Kuzuia Mimba Na Madhara Yake

 

SWALI:

Assalamu "alaykum,

Tunamshukuru Allah (S.W) kwa kutusaidia ndugu zenu inshaalah Mungu atakulipeni mema.

Suali langu, ni jee utumiaji wa mpira (Condom) wakati wa kuingiliana mke na mume inafaa kiislamu au haifai? Na je kama haifai ni kwa sababu gani? Na pia nataka kujua kama ina madhara fulani. Shukran.


 

 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

 Kabla ya kuingia katika swali lenyewe ni vyema tutazame historia fupi ya mipira (condom). Mipira ilitengenzwa hapo mwanzo kwa ajili ya kuzuia mimba na hivyo kumpatia fursa mama kuweza kujiuguza baada ya mazazi kabla ya kushika nyengine. Baadaye ulipoingia ugonjwa hatari wa UKIMWI mipira kama hiyo ilitumiwa kwa kuwakinga wagonjwa kuambukizana ugonjwa huo hatari.

Lakini shughuli hizi zote ziliondoka pale mataifa yaliyoendelea yalipotaka kueneza uasherati kwa wananchi wa nchi zingine katika ulimwengu. Na hili limeonekana wazi hasa katika mataifa ya ulimwengu wa tatu ambapo yanasaidiwa na mataifa ya kimagharibi ili kugawa mipira kama hiyo bure au kwa kununua kwa gharama ndogo sana. Kwa ajili ya kutolewa bure vijana ikiwa wameoa au wameolewa au hawajaoa au kuolewa, wamekuwa wakitekeleza tendo la mapenzi kwa sababu ya kutolewa hofu kuwa kwa kuvaa hiyo mipira watakuwa wamejikinga na ukimwi. Zinaa ilikithiri na athari yake kwa jamii ikawa kubwa kama inavyoonekana sasa.

Mpira wenyewe si haramu isipokuwa matumizi yake ndiyo yanaweza kupelekea katika uharamu. Mfano wake ni kama kisu ambacho uharamu na uhalali unategemea matumizi yake. Ukikitumia kumuua mtu basi kitendo kile kitakuwa ni haramu, lakini kikitumiwa katika kumchinja mnyama wa halali au kwa matumizi ya jikoni basi kutakuwa hakuna tatizo lolote. ndio ipo kanuni katika Fikihi inayosema: “Chochote kinachopelekea katika haramu, pia kinakuwa haramu”. Na Uislamu kawaida unaziba uwazi wowote wa kumpeleka mtu katika haramu, ndio Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akasema:

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” ().

Allah hapa Hakusema msizini bali Amesema msikaribie kumaanisha jambo lolote ambalo linaweza kumpeleka mtu katika zinaa pia halifai. Na ndio Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatueleza kuwa zinaa ya macho ni kuangalia ya haramu, zinaa ya miguu ni kutembea kuelekea yalipo haramu, zinaa ya masikio ni kusikia, na sehemu za siri kuyakinisha hilo au kukataa. Ndio mshairi wa hivi karibuni alisema: “Mwanzo mtu anatizama, kisha anatabasamu, kisha kutikisa kichwa, kisha maagano na mwisho ni uharara wa kitanda”.

Hivyo, ikiwa ni kuingilia kwa mume na mke wa halali kutumia mpira haina tatizo lolote kwani wanazuoni wamechukua Qiyaas ya ile njia iliyokuwa ikitumiwa na Maswahaba katika zama za Mtume wa Allah (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), nayo ni Azl (kumwaga mbegu za uzazi nje wakati wa kushusha).

Jaabir ibn ‘Abdullah (Radhiya Llaahu ‘anhu) anasema tulikuwa tukifanya azl na Qur-aan inateremka na Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asitukataze hilo (al-Bukhaariy na Muslim).

Na Swahaba mmoja alimuomba Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ruhusa ya kufanya Azl, naye akamwambia ya kwamba atakachokileta Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) hakuna awezaye kukizuia.

Lakini jambo ambalo lafaa lieleweke ni kuwa ni lazima kuwe na maridhiano baina ya mume na mke bila ya mke kulazimishwa katika hilo. Jambo ambalo linaeleweka ni kuwa kuvaa mpira katika kutenda tendo la ndoa kunapunguza matamanio na inakuwa wanandoa hawapati ile ladha ambayo inafaa ipatikane, kwa sababu ngozi zao hazigusani.

Tanbihi ni kuwa ikiwa nia ni kuchelewesha kuzaa kwa mke kwa sababu ambazo zinakubalika kisheria, njia hii si thabiti ya kuzuia mimba. Na kwa utafiti uliofanywa ni kuwa utumiaji wa mpira hauzuii mwanamke kupata ukimwi.

Kwa faida zaidi, bonyeza viungo vifuatavyo:

Njia Gani Inayopasa Katika Sheria; Kuzuia Au Kupanga Uzazi?

Kupanga Uzazi Na Sio Kuzuia Uzazi

Nimeshauriwa Kuzuia Uzazi Na Daktari

Utumiaji Kondom Kwa Mke Anaedai Kuwa Ni Mgonjwa

Utumiaji Wa Mpira (Condom)

20 Kuhalalishwa ‘Azl (Kuchopoa Kabla Ya Kushusha)

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share