((الْبِرُّ حُسْنُ الْخُلُقِ وَالإِثْمُ مَا حَاكَ فِي نَفْسِكَ وَكَرِهْتَ أَنْ يَطَّلِعَ عَلَيْهِ النَّاسُ)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa An-Nawwaas bin Sam’aan (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Wema ni tabia njema, na dhambi ni jambo lenye kutia shaka katika nafsi yako na ukachukia watu wasije wakalijua)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Maana ya Al-Birr ni aina zote za wema, hivyo asidharau mtu kufanya jambo lolote la kheri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖوَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾ 

Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi lakini wema ni mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na akawapa mali juu ya kuipenda kwake jamaa wa karibu na mayatima na masikini na msafiri na waombao na katika kukomboa watumwa na akasimamisha Swalaah, na akatoa Zakaah na watimizao ahadi zao wanapoahidi, na wanaosubiri katika dhiki za ufukara na maafa ya magonjwa na njaa na katika vita. Hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye taqwa. [Al-Baqarah (2: 177)]

 

 

2. Muislamu amesisitizwa kuwa na tabia njema, kwani itampatia manufaa Aakhirah, mojawapo ni kuwa karibu na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) huko Jannah kama ilivyothibiti katika Hadiyth.

 

Rejea Hadiyth namba (66), (127).

 

 

3. Kutambua kitendo cha dhambi ni kwa ishara mbili: Kwanza ni kusitasita katika nafsi, inapasa haraka uepuke nacho kitendo hicho. Pili ni kuchukia au kukhofu watu wengine wasije kujua kuwa unatenda jambo ovu. 

 

 

4. Hadiyth hii ni dalili kwamba nafsi imeumbwa katika "fitwrah" yaani, maumbile ya asili ya Kiislamu; yaani asili ya roho kuwa katika kutakasika bila ya kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى).  Anasema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

 ((Kila kinachozaliwa kinazaliwa katika Fitwrah…)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Rejea pia: Al-A’raaf (7: 172).

 

 

5. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Hamhesabii mtu kitendo kiovu kikibakia katika nafsi bila ya kukitenda. Ama pale anapokitenda, ndipo atakapokuwa ameingia katika dhambi. Ni Rahma pia kwamba kila jambo la kheri analolitilia niyyah Muislamu, lina thawabu japo kama hakuwahi kulitenda. Na anapolitenda hupata thawabu mara kumi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦٠﴾

Atakayekuja kwa ‘amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo. Na Atakayekuja kwa ovu basi hatolipwa ila mfano wake, nao hawatodhulumiwa. [Al-An’aam (6: 160)]

 

Na Hadiyth: ((Allaah Ameandika mema na mabaya. Kisha Akayabainisha. Basi atakayetia niyyah kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia niyyah kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya, ataandikiwa dhambi moja)).[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

6. Hadiyth hii ni miongoni mwa zinazojulikana kuwa ni: ‘Jawaami’ul-Kalim’ (Mjumuisho wa maana nyingi katika maneno machache) aliyopewa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

 

Share